Wednesday 16 November 2016

MAKAMU WA RAIS MHE.SAMIA AZINDUA KAMPENI YA UCHUNGUZI WA SARATANI YA MATITI....ASEMA 50% YA VIFO VYA WANAWAKE HUSABABISHWA NA SARATANI HIYO


Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi kuwa serikali imeweka mipango na mikakati thabiti ya kukabiliana na idadi kubwa ya vifo vinasababishwa na saratani  hasa saratani ya matiti na mlango wa kizazi kote nchini.

Ametoa kauli hiyo jana  katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza wakati akizundua kampeni ya uchunguzi wa saratani ya matiti na mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi mkoani Mwanza.

Samia alisema Tanzania ikiwa ni nchi mojawapo Kusini mwa Jangwa la Sahara ina kiwango cha juu cha vifo vya saratani ya matiti na mlango wa kizazi ambapo asilimia 60 ya vifo vyote   vinavyotokea Kusini mwa jangwa la Sahara vinasababishwa na saratani hiyo.

Makamu wa Rais alisema kuwa vifo vingi vinatokana na uelewa mdogo, imani potofu, gharama kubwa za matibabu, unyanyapaa na kuwepo kwa vituo vichache wa kufanyia uchunguzi  hapa nchini ambapo kwa sasa tiba ya mionzi inapatikana katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dar es Salaam.

Katika kukabiliana na tatizo hilo, Makamu wa Rais alisema kuwa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea kiasi cha shilingi bilioni Tano kutoka Benki ya Dunia fedha ambazo zitawezesha vituo Vitatu kwa kila Halmashauri ambavyo vitasaidia kuboresha huduma za uchunguzi na matibabu ya mapema ili wanawake kote nchini hasa wale wale wa vijijini waweze kupata huduma hizo kwa urahisi na kwa ukaribu kwenye maeneo wanayoishi.

“Wote ni mashuhuda kwa namna saratani ya mlango wa kizazi inavyosababisha vifo vingi hali ambayo hutokana  na magonjwa wanaogundulika na ugonjwa kuwa tayari wamefikia hatua isiyotibika na kwa pamoja saratani hizi mbili husababisha zaidi ya asilimia 50 ya vifo vyote vya akinamama”

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa kwa sasa tayari kuna vituo takribani 300 vinavyotoa huduma za upimaji wa dalili za awali katika vituo vya afya kote nchini na hivyo vituo vipya vitaongeza huduma endelevu ili kupunguza vifo vitokanavyo na saratani.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alisema kuwa Tanzania  ni miongoni mwa nchi zenye wagonjwa wengi wa saratani ya mlango wa kizazi na pia ndiyo inaongoza katika nchi za Afrika Mashariki.

Alisema kuwa idadi ya wanawake 6,241 hugundulika kuwa na saratani kila mwaka  na kati yao zaidi ya nusu yaani 4,355 hufariki dunia.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA