Wednesday 5 August 2015

JE UMETENDWA NA UNATAKA KUANZISHA MAHUSIANO MAPYA? SOMA HAPA


UHALI gani mpenzi msomaji wa FUNGUKA LIVE BLOG.
Ni dhahiri kwamba asilimia kubwa ya watu kabla ya kufikia kwenye hatua ya kufunga ndoa, wanakuwa wamepitia maumivu mengi. Wanatendwa vya kutosha.

Wanakuwa na ‘majeraha’ ya kutosha. Kuna ambao huenda mbali zaidi kimawazo hadi kufikia hatua ya kusema ‘sitapenda tena.’ Hivyo ndivyo mapenzi yalivyo!

Kwenye kipindi cha kutendwa, inahitaji akili ya ziada kung’amua kwamba unapaswa kufanya nini na kwa wakati gani. Ukikurupuka utaambulia maumivu. Unahitaji suluhisho la kutendwa lakini  mwisho wa siku unaambulia maumivu makali zaidi.

Unaachana na huyu, unaamua kuanzisha uhusiano mwingine haraka ili kupunguza maumivu bila kujua huyo unayemfuata naye ni tatizo zaidi ya lile la awali.

Unakuwa umeruka majivu na kukanyaga moto. Kwa sababu tu ya kutotuliza akili yako. Unaingia kwenye penzi ambalo linakupa ‘stress’ zaidi ya lile la awali, maumivu yake yanakuwa ni mara mbili ya yale ya awali.

 Hapo ndipo unapojikuta unatoa kauli za majuto. Unakosa amani. Unatamani dunia ipasuke na wewe uingie ndani.

Ili usiambulie maumivu hayo, unapaswa kujifunza mambo yafuatayo  kabla ya kuanzisha penzi jipya.

Jiulize ni sababu gani zilizokufanya uumizwe. Je, wewe ndiyo chanzo cha kutendwa kwako? Mpenzi wako wa awali alikuwa na sifa za kuwa mchumba na baadaye kuwa mume?

Ukitafakari hapo kwa makini, utapata jibu. Litakusaidia sana siku za usoni. Utagundua ulikosea wapi. Kama mtu huyo hakuwa mkweli, hakuwa na penzi la dhati, utakuwa umeshajifunza na kumjua mtu mwenye mapenzi ya kweli ana sifa gani.

Lazima umtambue mapema mwenzako ana malengo gani na wewe. Siku zote sura ya mtu huwa haifichi kile kilichomo ndani ya moyo wake. Anayekupenda toka moyoni utamjua tu.

Acha papara ya kuingia kwenye uhusiano mpya. Jiridhishe kwanza katika maeneo yote. Historia ya mtu kitu kigumu kukipata. Kupitia marafiki, ndugu na jamaa zake utaweza tu kumjua ni mtu wa aina gani.

Mchunguze kupitia watu wanaomzunguka. Hata kama ataficha ‘makucha’ yake lakini kupitia watu wake utaweza kumjua yeye ni mtu wa aina gani.

Haiwezekani mtu akawa na marafiki wapole, wacha Mungu, yeye akawa mkorofi. Mkorofi anakuwa na wakorofi wenzake. Chagua mtu ambaye unaona ana sifa njema kama ulizonazo wewe.

Kama uliingia kwenye penzi lake pasipo kujua historia ya unayeanzisha naye uhusiano, utakuwa umejifunza. Usikubali tena kuingia katika uhusiano na mtu bila kujua historia yake. Wengi ni matapeli, unapaswa kumjua mtu vizuri kabla ya kuanzisha naye safari.

Yawezekana tatizo lilikuwa ni dini. Aliamua kukuacha kwa sababu alijua hawezi kukubadilisha. Akakupotezea muda na kukuacha solemba, hilo nalo uwe nalo makini. Ukiona mnapishana dini na mwenzi wako na unauona ugumu wa nyinyi kukubaliana, ni vyema ukaacha kuingia penzini.

Ni hatari kuanzisha uhusiano na mtu ambaye mmetofautiana imani bila kuwa na mwanga wa suluhisho hilo. Ukiona kuna tatizo hilo na mwenzako anajifanya kulipotezea, usikubali. Unapaswa kujiongeza haraka.

Yawezekana halizungumzii kwa sababu hana malengo na wewe. Ameshaona kizingiti hivyo anaamua tu kukuhadaa kwa maneno mazuri kumbe moyoni anatafuta au anaye anayemfaa.

Kikubwa kuliko mambo yote niliyoyaainisha hapo juu ni Mungu. Mtangulize yeye kwa kila jambo. Kwa imani yako, muombe akupe mke au mume mwema, uombe kwa kumaanisha.

Omba wakati na wewe kweli umejiweka katika mazingira ya kumpata mume au mke mwema.

 Kwa leo ni hayo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. 

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA