SERIKALI KUTUMIA TSH. BILIONI 5 KUHUDUMIA KAMBI ZA MADAKTARI BINGWA WA MOYO
PICHA TOKA MAKTABA |
Na Nyakongo Manyama
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 5 katika mwaka 2015/16 kwa
ajili ya kuhudumia kambi za Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo ili kurahisisha
upatikanaji wa huduma za matibabu ya magonjwa hayo kwa Watanzania.
Lengo la mkakati huo ni
kuhakikisha Wagonjwa wengi wanahudumiwa katika kipindi kifupi pamoja na
kupunguza gharama za kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, ambao wengi wao husafiri
kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya moyo, figo na saratani.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Dkt. Donald Mmbando wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Dkt. Mbando alisema katika wiki
ya kwanza iliyoanza wiki hii Madaktari hao wanatarajia kutoa huduma kwa
wagonjwa 20 na kuifanya Serikali kuokoa kiasi cha Tsh. Milioni 500 ambazo
zingetumika kuwasafirisha wagonjwa hao nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
“Tumeokoa kiasi cha Tsh. Bilioni
1 zilizopaswa kutumika kuwapeleka nje ya nchi wagonjwa hawa, tutahakikisha kuwa
Wataalamu hawa wanafanya kazi kwa pamoja na Madaktari wetu ili waweze
kuwajengea uwezo katika kutibu magonjwa haya”
alisema Dkt. Mmando.
Alisema Serikali pia ipo katika
mchakato wa kuzijengea uwezo hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Taasisi ya
Kansa ya Ocean Road na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kuziwezesha
hospitali hizo kuwa na Wataalamu na majengo ya kisasa kwa ajili ya kutoa huduma
za matibabu kwa Watanzania.
Aidha alisema Serikali imepanga
kufanya mazungumzo na taasisi za kiraia na nyingine ikiwemo taasisi ya Rotary Club
zilizokuwa zikisafarisha watoto wenye matatizo ya ugonjwa wa moyo, kuwekeza
nguvu nchini kwani Tanzania kwa sasa ina wataalamu wa kutosha kwa ajili ya
kuwatibu wagonja hao.
Kwa mujibu wa Mmbando alisema
magonjwa ya moyo ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, hivyo aliwataka
Watanzania kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuacha kunywa
pombe na uvutaji wa sigara na kutazama desturi za ulaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi
ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Prof. Mohammed Janabi alisema katika kipindi cha
wiki mbili ambazo madaktari hao watakuwepo hapa nchini wanaweza kuhudumia jumla
ya wagonjwa 55, na hivyo kuifanya Serikali kuokoa kiasi cha Tsh. Bilioni 1.2.
MAELEZO,
Dar es salaam.
02/12/2015.
0 comments:
Post a Comment