TCAA KUWAHUDUMIA WATEJA WAKE KIMKAKATI
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau kupitia Dawati la Huduma kwa Wateja, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kupokea maoni na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haraka na kwa ufanisi.
Akizungumza katika Banda la TCAA kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa wa Dawati la Huduma kwa Wateja, Bw. Rashid Mngoya, alisema dawati hilo limeanzishwa ili kuwa kiungo kati ya Mamlaka na wananchi kwa kuwapatia taarifa sahihi kuhusu huduma mbalimbali za usafiri wa anga.
Alieleza kuwa kupitia dawati hilo, wadau wanaweza kuuliza maswali, kuwasilisha maoni, kutoa mapendekezo au changamoto wanazokutana nazo, pamoja na kupata mwongozo kuhusu taratibu mbalimbali zinazosimamiwa na TCAA.
Kwa mujibu wa Bw. Mngoya, uwepo wa dawati hilo unaimarisha mawasiliano kati ya TCAA na wateja wake, huku ukihakikisha hoja na malalamiko yanashughulikiwa kwa wakati ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.
Alisisitiza kuwa TCAA itaendelea kuboresha huduma zake kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa katika usalama, ulinzi na utoaji wa huduma bora kwa wadau wote wa sekta ya usafiri wa anga.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa TCAA, Bw. Ally Changwila, alisema Mamlaka imefanya maboresho mbalimbali katika mifumo yake ya mawasiliano ili kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi. Alitaja mojawapo ya maboresho hayo kuwa ni tovuti ya TCAA ambayo sasa inapatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, ikiwa na taarifa zilizoboreshwa na sehemu maalum ya Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs) ili kuwasaidia watumiaji kupata majibu ya haraka kuhusu huduma mbalimbali.
Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Sabasaba, TCAA inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake ya kiudhibiti, haki na wajibu wa abiria, matumizi salama ya ndege zisizo na rubani (drones), pamoja na huduma nyingine zinazohusiana na sekta ya usafiri wa anga.
Hatua hizi zinaonyesha dhamira ya TCAA ya kuendelea kuboresha huduma kwa wateja, kuimarisha mawasiliano na wadau na kuongeza uelewa wa umma kuhusu mchango wa Mamlaka katika kuhakikisha sekta ya usafiri wa anga nchini inaendelea kuwa salama, yenye ufanisi na kuendana na viwango vya kimataifa.



0 comments:
Post a Comment