Azam FC leo wameweza kuibuka na ushindi wa goli 1-0 mbele ya KCCA ya Uganda kwenye mchezo wa kundi B michuano ya Kagame inayoendelea kutimua vumbi jijini Dar es Salaam mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jioni ya leo.
John Bocco ‘Adebayor’ aliifungia Azam goli pekee lililoipa timu yake ushindi mwanzoni wa kipindi cha kwanza. Baada ya ‘Wanalambalamba’ kupata goli hilo walitawala kipindi hicho wakicheza soka la pasi nyingi fupifupi na mara chache walipiga mipira mirefu.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Azam wakiwa mbele kwa goli 1-0 dhidi ya KCCA ya Uganda ambayo ilitafuta kwa udi na uvumba goli la kusawazisha lakini ukuta uliokuwa ukiongozwa na Pascal Wawa akisaidiana na Said Morad pamoja na Agrey Morris ulikuwa haupitiki kirahisi.
Kipindi chapili hakikuwa kikali kama kipindi cha kwanza kwasababu timu zote zilitengeneza mashambulizi machache, Azam wakilinda zaidi goli lao na kutengeneza mashambulizi machache ya kuvizia.
Azam walifanya mabadiliko kwa kuwaingiza Kipre Tchetche, Jean Mugiraneza pamoja na Mudathir Yahya lakini kuingia kwao hakukubadili matokeo kwani hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika, Azam wakafanikiwa kuungana na KMKM ya Tanzania visiwani kuibuka na ushindi baada ya wawakilishi wengine wa Tanzania (Yanga) kupoteza mchezo wao wa ufunguzi dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
0 comments:
Post a Comment