Wednesday 17 January 2018

SASA UMEHITIMU ELIMU YA CHUO KIKUU

Image result for university graduate
Kwanza kabisa nikupongeze kwa hatua uliyofikia, najua umekumbana na vikwazo vingi lakini haukukata tamaa ndio maana umefikia hatua hiyo.
Mnamo mwaka 1975,Hayati Mwalimu J.K Nyerere wakati anakifungua rasmi chuo kikuu cha Dar es salaam alisema Maneno yafuatayo,
Nanukuu
"UNIVERSITY IS A PLACE WHERE PEOPLES MIND'S ARE TRAINED FOR INDEPENDENT THINKING AND PROBLEM SOLVING, SHORT OF THAT, THAT IS NOT A UNIVERSITY"

Tafsiri
Mwalimu alimaanisha Chuo kikuu ni mahali ambapo akili za watu hufundishwa kuwa na fikra za kujitegemea na kutatua matatizo, pungufu ya hayo hicho sio Chuo kikuu.
Hivyo basi kuna mambo mawili ambayo Mwalimu aliyachukulia kama sifa kubwa za msomi wa ngazi ya Chuo kikuu ambayo ni,

1.Fikra za kujitegemea ( Fikra huru).
2.Kutatua matatizo.

Ni dhahiri kabisa kwa kiasi kikubwa jamii kubwa ya wasomi leo imezikosa sifa hizo mbili na kinyume chake wasomi wengi wamekuwa chanzo cha matatizo na sio watatuzi wa matatizo, pia wasomi wengi ndio wenye fikra tegemezi.
Kwa kiasi kikubwa jamii ya leo inaangushwa na wasomi kwa sababu mbili,
1.Wasomi kutotambua wajibu wao hivyo kushindwa kuutimiza.
2.Wasomi kutambua wajibu wao ila kutenda tofauti na vile wanavyotakiwa kufanya.

Leo hii wasomi ndio wanaoongoza kulalamika na kulaumu kila hali wanayoiona mbele yao, wanailaumu serikali, mazingira na chochote kile wanachofikiri ni chanzo cha kushindwa kwao.
Jamii kwa ujumla imegubikwa na sintofahamu na tegemeo lao kubwa wanakusubiri wewe msomi utoe suluhisho la sintofahamu hiyo.
Si sahihi, si vyema, si haki kama msomi usipoamka, kujitambua na kubadilika ili uanze kuleta matokeo chanya kwenye jamii yako.

HUU NI USHAURI WANGU KWAKO MSOMI.
1.Kuhitimu digrii isiwe fimbo ya kuwachapia wengine ifanye mbeleko iwabebe wengine, acha dharau, acha kiburi, acha kujikweza wakati huu unapoinuliwa ndio wakati wa kunyenyekea sana wafanye wengine waone umuhimu wa usomi wako.
2.Badala ya kuwatishia wenzako kwamba ukutane nao baada ya miaka kadhaa, anza kusaidiana na wenzako kwa ushauri na vitendo ndipo utakapofanikiwa, acha tabia ya ubinafsi na uchoyo ukiona fursa washirikishe na wenzio.
3. Jenga fikra za kujitegemea, usibebwe na kila upepo, acha tabia ya kulaumu na kunung'unika bali jifunze kufikiri zaidi ya changamoto unazoziona wakati wengine wanakesha kuzijadili changamoto wewe fikiri suluhisho la changamoto hizo.
4. Haijalishi upo bado nyumbani au popote pale, jambo lolote unalotakiwa kulifanya lifanye kwa uaminifu, ufasaha na ustadi mkubwa lina maana kwenye maisha yako ya baadae.
5.Ongeza thamani katika ujuzi wako
Mfano kama wewe ni mwalimu anza kuandika vitabu, kama umesomea biashara anza kuuza kitu chochote kidogo, kama wewe ni daktari anzisha hata kikundi cha watu wape ushauri kuhusu afya.

6.Ukipata fursa ya kujifunza jambo jipya usisite ipo siku litakusaidia.
7.Fikiri mbele zaidi ya ajira, kushindwa kuajiriwa kusikufanye Ukawa kama mfu buni jambo litakalokufanya uzalishe "UNAWEZA KUKOSA AJIRA LAKINI HAUWEZI KUKOSA KAZI YA KUFANYA.
8.Fikiri, waza, nena, tenda sawasawa impasavyo msomi kuwa, vitendo vyako siku zote viwe vya kujenga na kuigwa.
9. Kumbuka elimu uliyoipata ni zawadi tu sio kwamba ulistahili sana, kumbuka kulipa fadhila kwa kuisaidia jamii yako kutatua changamoto zinazowakumba, jitahidi kuwasaidia wengine pia.
Kuna utofauti kati ya "To be grown up na to be grown older"
Ndugu mhitimu jionyeshe kama umekua na sio umeoongezeka tu miaka.
JAMII INAKUSUBIRI NA INAKUTEGEMEA. FUNGA MKANDA SAFARI NDIO INAANZA

-Mwl Kihwaga

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA