NABII MPYA AIBUKA JIJINI DAR....ANATIBU HOMA YA DENGUE KWA KUNYWA JUISI....ANASEMA HOMA HII HAIAMBUKIZWI NA MBU BALI NI PIGO TOKA KWA MUNGU

aarifa za kuwepo kwa nabii huyo anayejulikana kwa jina la Yaspi
Bendera, kumefanya baadhi ya wagonjwa kuanza kumiminika katika kanisa
lake la Ufunuo kwa Watu Wote lililopo eneo la Yombo Buza-Kipera, Wilaya
ya Temeke, wengine wakidaiwa kutoka hospitalini, kwenda kupata
‘uponyaji’.
Lakini serikali imeonya dhidi ya vitendo vya baadhi ya watu
kuwaondoa wagonjwa hospitalini na kuwapeleka kwenye maombi, ikisema mtu
yeyote anayesababisha wagonjwa kuondolewa hospitalini kwa ajili ya
kwenda kufanyiwa maombi atachukuliwa kuwa ni adui namba moja katika
jitihada za kupambana na ugonjwa huo na kusisitiza kuwa wagonjwa ni
lazima kwanza watimize dozi wanazopewa na wataalamu hospitalini ndipo
waendelee na imani zao.
Wakati wataalamu wakisema kuwa ugonjwa huo unatokana na mbu
aina ya aedes egypti, Nabii Yaspi anadai kuwa homa ya dengue ni pigo
lililoletwa na Mungu kwa watu wasiotaka kumtii.
Nabii huyo alidai kuwa alionyeshwa na Mungu miezi miwili iliyopita
kuwa homa ya ugonjwa huo ingeibuka nchini na kwamba itawaathiri zaidi
watu wazima kuliko watoto.
Alidai kuwa moyoni ana siri nzito ambayo atamwambia mkuu wa nchi
peke yake na iwapo atakosa fursa ya kufanya hivyo, hatamwambia mtu
mwingine.
“Nina siri ambayo nataka kumwambia Rais Jakaya Kikwete na
tayari nimeshaomba kukutana naye. Kama akikataa sitamwambia mtu mwingine
yeyote,” alisema.
Nabii Yasp alitoa madai hayo huku ugonjwa huo ukiwa ushaua watu
sita na wengine 600 kuugua katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha,
Shinyanga, Zanzibar na Lindi.
Inadaiwa kuwa mpaka sasa, nabii huyo ameshaponya watu sita kwa kutumia kinywaji cha juisi na maombi.
“Kuna mgonjwa wa dengue alikuja kanisani Jumapili kuombewa
akitoka wodini Muhimbili, baada ya maombezi alipona kabisa na sasa ni
mzima,”alisema.
Inadaiwa kuwa mgonjwa huyo aliambiwa na nabii anyanyuke
akashindwa, lakini baada ya kunyweshwa juisi hiyo na kuombewa aliulizwa
kitu gani hawezi kufanya na ambacho angependa kufanya wakati huo, ndipo
mgonjwa alijibu kuwa alitaka kutembea, nabii alimwambia “simama
utembee”.
Katika hali isiyo kuwa ya kawaida, Emmanuel badala ya kutembea alianza kukimbia kwa furaha akizunguka kanisani.
Baada ya tukio hilo, mgonjwa huyo aliambiwa arudi hospitali akawajulishe madaktari kuwa amepona.
Mgonjwa alirudi Hospitali ya Muhimbili kutolewa mpira kama
alivyokuwa ameshauriwa na nabii. Siku tano baadaye alikwenda kanisani
kumshukuru Mungu, huku akisimulia namna alivyowashawishi wagonjwa
wengine wa dengue kwenda kunywa juisi ya muujiza.
Kauli ya serikali ya mkoa
Lakini, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amekemea
kitendo hicho akisema mtu yeyote anayesababisha wagonjwa watolewe wodini
kwa ajili ya kwenda kuombewa, atachukuliwa kuwa adui namba moja dhidi
ya jitihada za serikali za kutokomeza ugonjwa wa homa ya dengue.
Sadiki alisema mgonjwa anayetaka kwenda kuombewa aende baada ya
kumaliza dozi aliyoandikiwa na siyo kuondoka hospitalini na kuacha dawa.
“Sitaki kuiingilia imani, lakini kumtoa mgonjwa hospitali akaombewe hilo silikubali,” alisema
mkuu huyo wa mkoa na kuongeza kuwa baadhi ya watu wameanza kupotosha
wananchi kuwa majani ya mipapai yanatibu ugonjwa huo.
Mganga Mkuu Hospitali ya Temeke
Mganga mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dk Silvia Mamkwe alisema ni vyema
watu wakaheshimu imani zao, lakini siyo sahihi mgonjwa wa homa ya
dengue kuacha dawa kwa sababu ya maombi.
Alisema sheria za manispaa zipo wazi kabisa kuhusu taratibu
zinazotakiwa kufuatwa kwa mtu anayetaka kumtoa mgonjwa wodini, kwa hiyo
ni kosa mgonjwa kuondoka wodini kwenda kuombewa.
>>Mwananchi
0 comments:
Post a Comment