Friday 17 July 2015

HII NDIO HISTORIA YA MZEE OJWANG ,IJUE SABABU YA KIFO CHAKE


Marehemu Mzee Ojwang 

Nairobi, Kenya. Siku 4 baada ya gwiji wa kuvunja mbavu kutoka Kenya, Benson Wanjau `Ojwang’ kuaga dunia katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta, mchekeshaji mwingine aliyekuwa akifanya kazi kwa ukaribu kabisa na Mzee huyo (kama mkewe), Mary Khavere `Mama Kayai’, amesema ingewezekana kabisa kuokoa maisha ya mzee huyo lakini alipuuzwa na hakuna aliyekuwa akisikia kilio chake cha muda mrefu.
Mama Kayai ambaye ni mmoja kati ya wachekeshaji wa vipindi maarufu vya Vitimbi na Vioja Mahakamani, ameuambia mtandao wa Standard Digital kwamba Marehemu Ojwang, ambaye aliacha kuonekana kwenye upeo wa wadau wa vichekesho mara baada ya kuanza kuugua macho mwaka mmoja uliopita, alikuwa akilalama] siku za mwishoni mwa maisha yake, lakini hakuna aliyekuwa akimfuatilia.
“Inauma sana kusikia huyu mzee ambaye ni baba wa wachekeshaji nchini amefariki, lakini kinachouma zaidi ni kwamba mzee ameomba sana msaada lakini hakuna ambaye alijitokeza mpaka alipofikia hali mbaya zaidi”, alisema kwa masikitiko Mama Kayai.
Akionekana kuwa na hisia kali za majonzi alisema ni watu wachache ambao leo wanaweza kujitokeza na kusema hawajawahi kupata huduma nzuri ya vichekesho ya Mzee Ojwang lakini wengi wao wamewahi kumuona na kumfurahia, ingawa katika siku za mwishoni mwa uhai wake hakupata ushirikiano wa kutosha, kuokoa maisha yake.
Mzee Ojwang, amefariki bila ya kukutana ana kwa ana na rais wake, Uhuru Kenyatta, mtu ambaye alikuwa akiomba na kuomba itokee siku wakutane ili aongee naye japo kwa dakika chache.
Alichougua
Mwanzoni mwa mwaka huu, Mzee Ojwang alipata tatizo la macho na Seneta wa Jiji la Nairobi Mike Sonko alichukua jukumu la kumpeleka Hospitali ya Loresho ambako alifanyiwa upasuaji na tatizo hili lilisababisha gwiji huyo kupotea kabisa kwenye picha za runinga.
“Tangu hapo alikuwa katika hali nzuri tu na alikuwa akiishi maisha ya furaha nyumbani lakini kwa kuwa hakuwa na kazi, kuna wakati maisha yalikuwa magumu na akawa analazimika kuomba msaada kwa jamaa”, alieleza mke wake, Augusta Wanjiru
Wanjiru alisema baada ya upasuaji, kiafya hakuwa na hali mbaya ingawa jumatatu iliyopita, alianza kulalamika anaumwa akawa anatapika mara kwa mara, hali ambayo wenyewe hawakuitilia wasiwasi.
“Jumamosi usiku alianza kulalamika tumbo, na ilipofika Jumapili ikabidi tumpeleke hospitalini na akakutwa na homa ya mapafu na alifariki jioni yake,” alieleza mama huyo kwa masikitiko.
Binti yake, Patricia Njeri alisema kwamba mwili wa baba yake, ulitolewa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa ya Kenyatta na kuhamishiwa katika vyumba vya kampuni rasmi ya mazishi Kenya iitwayo Lee Funeral Home ya jijini Nairobi kusubiri mipango ya mazishi.
Ojwang katokea wapi?
Ojwang aliyezaliwa Nyeri mwaka 1937, alipata elimu ya msingi katika shule ya kanisa iliyoitwa Purnwani Missionary na baada ya kufaulu mitihani yake mwaka 1952, alijiunga na Kagumo High School.
Mzee Onjwang alikuwa ni mwanamahesabu hatari. Ingawa aliacha shule akiwa kidato cha pili tu kutokana na matatizo ya kiuchumi.
Kazi ya kwanza kufanywa na Mzee Ojwang ilikuwa ni kufua katika kampuni ya White Rose Dry Cleaners iliyopo eneo la viwanda jijini Nairobi.
Aliingiaje kwenye sanaa?
Uchangamfu wake na maneno ya kufurahisha alipokuwa kazini kwake vilisababisha watu wengi waamini kwamba yeye ni mchekeshaji bora, wakamshauri aingie kwenye fani hiyo kwani ndiyo haswa, iliyomstahili. Naye bila kinyongo akajiunga na kundi la Tausi Drama Club lililopo Bahati Estate Nairobi miaka ya 1970.
Hakuna aliyemkataa kipindi hicho na kila alipofanyiwa jaribio aliwaacha hoi waliokuwa wakimsaili kwa jinsi alivyoweza kuwavunja mbavu.
Kabla ya kuwa mchekeshaji aliwahi pia kujaribu kucheza mpira huko Makongeni, alikokulia, wakati wazazi wake wakifanya kazi katika Kampuni ya Reli ya Kenya.
Ojwang, alifanya kazi na kundi la Tausi kwa miaka 10 kabla ya kukutana na Mama kayai mwaka 1980, wakiwa wasanii wa majaribio wa kipindi kipya cha televisheni kilichoitwa Darubini. Kipindi hiki kiliwapa yeye na wenzake fursa ya kufanya ziara nchini Ujerumani ambako walifunguka kifikra.
Kipindi cha Darubini ndicho kilichobadilishwa jina na kuitwa Vitimbi, mwaka 1985 na mpaka leo kinaonekana katika kituo cha Televisheni cha KBC.
-MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA