Monday 14 March 2016

SIMBA YAUNGURUMA TAIFA,YAILAZA PRISONS 1-0

simba_muda
simba_muda
Wachezaji wa timu ya Simba wakishangilia.
Said Ally, Dar es Salaam
SIMBA ni mfalme wa pori, akipita wanyama wengine wote wanapaswa kukaa kimya kuonyesha heshima na ndivyo inavyojithibitisha kwa Wekundu wa Msimbazi ambao hivi sasa moto wao unawanyamazisha kila wanayekutana naye.

Baada ya kuichapa Mbeya City mabao 2-0 bila huruma, jana ilikuwa ni zamu ya Tanzania Prisons ambao baada ya kubana sana, hatimaye waliachia dakika za mwishoni kabisa.
Jana ilikuwa ni ushindi wa bao 1-0 tu lakini wenye faida kubwa kutokana na Wekundu hao sasa kufikisha pointi 54 ambazo ni nne zaidi ya wapinzani wao Yanga walio katika nafasi ya pili na saba zaidi ya Azam, ingawa Simba ana michezo mitatu zaidi ya Azam na miwili zaidi ya Yanga.

Simba-Day-559x520
Simba-Day-559x520

Kocha Mganda Jackson Mayanja alipewa cheo cha ukocha Simba akiwa kama msaidizi baada ya Dylan Kerr kutimuliwa, huku Simba ikifanya mchakato wa kumtafuta kocha mwingine, kinyume chake amefanya kweli ambapo jana aliiongoza Simba kushinda mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons bao 1-0, idadi ambayo imefanya awe ameshinda mechi tisa kati ya 10 alizoiongoza timu hiyo.
Wakati Mayanja akifanya hayo, Awadhi Juma aliingia katika dakika ya 71 kuchukua nafasi ya Justice Majabvi kisha kufunga bao la pekee dakika ya 87 katika mchezo huo kwenye Uwanja wa Taifa, ambao ulikuwa mgumu huku watu wengi wakiamini utamalizika kwa suluhu.
Mtanange huo wa jana ulikuwa mgumu muda mwingi huku Simba wakikosa nafasi nyingi ambapo mara mbili mshambuliaji wao, Ibrahim Ajib aligongesha mwamba.
Kipindi cha kwanza, Simba waliingia kwenye eneo la 18 la Prisons mara 17 na kupiga mashuti matano langoni lakini hawakuweza kupata chochote, kipindi cha pili wakaingia kwenye anga za wapinzani wao hao mara 10, wakapata bao hilo moja.
Kwa ujumla mechi nzima, Simba ililishambulia lango la Prisons mara 27, wakipiga mashuti tisa kwenye lango la Prisons. Wekundu walipiga mashuti nane yaliyokwenda nje ya lango ‘off target’ katika mchezo mzima.
Prisons ambayo iliingia kwenye pambano hilo ikiwa kwenye ubora wa hali ya juu, ni timu ambayo haifungiki kirahisi, katika mechi zao 22 walikuwa wamefungwa nne tu msimu mzima, wakiwa katika nafasi ya tano. Hata hivyo inaonekana kwenye mchezo wa jana waliingia kwa nia ya kutafuta sare tu.
Walipiga mashuti saba tu mchezo mzima huku mawili pekee ndiyo yakilenga lango. Kocha Jackson Mayanja, amesema: “Wapinzani wetu walikuwa wanatumia mfumo wa kulinda zaidi badala ya kushambulia, tukalazimika kutumia washambuliaji wengi.
“Nimefurahi kupata ushindi, niliwatuma wachezaji wangu kupambana muda wote wa mchezo na hiyo ndiyo sababu ya kushinda.”
Kocha Salum Mayanga wa Prisons ambaye timu yake inaheshimika kwa soka safi ikiwa na wachezaji wengi mahiri akina Jeremiah Juma na Mohammed Mkopi, amesema: “Nawashukuru wachezaji wangu wamepambana ingawa tumepoteza mchezo, sasa tunajipanga kwa ajili ya mechi ijayo, tunaelekea Tanga.”
Katika mchezo huo, Ajib ndiye aliyeonekana kuwa msumbufu kwa mabeki wa Prisons na kujikuta wakimchezea faulo mara kadhaa, lakini kipa wa Prisons, Beno Kakolanya naye alifanya kazi nzuri ya kuchomoa michomo mingi ya Simba.
Katika mchezo huo, straika wa Simba, Hamis Kiiza alishindwa kabisa kung’ara kama ilivyo kawaida yake huku akipata nafasi moja tu kipindi cha kwanza ambapo alibaki yeye na kipa lakini shuti lake lilitoka nje.
Simba pia walimtumia mshambuliaji wao aliyekuwa majeruhi muda mrefu, Paul Kiongera, aliyeingia kuchukua nafasi ya Kiiza katika dakika ya 83.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA