Wanafunzi wa Sekondari Mtwara walala sakafuni
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi. Dk. Shukuru Kawambwa
Wanafunzi 68 kati ya 556 wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bweni katika Manispaa ya Mtwara-Mikindani, wanalazimika kulala chini kutokana na upungufu wa vitanda.
Shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha sita na mabyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma, pia haina uzio, jambo ambalo wananchi hupita eneo la shule hata nyakati za usiku.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Ernest Mwongi, aliyasema hayo alipokuwa akisoma taarifa ya shule hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi vitanda 32 vilivyotolewa na Benki ya Posta tawi la Mtwara.
Mwongi alisema kuwa hivi sasa shule ina vitanda 210 wakati mahitaji halisi ni vitanda 278.
"Hii ni shule tunaitegemea kwa kiwango kikubwa hapa mkoani kwetu. Kwa mfano, mwaka jana, kati ya wanafunzi 76 waliohitimu kidato cha sita, 75 walifaulu na kujiunga na elimu ya juu na vyuo mbalimbali," alisema.
Aliongeza: "Bado tuna matumaini makubwa na shule hii, wanafunzi wa kidato cha sita tunaowategema kuanza mitihani yao Mei 5, mwaka huu, wameonyesha kiwango kizuri katika mitihani yao ya majaribio kwa kupata nafasi ya pili kwa Kanda ya Kusini na kuwa shule ya kwanza kimkoa."
Awali akikabidhi vitanda hivyo, Meneja wa Benki ya Benki ya Posta tawi la Mtwara, Omary Kilimo, alisema benki hiyo imeamua kuunga mkono mpango wa serikali wa kutekeleza Matokeo Makubwa Sasa.
“Benki ya Posta ni ya kizalendo na kwa kutambua uzalendo wetu, tumeamua kutumia faida kwa kununua vitanda 32 vyenye thamani ya Shilingi milioni 5.7 kwa ajili ya kusaidia watoto wa Kitanzania,” alisema.
Aidha, Kilimo aliziomba taasisi za fedha mjini hapa kuangalia namna ya kuisaidia shule hiyo ambayo bado ina upungufu wa vitanda na uzio.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile, alisema kuwa serikali ina kila sababu ya kutunga sheria ya kuzibana kampuni za uwekezaji ambazo zimekuwa hazitoi kwa wananchi faida inayopatikana.
"Kuna kampuni kubwa zinazopata faida kubwa, lakini bado haziwasaidii wananchi. Hii siyo sawa kabisa ni jukumu la serikali kuangalia namna ya kuzibana kampuni ambazo hazitumii faida yake kusaidia jamii," alisema Ndile.
Kuhusu suala la uzio wa shule, Munila Abbdillah, mwanafunzi wa kidato cha tano, alisema kuwa wananchi wamekuwa wakipita katika maeneo hayo licha ya uongozi wa shule kuendelea kukemea suala hilo.
Uzio ni tatizo kubwa hapa shuleni kwetu, lakini tunamshukuru Mungu wanafunzi hawatoroki, tumekuwa tukijifundisha sisi wenyewe namna ya kujilinda na kujitunza kama watoto wa kike," alisema Abdillah.
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mtwara, ilianzishwa mwaka 1956 wakati ikiwa na darasa la tano hadi sita.
Hata hivyo, mwaka 1962, shule hiyo ilianza kudahili wananfunzi wa sekondari.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment