Friday 4 July 2014

SHEHE AKERWA NA SWAUMU ZA KINA WEMA SEPETU,SNURA NA MASTAA WENGINE


SHEHE Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum ameonesha kukerwa kwake na mastaa wa Bongo ambao ni Waislam na wanaishi na wenza wao bila ndoa, hasa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.

Akizungumza na mwandishi wetu juzi, Shehe Alhad alisema kwa mujibu wa imani ya Dini ya Kiislam, Muislam hupaswa kufunga mwezi mtukufu kama hana matatizo ya kiafya.
Alisema kwa wale Waislam ambao wapo katika uhusiano usio wa ndoa nao hutakiwa kujiandaa kwa mwezi huo wa toba kwa kutengana na wenza wao mpaka mfungo utakapomalizika.

Shehe huyo aliongeza kuwa ni makosa kwa Muislam kufunga akiwa anaishi na mpenzi wake pasipo ndoa na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo ni sawa na kushinda na njaa.
“Mwislam yeyote asiye katika ndoa lakini akafunga mwezi mtukufu hali akiwa anaishi na mpenzi wake ni bure na suala hilo ni sawa na kujikalisha na njaa tu.  Hata kama hawatashiriki zinaa lakini tunaambiwa tusiikaribie zinaa.
“Hivyo lazima atengane na mpenzi wake huyo kwa kukaa naye mbali na kusiwe na mawasiliano ya kimapenzi kati yao,” alisema Alhad.

Wakali katika tasnia ya filamu Bongo Wema Sepetu na Snura Mushi.

Kwa kusema hivyo, Shehe Alhad aliwagusa mastaa wa Bongo ambao wanajulikana kuwa na uhusiano wa kimapenzi lakini hufunga kila ufikapo Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Baadhi ya mastaa wasio kwenye ndoa lakini wamefunga mwezi huu walizungumza na waandishi wetu ambapo walidai kutimiza masharti ya mwezi huo kwa kutengana na wenzi wao, baadhi yao ni:-
Snura Mushi ambaye yupo katika uhusiano wa kimapenzi na Dj Hunter wa Maisha Club mkoani Mbeya, amesema:
“Mwenzangu yupo Mbeya hivyo tumetengana. Nilijiandaa miezi miwili kabla kwa ajili ya kufunga mwezi huu. Huwa tunawasiliana tu kwa salamu na mambo ya kawaida.”

Mkali katika tasnia ya filamu Bongo Rose Ndauka.

Zuwena Mohammed ‘Shilole’ ambaye pia yupo katika uhusiano na dogo Mbongo Fleva, Nuhu Mziwanda naye amefunguka: “Naipenda sana dini yangu ndiyo maana nimetengana na mwenzangu kwa sasa. Tunazungumza jioni tena baada ya kufuturu.”
Rose Ndauka, yeye yupo kwenye uhusiano na mzazi mwenziye, Malick Bandawe:
“Yah mimi mwenyewe nimefunga na mwenzangu naye amefunga, tumetengana mimi nimerudi kwa mama mpaka mwezi uishe. Huwa tunapigiana simu kwa ajili ya kunijulia hali yangu na ya mtoto.”
Wema Sepetu hakupatikana kwenye simu, lakini na yeye yupo kwenye uhusiano na Mbongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ wote wakiwa kwenye imani inayowataka kufunga mwezi huu kama hawana matatizo ya kiafya.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA