Friday, 25 December 2015

AKINA MAMA NA VIJANA NI NGUZO KUBWA YA KULETA MABADILIKO KATIKA VIJIJI

.

 Bwana Bony Lukas akieleza jinsi anavyofanya uraghbishi hasa katika kuwasaidia vijana kujua haki zao na kujitambua.

Na Fredy Njeje wa Blogs za Mikoa
Ni suala ambalo lipo wazi kuhusu tofauti za kimaisha baina ya wakazi wa mijini na vijijini, ila changamoto nyingi zaidi zinaonekana kuwakabili zaidi wale wanaoishi vijijini. Huko wananchi wanakosa huduma ambazo kimsingi ni haki zao na hivyo kutokuwa na usawa baina yao na wale wa mijini.
Picha kubwa inayojionesha vijijini kwa upande wa wanawake ni hasi kwa kiasi Fulani ukilinganisha na ile ya wanaume. Usawa wa kijinsia na kielimu baina yao na wanaume ni mkubwa sana, kesi za unyanyasaji kwao ni nyingi zaidi.  Pamoja na jihudi nyingi za kuwawezesha wanawake bado hawajapata nafasi ya kutoshwa kuweza kusikilizwa. Wanaume wameendelea kuwa watoa maamuzi na wanufaikaji wa kimfumo. 
 Mmoja wa waraghbishi akiwa anaonesha ripoti ya wanafunzi watoro katika shule ya msingi ya Nyandekwa .
Takwimu zinaonesha kuwa hata idadi ya ufauru kwa wasichana kwa Shule za msingi imeongezeka ambapo mwaka 2013 wasichana waliofaulu ni  281,460 sawa na asilimia 50.20 ya wanafunzi 560,706 wakati wavulana waliofaulu  ni 279,246 sawa na asilimia 49.80. Kabla ya ya matokeo wasichana waliofanya mtihani walikuwa 456,082 sawa na asilimia 52.68 na wavulana 409,745 sawa na asilimia 47.32. Mwaka 2014 jumla ya watahiniwa 808,085 wa shule za msingi Tanzania wasajiliwa kufanya mtihani huo wakiwemo wasichana 429,624 sawa na asilimia 53.17 na wavulana 378,461 sawa na asilimia 46.83. Jumla ya watahiniwa 451,392 kati ya 792,118 walifanya mtihani, wasichana waliofauru ni 226,483 ambao ni sawa na asilimia 53.59 na wavulana 224,909 sawa na asilimia 46.41. 
 Mraghishi Mariam Stephano (katikati) akieleza jambo wakati wa kikao.
Katika nchi yetu ya Tanzania kuna makabila zaidi ya 100 na kila moja likiwa na mila na tamaduni zake. Ni vizuri ikaeleweka kwamba wazee wetu hawakuwa wakichangamana kimakabila hivyo ni watu wachache walikuwa wanahama toka sehemu moja kwenda nyingine. Aina hii ya maisha ilipelekea wengi wao kuoana wa kabila moja, tofauti ikiwa ni vijiji ama kata, ila wengi ilikuwa toka mkoa ama wilaya moja. 

Tofauti na sasa  ambapo watu wanachanganyikana kutokana na shughuli za kiuchumi na kijamii. Hali hii ya kuchanganyikana baina ya makabila ndani ya mkoa ama wilaya ama kijiji kimoja imeleta tamaduni tofauti na zile ambazo zilikuwa zimezoeleka kiuchumi na kijamii.

Pamoja na mchanganyiko huo bado kumekuwa na changamoto nyingi sana zinazowakabili wakazi wa vijijini. Bado wanaishi kwenye lindi la umaskini na ukosefu mkubwa wa huduma za kijamii. Changamoto hizi zinasababisha baadhi yao kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanadai na kusimamia haki za msingi za kijamii; hawa wanaitwa waraghbishi.

Waraghbishi ni mtu mmoja mmoja ama kikundi cha watu ambao wamevutika kufanya uraghbishi aidha kwa kufundishwa ama kwa kuona matokeo ya matendo wanayofanywa na wanajamii wenzao. Hususani wale ambao wanachukua hatua katika kustawisha au kulinda haki za binadamu na kuwakumbusha wenzao majukumu yao kwa maslahi ya kijamii, kiuchumi ama kisiasa.
 Matilda Peter(wa pili kushoto) aliyeanza Uraghbishi 2015 akieleza namna anavyofanya Uraghbishi kwa kuwapa elimu wasichana juu ya kujitambua, na kuepuka mimba za utotoni
Moja ya haki hizo ni zile za wanawake ambao kwa muda mrefu wameonekana kuwa nyuma zaidi. Hali hii imewaondelea kujiamini na kujiona wao ni wa daraja la pili na hivyo kutokuwa na sauti katika jamii zao.
Mmoja wa waraghbishi hao ni Bw. Bony Lukas toka kijiji cha Nyandekwa wilayani Kahama katika mkoa wa Shinyanga. Mraghbishi huyu ameweza kuelimisha watu wa kijiji chake. 

Akielezea jinsi anavyoraghbisha vijana katika kijiji chao, Lukasi anasema:
“Vijana ndio wenye nguvu za kuweza kuleta maendeleo na ndio wenye mchango mkubwa ndani ya jamii zetu. Kwa hiyo ni lazima wawe ni watu wenye kujitambua katika nyanja zote. Ili waweze kupata nafasi mbalimbali za kuweza kutoa mchango wa mawazo ili yaweze kufanyiwa kazi”
Hali inatokana na ukweli kwamba vijana wamekuwa nyuma kwa muda mrefu bila. Uraghbishi kwao ni mrejesho wa nafasi finyu ambazo vijana wa vijijini wamekuwa hawapewi nafasi ya kuweza kuchangia pindi wawapo  katika mikutano ya kimaendeleo ndani ya vijiji. Hii ilitoa nafasi ya mraghbishi kupokea  mawazo kutoka kwa vijana wa kike na wakiume kwani vijiji  vilivyo vingi hupuuza mchango wa mawazo ya mtoto wa kike na kumuona hana thamani. 

Kwa mantiki hiyo mraghbishi Lukasi aliweza kuwatia ujasiri kwa kutoogopa kwani watakavyo kuwa na roho ya uoga ndio itakayo wafanya wabaki nyuma kimaendeleo. Kuna msemo unasema “woga wako ndio umaskini wako”. Hivyo alihakikisha anawawezesha vijana kujiamini na kushirikiana vyema na uongozi  wa kijiji.  

Elimu ya jinsia pia ni tatizo katika vijiji vingi vya hapa Tanzania ambapo mraghbishi Miriam Stephano yeye aliweza kutumia nafasi hiyo kwa kuweza kuwaelimisha vijana kuhusu elimu ya jinsia. Akilielezea hilo anasema:
“Hapa kijijini kuna vijana wa rika tofauti tofauti. Wapo wale ambao ndio wanabalehe na wale waliovuka hiyo ngazi ya kubalehe. Mabadiliko hayo ya kimaumbile hupelekea vijana wengi kuanza kuwa na muelekeo usio sahihi. Sababu ikiwa ni mihemko inayo wakumba  pindi wawapo katika shughuli za kila siku hasa kwa wale wanao soma.” 
Mraghbishi Bujika Adam Joseph  kutoka kijiji cha Guduba akitoa mchango wake wa namna alivyofanya uraghbishi kwa kuwahimiza vijana kuhudhuria mikutano ya vijiji ili nao wapate kushiriki katika kutoa mawazo na michango yao mbalimbali ya mawazo.
Vijana hawa katika kijiji hicho wanapata changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya kimaumbile. Hili linapeklekea kupata mimba za utotoni pamoja na maambukizi ya virusi vha Ukimwi. Hivyo kupitia waraghbishi vijana hawa wamekuwa wakipewa elimu ili waweze kujikinga na kujiepusha na hari zinakokuwa zikiendelea kuleta mabadiliko katika miili yao.
Changamoto hii ndio iliyomplekea mraghbishi huyu mwanamke toka kijiji cha Nyendekwa, wilayani Kahama Bi. Mariam Stephano kuraghbisha  kundi hili, kama anavyofafanua yeye mwenyewe:  
“Nikiwa kama mwanakijiji mraghbishi huwa ninapita katika mashule mbalimbali. Huko naomba ruhusa kwa mwalimu mkuu na kuweza kuzungumza na wanafunzi wa kike jinsi gani wanaweza kushughulika na mabadiliko ya miili yao. Nawaelekeza nini wafanye pindi wanapofikia umri wa kubalehe. Hapo ntawafundisha usafi wa mwili na namna ya kukwepa vishawishi vitakvyowapelekea aidha kupata maambukizi ya virusi vya Ukumwi ama mimba za utotoni”

Elimu hii ya jinsia inawasaidia watoto katika kijiji cha Nyandekwa, kwani wengi wao huanza kujitambua na kuwa na akili ya kutafakari yale yaliyo mema na mabaya. Na pia inawasaidia hata upande wa serikali katika dhana ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi na magonjwa ya zinaa. 
Bi Anna  Zengu aliyepata uwenyekiti wa Kitongoji cha Busolwa kutokana na Uraghbishi akielezea kwa kina jinsi alivyo wasaidia akina mama wenzake kujitambua na kujua umuhimu wa kupiga kura na kuchagua viongozi bora wanaofaa kuongoza Taifa.
Kwa upande wa mraghbishi Wilbert Michael kutoka kijiji cha Kakebe wilayani Kahama yeye alifanya utafiti usio rasmi juu ya tabia za uongozi wa kijiji chao. Hapo aliweza kugundua mambo kadhaa yaliyokuwa yakifanywa na viongozi wa kijiji hicho pasipo kuwashirikisha na wananchi. Na walifanya hivyo kwa maslahi binafsi.
Akielezea hali hiyo, Michael anasema:
“Kupitia uraghbishi nilionao niliweza kufuatilia mambo mbalimbali katika ofisi ya kijiji pamoja na ile ya kata. Lengo ikiwa ni kubaini tatizo lililokuwa linakabili kijiji. Kubwa likiwa ni viongozi kujali maslahi binafsi, hapakuwa na uwazi kwenye mikataba ya kimaendeleo ya kijiji,”
Swali la kujiuliza yeye mraghbishi alijuaje habari hizo, akijibu swali hilo ansema:
“Nililigundua kupitia mbao za matangazo ambapo walibandika tangazo la kuingia kwa mkataba na watu wanao sambaza vyandarua  vijijini na wao kuchukua kama ni mradi wa kujipatia kipato. Kupitia mradi vijana walitakiwa kugawa vyandarua hivyo, na hivyo ilikuwa ndio iwe ajira yao.”
Badala yake Mwenyekiti na Afisa Mtendaji wa kijiji wao wakawa wanawachangisha vijana fedha kiasi cha shilingi elfu kumi (10,000) kwa kila mmoja.  Lengo lao likiwa ni kuwasajili kwa kuwa wasambazaji wa vyandarua hivyo kinyume cha dhana nzima ya kuleta maendeleo kijini. 

Na ndipo mraghbishi Michaeli  alitumia uraghbishi wake kwa kuweza kuwataarifu wananchi na ndipo wananchi walipoamua kumwajibisha mwenyekiti huyo. Walichoamua ni kupeleka malalamiko katika ngazi mbalimbali za kata na wilaya ili waweze kumvua madaraka yake na kupendekeza jina la mweenyekiti mpya wanayemtaka na atakayeshirikiana na wanakijiji.
Hii ni dhahiri kwamba bado wananchi wanaoishi vijijini wanahitaji elimu ya kiraia itakayowawezesha kuwasilisha matatizo yao kwenye ngazi husika. Ili nao waweze kuwasaidia wenzao wanapogundua yale yanayofanywa na viongozi wao hayaendani na dhana ya ukweli na uwazi.  Na piakuwa na ujasiri wa kuweza kuongea sehemu mbalimbali. 
Baadhi ya wakazi wa kata ya Nyandekwa wakiwa wanajadiliana jambo

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA