KAMA KWELI UNAHITAJI MWENZI WA MAISHA: HII INAKUHUSU
Ni njia gani za kumpata mwenzi wa maisha yako? Inawezekana unakabili mtihani mzito, hujui ni yupi wa nafsi yako. Bila shaka unamtaka yule wako wa kufa na kuzikana.
Mada hii inakuja na suluhisho mahsusi kwako, kumjua mapema anayekufaa, anayeweza kudumu nawe maishani. Zingatia kwamba mwenzi sahihi wa maisha yako ni hatua muhimu kuelekea kwenye mafanikio.
KWANZA TAMBUA HILI
Uhusiano wa kimapenzi ni suala binafsi. Kwanza kabisa ni sanaa inayokutaka uangalie mahitaji yako mwenyewe. Je, unahitaji nini kwa mtu ambaye ungependa awe mwenzi wa maisha yako?
Yale unayotaka kutoka kwa mtu ambaye unapenda awe mwenzi wa maisha yako, unapaswa kuyapa kipaumbele. Hata siku moja, usithubutu matamanio ya mwili na moyo yakupe mwongozo wa kumwona umpendaye.
NANI MWENZI WA MAISHA?
Ni swali ambalo unapaswa kujiuliza. Kwa uwazi kabisa, unatakiwa kuzingatia kuwa mwenzi wa maisha ni yule ambaye utachangia naye mambo mengi kwa uaminifu na maelewano makubwa.
Mwenzi wa maisha si mtu unayeweza kuwa naye kwa mantiki ya kupeana tulizo la ngono unapohitaji au kampani ya kwenda kuangalia ‘muvi’, muziki, ufukweni na kwingineko unapoona huhitaji kuwa peke yako.
Mwenzi wa maisha ni yule atakayefanya ujione umekamilika, bila kujali ‘ubize’ wala ukapa ambao pengine unao ndani ya jamii inayokuzunguka.
Kingine cha kuzingatia ni kwamba, mwenzi wa maisha yako ni yule ambaye anakukubali na kukupenda kama ulivyo, bila kuwepo kwa nyongeza ambazo zitatokana na kukubadilisha kutoka yule wa zamani.
Kupata mwenzi wa maisha mwenye sifa kamili, ni sawa na kupatia herufi ya mwisho kwenye mchezo wa kubahatisha. Kwa maana hiyo, baada ya kumpata, kila kitu kinakuwa kimekamilika maishani mwako.
NANI MWENZI WA MAISHA YAKO?
Pointi ya msingi kuzingatia ni kwamba unahitaji kuwa na yule anayekubalika ndani ya nafsi yako. Hivyo basi, fikiria kwa yale yanayoweza kukufanya uwe na furaha, pia yanayoweza kukupa huzuni.
Zingatia mapitio yako ya nyuma kuona ni kwa namna gani yamekutengeneza mpaka kufika ulivyo sasa. Jiulize pia kuhusu ndoto na malengo yako siku za usoni.
Ikiwa tu utaweza kutambua mahitaji na matarajio yako ya kimaisha, bila shaka utaweza kutambua ni mtu gani anayefaa katika kukusaidia kutimiza kila kilichomo ndani ya malengo yako.
JENGA IMANI
Kutafuta mwenzi wa maisha siyo suala la kuangalia mtu wa kwenda naye klabu kujirusha usiku. Vile vile ni muhimu kutambua kwamba inaweza kukuchukua muda kupata mtu wa kukidhi vigezo vyako.
Pamoja na ukweli huo, bado unatakiwa uwe na imani kwamba itafika wakati utasahau habari za kutafuta mwenzi na utakuwa mwenye furaha, ukijipongeza kwa kumpata anayekufaa.
Mapenzi ni mchezo lakini ni rahisi kuucheza ukitambua kanuni zake. Hii ina maana kuwa unapokuwa kwenye kipengele hiki, unakuwa na jukumu moja zito la kuhakikisha unampata yule mwenye uwezo wa kukonga moyo. Mwenye sura ya kutimiza malengo yako.
Hata hivyo, muhimu kwako ni kuwa mtulivu na kuacha macho yafanye kazi ya kuangaza kwa utaratibu, halafu akili ifanye kazi ya kutathmini kiwango cha huyo atakayeonwa.
Kitu kingine ambacho unatakiwa kuheshimu ni kuwa, wawili wanaopendana, kila mmoja kwa nafasi yake ni nusu ya kitu kizima kinachoitwa ndoa au wapenzi, hivyo wanapounganishwa ndiyo kinapatikana kitu kizima.
Ukiamini kuwa wewe ni nusu na utakamilika baada ya kukutana na mwenzi wako, unachotakiwa kufanya ni kujenga imani kwamba mwenzi wako yupo sehemu kwa ajili yako, hivyo endelea kumtafuta na siku moja utamuweka mikononi mwako.