Thursday, 21 May 2015

AMEKUSALITI, LAKINI BADO UNAMPENDA?



Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kukutana tena na wewe msomaji wangu mpendwa wa safu hii nzuri ambapo tunajuzana, kushauriana na kuelimishana kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi.

Mada yetu ya leo, kama inavyojieleza kwenye kichwa cha habari, ni mambo unayopaswa kuyafanya unapogundua mpenzi wako amekusaliti wakati bado unampenda na unahitaji kuendelea kuwa naye katika uhusiano wa kimapenzi.

Vitabu vya dini zote vinaeleza kuwa kosa pekee linaloweza kuivunja ndoa, hata ile iliyofungwa kwa baraka za Mungu, iwe ni madhabahuni au msikitini, ni USALITI. Yaani hata kama ulikuwa unampenda vipi, ikitokea amekusaliti na umegundua ukiwa na ushahidi, una haki zote za msingi za kutoa/kudai talaka au kuachana kabisa (kama bado hamjaoana).

Hata hivyo, kuna mazingira ambayo yanaweza kukutokea, ukagundua mkeo, mumeo, mchumba au mpenzi wako amekusaliti lakini kutoka ndani ya moyo wako, ukawa haupo tayari kuachana naye kwa sabahu bado unampenda sana licha ya kwamba amekukosea.

Kutokana na maombi maalum ya wasomaji wangu kadhaa ambao wamekutana na hali kama hiyo na hawajui cha kufanya, ndiyo maana leo nimeamua tuijadili mada hii na wewe msomaji wangu.
Naamini mimi peke yangu sijui kila kitu wala ushauri wangu hauwezi kuwa wa mwisho lakini nataka kukushirikisha wewe msomaji wangu, hebu niambie utafanya nini unapotokewa na tukio kama hili? Unampenda kwa moyo wako wote, umemfanyia mambo mengi lakini mwisho ukagundua kuwa amekusaliti, utafanya nini?

Mapenzi yamegeuka shubiri, usaliti na maumivu ya moyo yamegeuka na kuwa sehemu ya kawaida katika uhusiano wa kimapenzi. Watu wengi wanalia kwa sababu wanasalitiwa au waliwahi kusalitiwa na wenzi wao, si wanawake, si wanaume, si wanandoa, si wachumba wala wapenzi!

Zipo sababu nyingi zinazosababisha usaliti lakini lengo langu leo siyo kuzungumzia hilo bali ni kujaribu kuiponya mioyo ya wote waliojeruhiwa na watu wanaowapenda sana kwa kuwasaliti.
Yawezekana ulitokea kumpenda sana mwenzi wako, ukaamini wewe ndiyo kila kitu kwake, ukamtimizia kila kilichokuwa ndani ya uwezo wako lakini mwisho, ukaambulia maumivu baada ya kugundua kuwa yupo mwingine anayekuibia mali zako.

Sitaki kupingana na maandiko ya vitabu vitakatifu au sheria ambazo zipo wazi kwamba malipo ya usaliti ni kuvunjika uhusiano lakini nataka tujadiliane, ni lazima kila unapogundua kuwa mwenzi wako amekusaliti dawa yake ni kupeana talaka au kuachana kwa ugomvi?

Mathalani umefunga ndoa na kuishi na mwenzi wako kwa kipindi kirefu mkipendana, kujaliana na kuoneshana kila aina ya mahaba lakini akateleza na kukusaliti ilihali bado anakupenda na wewe unampenda, utakapoamua kuachana naye na kwenda kwa mwingine, ukigundua naye anakusaliti utafanya nini? Utaachana na wangapi?

Siyo mara zote talaka au kuachana huwa suluhisho la usaliti ndani ya ndoa. Siwafundishi watu wasaliti ndoa zao au uhusiano wao kwa makusudi wakitegemea kusamehewa, hapana.
Nataka uelewe kwamba hata baada ya mwenzi wako kukusaliti, bado mna nafasi ya kuendelea na maisha yenu ikiwa wote wawili mtaamua kulishughulikia tatizo hilo kwa kina bila kujali watu wa nje wanasemaje.

Usikilize moyo wako, ni kweli amekusaliti! Amekuumiza, unahisi dunia yote imekuelemea, unatamani kufa au kuua, lakini je, moyo wako unakuambia nini? Upo tayari kumruhusu mwizi wako ndiyo awe mmiliki halali wa mwenzi wako ambaye bado unampenda?

Unaweza kuniandikia maoni yako nami nitakujibu..Asante

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA