Tuesday, 17 June 2014

**UNYAMA MKUU*** MTOTO ATESWA SIKU 730! ANGALIA PICHA


Mtoto Melina wa (15) aliyefika katika Jiji la Dar es Salaam mwaka 2012 akitokea kijijini Ishozi- Kiziba, Kagera kwa lengo la kufanya kazi za ndani, yaani ‘hausigeli’ akiwa amejeruhiwa vibaya na bosi wake anayefahamika kwa jina moja la Yasinta.
SIKU 730 au miaka miwili ya unyama na ukatili uliombatana na vipigo mfululizo, vimempa wakati mgumu katika maisha mtoto wa miaka 15, Melina aliyefika katika Jiji la Dar es Salaam mwaka 2012 akitokea  kijijini Ishozi- Kiziba, Kagera kwa lengo la kufanya kazi za ndani, yaani ‘hausigeli’Melina amelazwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi) ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar baada ya kujeruhiwa vibaya usoni na kichwani na bosi wake anayetajwa kwa jina moja la Yasinta ambaye ni mwanasheria mkubwa nchini.

Tukio hilo la kusikitisha, lilijiri Ijumaa iliyopita nyumbani kwa mwanamke huyo, Boko-Magengeni jijini Dar ambako Melina alikuwa akifanyia kazi.
Majeraha ya kichwani aliyopata mtoto Melina baada ya kupigwa na kwanja la kufyekea nyasi.
Binti huyo ambaye wakati anafika jijini Dar alikuwa na miaka 12, licha ya umri wake kuwa mdogo alifanya kazi kwa bidii ili mshahara wake uweze kuwasaidia wazazi wake ambao hawajiwezi kimaisha kule kijijini.
SAKATA ZIMA LA MELINA 
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Melina alichukuliwa na bosi wake huyo kwa makubaliano ya mshahara wa shilingi  40,000 kwa mwezi huku shilingi 20,000 zikitumwa nyumbani kwao Kagera.

“Lakini katika hali ya kushangaza, bosi wake alikuwa hampi zile shilingi 20,000 kama makubaliano yao yalivyokuwa akisema kwamba anamtunzia kuepuka matumizi mabaya.
“Ikaelezwa kuwa, akiwa ndani ya kazi, binti huyo alijikuta akipata mateso makubwa kama vile kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili kwa madai ya kukosa, kufanya kazi vibaya au tofauti na maelekezo,” kilisema chanzo.
Melina akiendelea kuuguza majeraha akiwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi) ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar baada ya kujeruhiwa vibaya usoni na kichwani na bosi wake.
BINTI MWENYEWE ANASIMULIA
Akizungumza kwa uchungu akiwa hospitalini hapo, Melina anaanza kwa kusema:
“Nimechoka sana ndugu zanguni, nimeteseka sana, nisaidieni nirudi kwetu Kagera. Kosa dogo napigwa na blenda na nyaya za kompyuta. Ndiyo maana sehemu mbalimbali za mwili hadi kichwani nina makovu kama hivi.

“Mara hii ya mwisho nilipigwa na kwanja la kufyekea ndiyo majeraha haya. Wakati akinitesa bosi wangu alikuwa akiniambia hakuna wa kumtisha. Nisaidieni jamani, miaka miwili ya mateso  mfululizo sasa nataka kurudi kwa wazazi wangu japokuwa hawana uwezo tutaishi hivyohivyo tu. “

MAKOVU 73 KICHWANI, MWILINI
Mbali na majeraha mapya, mtoto huyo ana makovu (majeraha yaliyopona) 73 kichwani na mwilini mwake ambayo yote yanadaiwa yalitokana na adhabu ya mashambulizi ya kudhuru mwili ingawa haikubainika kama ni kutoka kwa bosi wake huyo au la!

...Sehemu ya bega aliyojeruhiwa mtoto Melina.
SIKU YA TUKIO
Juni 11, mwaka huu, saa 3 usiku, Melina alipelekwa  katika hospitali binafsi iliyopo Mbezi, Dar akiwa na majeraha makubwa kichwani.

Aliambatana na wanawake watatu, mama Betty, mama Winnie na mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Rwechungura.
Walisema wao ni majirani wanaoishi karibu na binti huyo na walifika hospitalini hapo kwa lengo la kumsindikiza na kujua nini kinaendelea.
DAKTARI NA MELINA
Habari zinadai kuwa, daktari aliyekuwa zamu usiku huo alishtushwa na hali ya Melina kwani alikuwa akitokwa na damu nyingi usoni na kichwani.
Aliwatoa wanawake hao nje na kumuuliza Melina nini kilimpata ambapo alijibu: “Nilianguka na  ndoo ya maji.”

...Sehemu ya mkono aliyoumizwa.
Daktari alimbana sana ndipo akapasua jipu kwamba alikuwa amepigwa na bosi wake na kwamba hata makovu mengine ni majeraha yaliyopona ambayo yalitokana na kipigo cha mara kwa mara.
DAKTARI AOMBA NAMBA ZA SIMU
Ikadaiwa kuwa, daktari huyo aliomba namba ya simu ya mmoja wa wale wanawake lakini walikataa na kumuomba daktari atoe yake wao ndiyo wangempigia.

SAKATA LATINGA POLISI
Habari zinazidi kudai kuwa, daktari huyo aliendelea kuokoa maisha ya Melina kwa kumshona nyuzi karibu kumi na mbili katika maeneo yaliyopasuka  lakini kutokana na hali ya majeruhi kuwa mbaya, ilibidi aende kutoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi cha Kawe. 

“Polisi walikwenda nyumbani kwa mwanasheria huyo, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida walikuta nyumba haina mtu tena ikiwa wazi kwa usiku huo.
“Inasemekana katika wale wanawake watatu waliompeleka Melina hospitali, mtuhumiwa alikuwepo ila alitoroka baada ya polisi kuonesha nia ya kumkamata.
“Hali ya Melina ilizidi kuwa mbaya. Alfajiri ya Juni 12, mwaka huu ilibidi ahamishiwe kwenye Hospitali ya Mwananyamala ambapo alipokelewa na kupewa matibabu. Hali ikazidi kuwa mbaya, akahamishiwa Muhimbili.
POLISI WAKIRI, WAMKAMATA MTUHUMIWA 
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,  Camillius Wambura alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kwamba, mtuhumiwa alitoroka lakini Jumamosi iliyopita alitiwa mbaroni maeneo ya Mbagala jijini Dar.

NI HAUSIGELI WA PILI 
Tukio la Melina ni la pili, wiki  mbili zilizopita, hausigeli mwingine, Yasinta Lucas alikumbwa na kadhia kama hiyo. Yeye alilazwa Hospitali ya Mwananyamala akidaiwa kuteswa, ikiwemo kung’atwa meno na bosi wake kwa kumtuhumu kutofanya kazi vizuri.

Bosi huyo alishapandishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar, Juni 12, mwaka huu na kusomewa mashitaka ya kujeruhi.
-GPL

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA