POLISI ALIYEUA MWANAFUNZI WA CHUO KIKUU JIJINI MBEYA AHUKUMIWA KIFO
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mbeya imemhukumu kunyongwa hadi kufa polisi wa upelelezi, Maduhu, F 5842, aliyekuwa akikabiliwa na shitaka la mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), Daniel Mwakyusa.
Aidha,
mahakama hiyo imewaachia huru washitakiwa wengine wawili wa kesi hiyo,
polisi wa upelelezi, Shaaban, F 7769, na polisi wa kike mpelelezi,
Neema, F 6545, baada ya kuwakuta hawana hatia.
Hukumu hiyo ya
kesi namba 16 ya mwaka 2013, ilitolewa jana mjini hapa na Jaji Rose
Temba, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili.
Awali,
ilielezwa mahakamani hapo na mawakili wa serikali, Archiles Mulisa
akisaidiwa na Catherine Paul kuwa washitakiwa walifanya mauaji ya
kukusudia Februari 14 mwaka 2012 kinyume cha Kifungu Namba 196 cha
Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa Marejeo mwaka 2002.
Mulisa
alidai washitakiwa hao kwa pamoja walihusika na mauaji ya Daniel
Mwakyusa baada ya kumpiga kwa kutumia silaha inayodhaniwa kuwa ni
bunduki, nje ya ukumbi wa starehe wa Universal uliopo Uyole jijini
Mbeya.
Akitoa hukumu ya kesi hiyo, Jaji Temba alisema anawaachia
huru mshitakiwa namba mbili, Shaaban ambaye alikuwa dereva wa gari ya
polisi kwa kuwa ushahidi uliotolewa, unadhihirisha kuwa alibaki ndani ya
gari akimsubiri mshitakiwa namba moja aliyeshuka na kuingia kwenye
ukumbi wa Universal.
Kwa upande wa mshitakiwa namba tatu, Neema,
Jaji Temba alisema aliridhishwa na mshitakiwa huyo kutohusika na mauaji
kwa kuwa siku ya tukio alikuwa akijisikia vibaya, hivyo alilazimika
kubaki na dereva kwenye gari.
Jaji Temba alisema mshitakiwa namba
moja, Maduhu, anahusika moja kwa moja na mauaji hayo, kutokana na
ushahidi wa kimazingira, kwani yeye ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho
kuondoka na Daniel Mwakyusa eneo la tukio na kumpeleka kwenye gari.
Alisema
sababu ya pili, ushahidi ulionesha kuwa silaha yake pekee ndiyo
iliyotumika, tofauti na za askari wengine kwa kuwa risasi tatu
zilionekana kupungua kati ya zile alizokabidhiwa sambamba na ushahidi wa
maganda matatu ya risasi, yaliyookotwa eneo la tukio.
Jaji Temba
alisema sababu ya tatu ni kuwa ushahidi uliotolewa, unaonesha kuwa
mshitakiwa huyo alikuwa wa mwisho kurejesha silaha, hivyo kuhusishwa
moja kwa moja na mauaji hayo.
Alisema kutokana na sababu hizo,
mahakama inamtia hatiani kwa kuua kwa kukusudia, hivyo mshitakiwa
Maduhu, amehukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Awali, ilidaiwa kuwa
siku ya tukio ilikuwa Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day), ambapo
mtuhumiwa akiwa doria na askari wenzie, alimkuta Daniel Mwakyusa akiwa
kwenye eneo la starehe na mwanamke anayesadikiwa kuwa alikuwa pia na
mahusiano na askari huyo.