Thursday, 24 April 2014

Polisi yawapiga ‘stop’ tena Ukawa Zanzibar


Dar/Arusha. Jeshi la Polisi Zanzibar limeendelea kuuchelewesha mkutano wa wanachama wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa madai kwamba hakuna askari wa kutosha kuulinda.
Awali, mkutano huo ulipangwa kufanyika Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Kibandamaiti, Unguja lakini jeshi hilo liliuzuia kwa madai ya kuwapo kwa habari za kiintelijensia dhidi ya tishio la maisha ya watu.
Awali, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema mkutano huo utafanyika leo katika uwanja huo.
Ukawa ni muungano wa vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, DP na wajumbe 25 kutoka kundi la wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, Msemaji wa Polisi Zanzibar, Mohamed Mhina alisema baadaye kuwa mkutano huo hautafanyika hadi Aprili 30, mwaka huu.
Alisema umezuiwa kwa sababu askari na maofisa wa polisi wanaotakiwa kuusimamia wako Dar es Salaam katika maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Tumekutana nao (CUF walioomba kibali kwa niaba ya Ukawa) na kukubaliana kwamba mkutano huo ufanyike Aprili 30 kwani askari waliopo hivi sasa ni wachache hawawezi kutosha kusimamia ulinzi kutokana na aina ya mkutano wenyewe. Hata hiyo siku hiyo hakutakuwapo na maandamano, bali wataruhusiwa kufanya mkutano pekee na siyo vinginevyo.”
Katibu wa Ukawa nje, Shaweji Mketo alisema wamekubaliana na jeshi hilo... “Aprili 30 tutafanya mkutano pale Kibandamaiti na siku inayofuata tutafanya mkutano Pemba.”
Wafuta mikutano ya Lema
Aidha, mkoani Arusha polisi wamefuta mikutano ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema iliyopangwa kufanyika katika kata za Daraja Mbili na Moshono.
Barua ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Giles Muroto, imesema CCM pia imeomba kufanya mikutano kwenye kata hizohizo na tarehe muda huohuo.

Alisema CCM Arusha kiliandika barua Aprili 19, mwaka huu kuomba mikutano hiyo wakati Lema aliomba kibali siku mbili kabla na kukubaliwa.
“Itakuwa siyo busara kuruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama viwili vinavyopingana kisera, maudhui na mtazamo katika eneo, muda na siku zinazofanana,” alisema Muroto.
Akizungumzia hatua hiyo, Lema alisema huo ni uthibitisho wa madai yake ya siku zote kuwa polisi wilayani Arusha wamekuwa wakitumiwa kisiasa na CCM kukabiliana na nguvu ya ushindani wa kisiasa kutoka vyama vingine.
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA