NIGERIA:JESHI LABADILI KAULI KUHUSU WANAFUNZI WALIOTEKWA NA BOKO HARAM
Jeshi la Nigeria limekanusha taarifa ya awali kuwa baadhi ya
wanafunzi wa shule waliotekwa nyara kutoka Chibok na wapiganaji wa Boko Haram,
wameachiliwa.
Msemaji wa jeshi nchini Nigeria, Meja Generali Chris
Olukolade, ameambia BBC kuwa wanawahifadhi wasichana kadhaa lakini akakana kuwa
wasichana hao ni baadhi ya wale waliotekwa nyara na wapiganaji wa Boko Haram
kutoka Chibok.
Zaidi ya wasichana 200 walitekwa nyara na Boko
Haram kutoka
shule ya mabweni Kaskazini Mashariki mwa jimbo la Borno.
Utekaji nyara huo ulisababisha ghadhabu kote nchini Nigeria
na duniani kote kiasi cha kusababisha kampeini ya kutaka kuokolewa kwa
wasichana hao kwenye mitandao ya kijamii.
Maandamano yenye kauli mbiu, (#BringBackOurGirls)
yaliandaliwa kutoa wito kwa watawala kuongeza juhudi za kuwanusuru wasichana
hao,
Muda mfupi baada ya kuwateka nyara,Boko Haram, ilitoa kanda
ya video wakisema kuwa wasichana hao wataachiliwa tu ikiwa serikali itakubali
kuwaachilia wapiganaji wa kundi hilo ambao wanazuiliwa.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ripoti ambazo
hazijathibitishwa zikisema kuwa serikali ya Nigeria imekuwa ikifanya mazungumzo
na Boko Haram, kubadilishana wasichana hao na wapiganaji wao wanaozuiliwa.
Tangu kutolew kwa amri ya kutotoka nje nyakati za jioni,
katika eneo la Kaskazini Mashariki kwa lengo la kutatiza harakati za Boko
Haram, kundi hilo limekuwa likiendeleza mashambulizi.
Wanawake wengi na watoto, wakiwemo wasichana wamekuwa
wakitekwa nyara.
Awali, Generali Olukolade aliambia BBC kuwa shughuli
inaendelea ya kuwaokoa wasichana hao na kwamba baadhi ya wasichana haio wako
salama katika kambi za jeshi.
Hata hivyo msemaji huyo baadaye alisema kuwa jeshi
linajaribu kuwatambua wasichana hao ambao wako chini ya ulinzi wa jeshi lakini
hawakurejea kutoka Chibok.
-BBC
-BBC