NEYMAR ALIMWA KADI NYEKUNDU ,BRAZIL WAKICHAPWA NA COLOMBIA,COPA AMERICA
Timu ya Taifa ya Brazil imechinjwa goli 1-0 dhidi ya Colombia katika mechi ya pili ya kundi C ya michuano ya mataifa ya America kusini, Copa America inayoendelea nchini Chile.
Goli pekee la ushindi la Colombia kwenye mtanange huo uliochezwa uwanja wa Santiago limefungwa dakika ya 36' kupitia kwa Jeison Murillo.
Dakika ya 90' Neymar wa Brazil na Carlos Bacca wa Colombia walioneshwa kadi nyekundu baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa.
Kadi hiyo ni aibu kubwa kwa Neymar kwani haikuwa na ulazima ikizingatiwa yeye ndiye nahodha wa Brazil na amebeba matumaini ya timu hiyo ambayo bado ina machungu ya kupigwa 7-1 na Ujerumani katika mechi ya nusu fainali ya kombe la dunia lililofanyika mwaka jana kwenye ardhi yao.
Tukio lilikuwa hivi: baada ya mwamuzi raia wa Chile, Enrique Osses kupuliza filimbi ya kumaliza mpira, Neymar alimpigia mpira kwa makusudi, Pablo Armero wa Colombia ambao ulimgonga mgongoni na ndipo vurumai ikaanza baina ya wachezaji wa timu zote mbili.
Wakati fujo hizo za wachezaji zikiendelea, Carlos Bacca alimsukuma mgongoni Neymar na ndipo mwamuzi akawaonesha kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Kwa mara nyingine tena, Radamel Falcao alionesha kiwango cha chini na alitolewa baadaye.
Mechi nyingine ya kundi C itapigwa usiku wa kuamkia kesho kati ya Peru na Venezuela.
0 comments:
Post a Comment