FAHAMU KUHUSU ATHARI NA KUEPUKA SHINIKIZO LA DAMU
Tarehe 7, Aprili kila mwaka, dunia huazimisha Siku ya Afya Duniani.
Shirika la Afya Duniani(WHO) hutoa kipaumbele katika uchaguzi wa magonjwa yanayosumbua dunia kwa kufanya kampeni ya mapambano dhidi ya magonjwa hatari yanayoleta changamoto katika jamii.
Ulimwenguni pote, shinikizo la damu linakadiriwa kusababisha vifo vya mtu mmoja kati ya kila watu wazima watatu wenye umri wa kuanzia miaka 25.
Watu bilioni moja duniani huathiriwa na ugonjwa wa shinikizo la damu. Kiharusi ni miongoni mwa vitu vinavyochangia kwa kiasi kikubwa matatizo ya shinikizo la damu na kupooza.
Kwa pamoja maradhi haya husababisha vifo na ulemavu kwa kiasi kikubwa.
Shinikizo la damu kama yalivyo maradhi mengine ya jamii hiyo, huua na kuacha madhara kwa mamilioni ya watu duniani.
Inakadiriwa kuwa, mwaka 2008 takribani watu 17.3milioni walikufa kwa magonjwa ya moyo.Huku 40% ya watu wazima wakipatwa na ugonjwa huu kwa mwaka 2008.
Asilimia 80 ya vifo vinavyotokana na Magonjwa yasiyoambukiza kwa vimetoka katika maeneo ya daraja la chini na kati kiuchumi hasa katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara.
Shinikizo la damu ni nini?
Shinikizo la damu ni msukumo wa damu ulio juu kuliko inavyotakiwa na kubaki katika hali hiyo kwa muda mrefu.Msukumo wa damu huhitajika mwilini ili kusambaza chakula,oksijeni na kutoa uchafu.
Kwa mujibu wa WHO msukumo wa kawaida kwa mtu mzima ni muhimu kwa ajili ya kulisha chembe hai za chakula,oksijeni na kuondoa uchafu.
Mtu kuwa na ugonjwa huu ni kujiweka n katika hatari yakupata shambulio la moyo,kiharusi na figo kushindwa kufanya kazi. Iwapo ukishindwa kukabili shinikizo la damu madhara zaidi hutokea kama vile upofu,mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio na moyo kushindwa kufanya kazi.
Hatari ya kupatwa na madhara ya shinikizo la damu, kama niliyoorodhesha huwa zaidi sana kwa wale wanaugua kisukari , umri unavyozidi kusogea hatari ya ugonjwa huu huongezeka,inakadiriwa watu wenye umri wa miaka 20-30 kati ya watu 10 mmoja hupata shinikiza la damu, na pia watu waliofikisha miaka50 kwa kila watu 10 watano hupata shinikizo la damu.
Idadi ya wagonjwa wa shinikizo la damu inazidi kuongezeka katika nchi za Afrika hasa zenye kipato kidogo kiuchumi kutokana na mtindo wa maisha, msongo wa mawazo na milo.
Hatari ya kupata shinikizo damu inaweza kupungua endapo utapunguza kula chumvi nyingi, kula mlo kamili, epukana na unywaji pombe uliopitiliza,mazoezi ya mwili mara kwa mara, linda uzito mwili ulionao usiongezeke na pia epukana na utumiaji tumbaku.
WHO katika siku ya afya duniani imeweka lengo kuu,ambalo ni kuwa na tahadhari zaidi, mienendo na tabia bora za kiafya, kuimarisha utambuzi na uwezeshaji wa kimazingira.
Nia na madhumuni ya lengo kuu la siku ya Afya Duniani 2013 ni kupunguza shambulio la moyo na kiharusi. Pia yapo malengo maalum kama vile;
Kwanza Kuongeza ufahamu zaidi katika mambo yanayosababisha shinikizo la damu na matokeo yake hapo baadaye.
Lakini pia kutoa taarifa zaidi kwa jamii namna ya kujikinga na shinikizo la damu na madhara yanayoambatana nayo.
Kuwapa msukumo zaidi watu wazima kufanya uchunguzi wa kitabibu wa mara kwa mara kuangalia msukumo wao wa damu.
Kuwa na mwamko binafsi namna ya kujikinga na shinikizo la damu na kurahisisha upatikanaji wa upimaji wa msukumo wa damu na gharama nafuu ili kila mtu anufaike na huduma ya upimaji.
Lakini pia, who inasisitiza serikali kubuni uwezeshaji wa kimazingira kwa ajili ya mienendo bora kiafya.
Dalili
Mara nyingi huwa hamna dalili zozote na kama zikiwepo mgonjwa huwa na dalili zifuatazo:
1. Uchovu
2. Maumivu ya kichwa
3. Kuhisi mapigo ya moyo kwenda haraka
4. Kichefuchefu
5. Kutapika
6. Damu kutoka puani
7. Kutoweza kuona vizuri (blurred vision)
8. Kusikia kelele masikioni
9. Na mara chache kuchanganyikiwa
Vipimo na uchunguzi
Huhitaji kupima angalau mara tatu kwa wiki moja ili kujua iwapo mgonjwa ana shinikizo la damu . vipimo hufanyika kwa kutumia kifaa kinachoitwa kitaalamu Sphygmomanometer. Vipimo vingine ni:
1. Damu ili kuchunguza wingi wa lehemu mwilini (cholesterol), na pia vitu kama (BUN, na electrolytes)
2. Kipimo cha mkojo (Urinalysis)
3. ‘ultrasound’ ya figo
Matibabu
Lengo ni kuzuia madhara ambayo yanaweza kuletwa na shinikizo la damu.
Jinsi ya kuzuia shinikizo la damu
1. Chakula cha afya kisicho na mafuta mengi na chenye madini ya potassium kitaalamu kinaitwa DASH diet (dietary approaches to stop hypertension)
2. Mazoezi mara kwa mara- angalau nusu saa kwa siku
3. Kwa wavutaji sigara kuacha kuvuta sigara
4. Punguza au kama unaweza acha unywaji wa pombe ( kwa wanaume angalau bia 2 kwa siku na wanawake bia 1)
5. Punguza utumiaji wa chumvi hasa ya kuongeza mezani (usitumie zaidi ya gramu 1.5)
6. Punguza msongo mawazo
7. Hakikisha unakuwa kwenye uzito wa afya, kama uko kwenye uzito wa hatari fanya mpango wa kupunguza uzito.
8. Matumizi ya mafuta ya samaki husaidia kupunguza shinikizo la damu, kwa wenye shinikizo la damu.
Hitimisho:
Ili kuepukana na kupata ugonjwa huu wa shinikizo la damu ni muhimu kuwa na kawaida ya kuangalia afya zetu mara kwa mara.
Lakini pia ni vyema kuangalia namna tulavyo. Kula mlo ulio kamili ni muhimu na kupunguza vyakula vya mafuta ya wanyama.
Kupunguza matumizi ya chumvi kwa wingi na kufanya mazoezi mepesi ya mara kwa mara angalau kwa siku dk 15.
0 comments:
Post a Comment