MISRI YAFUNGUA TENA KIVUKO CHA RAFAH KWA MUDA .
Misri imeufungua tena leo kwa muda wa siku tatu tu na kwa ajili ya masuala maalumu mpaka wake wa pamoja wa ardhini na Ukanda wa Gaza wa ardhi za Palestina baada ya kuufunga kwa muda wa siku 50.
Hayo yameelezwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya serikali halali ya Palestina inayoongozwa na harakati ya HAMAS, yenye makao yake huko Gaza. Kwa mujibu wa wizara hiyo, mpaka huo kupitia kivuko cha Rafah umefunguliwa kwa ajili ya watu wanaohitaji huduma za matibabu, wanafunzi wanaoelekea masomoni, raia wa kigeni na kwa ajili ya baadhi ya kesi maalumu za masuala ya kibinadamu. Serikali ya Misri imeweka vizuizi vikali katika kivuko cha Rafah tangu jeshi lilipomuondoa madarakani Rais halali wa nchi hiyo Muhammad Morsi anayetoka kwenye harakati ya Ikhwanul Muslimin yenye mfungamano na Hamas.
Aidha jeshi la Misri limebomoa mamia ya njia za chini kwa chini katika mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na eneo la Gaza ambazo zimekuwa zikitumiwa na Wapalestina kupitisha vifaa vya ujenzi na fueli na kusababisha eneo hilo kukosa nishati ya umeme kwa muda wa hadi masaa 16. Siku ya Jumanne iliyopita, Filippo Grandi, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) alitoa wito kwa Misri kufungua kivuko cha Rafah na pia akautaka utawala wa Kizayuni wa Israel ulegeze mzingiro ulioliwekea eneo la Ukanda wa Gaza kwa muda wa miaka minane sasa…/
0 comments:
Post a Comment