Monday, 19 December 2016

TUME YA MIPANGO YARIDHISHWA NA MPANGO WA KUBORESHA KIWANJA CHA NDEGE MTWARA KWA KIWANGO CHA KIMATAIFA

Kaimu Katibu Mtendaji kutoka Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (aliyevaa suti) akiwa pamoja na maofisa wa mamlaka ya viwanja vya ndege na wa Tume ya Mipango wakielekea kukagua maeneo mbalimbali ya kiwanja hicho.
Meneja wa Teknolojia na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini , Bw. Abdulatif Min-Hajj (aliyekaa kulia kwa Kaimu Katibu Mtendaji) akielezea mpango wa kuboresha kiwanja cha ndege Mtwara mbele ya timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango.
Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri akitoa ushauri kwa maofisa wa mamlaka ya viwanja vya ndege juu ya umuhimu wa kuwa na hati miliki ya eneo hilo.Mchumi Mkuu kutoka Tume ya Mipango, Bibi Salome Kingdom akiongea jambo na Bw. Daniel Werema kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wengine ni Mhandisi Omary Othman (aliyevaa t-shirt) na Bw. Hekima Chengula kutoka Tume ya Mipango.

Sehemu ya barabara inayotumika katika kutua na kuruka ndege (Runway) ya Kiwanja cha Mtwara. Urefu wa barabara hiyo ni mita 2258 na ina upana wa mita 30.
 
Na Adili Mhina, Mtwara. 

Katika kutekeleza Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mamlaka ya viwanja vya Ndege imedhamiria kufanya maboresho katika Kiwanja cha Ndege Mtwara kwa kiwango cha Kimataifa ili kuendelea kuimarisha huduma za usafiri wa anga nchini. 

Mapango huo umeelezwa hivi karibuni na Meneja wa Teknolojia na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini , Bw. Abdulatif Min-Hajj wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya Kiwanja hicho kwa Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri alipofanya ziara katika kiwanja hicho ikiwa ni mfululizo wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo unaofanywa na timu kutoka Tume ya Mipango. 

Meneja huyo alieleza kuwa mradi huo amabao ni mpango wa muda mrefu unaolenga katika kufanya upanuzi wa kiwanja pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa kwa ajili ya abiria upo katika hatua za awali ambapo mkandarasi mshauri tayari amewasilisha rasimu ya taarifa ya mpango mkuu (maste plan). 

“Katika mradi huu kiwanja cha Mtwara kitapanualiwa na kufikia code 4E ambapo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kama A340-200. Katika ujenzi wa jengo la abiria, kwa awamu ya kwanza tutajenga jengo lenye mita za mraba 6570 ili kufikia mahitaji ya mwaka 2023 na awamu ya pili tunatarajia kuwa na jengo la mita za mraba 10,880 ili kukidhi mahitaji ya abiria kwa mwaka 2033”, alieleza Meneja huyo. 

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri alieleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo inasisitiza kuwa na vianzio mbalimbali vya uchumi na kuwepo kwa miundombinu ya kutosha kuiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za kipato cha kati. Hivyo, mradi huo utasaidia kuimarisha uchumi wa nchi sambamba na kuongeza ufanisi katika usafiri wa anga. 

Aliongeza kuwa upanuzi wa kiwanja hicho utakapokamilika sio kwamba tu utasaidia usafiri wa anga peke yake bali kwa upande mwingine utafungua fursa mbalimbali za uwekezaji kwa sekta binafsi na kusaidia kuongeza uchumi kwa watanzania. 

“Nimeelezwa kuwa mradi huo ukikamilika kutajitokeza fursa za uwekezaji kama kujenga mahoteli makubwa ya hadhi ya nyota tano, kujenga eneo la biashara, ujenzi wa maduka na migahawa ya kisasa, ujenzi wa visima vya mafuta ya ndege, kutakuwa na jengo kubwa la kuhifadhia mizigo, na majengo ya kutengenezea ndege. Hizi zote ni fursa zitakazosaidia kuinua uchumi wa wananchi wetu,” alieleza. 

Hata hivyo Mwanri alishauri kuwa pamoja na kuwa na malengo mazuri ya muda mrefu mamlaka ya hiyo inapaswa kuendelea kutekeleza malengo yake ya muda mfupi katika kutatua changamoto za miundombinu ya barabara za ndege kiwanjani hapo ili kuendelea kuimarisha huduma za usafiri huku akishauri mamlaka hiyo kufanya jitihada za haraka kupata hati miliki pamoja na kufikiria kujenga uzio katika eneo la kiwanja hicho. 

“Mnapaswa kuendelea kutekeleza mipango ya muda mfupi wakati mnasubiri mradi mkubwa utekelezwe. Najua katika bejeti yenu ya sasa mtaendelea kukarabati miundombinu ili ndege ziendelee kutua na kuondoka kwa usalama. Vile vile angalieni namna ya kupata hati miliki na kujenga uzio wa eneo lote kwa ajili ya usalama na kuwadhibiti watu wenye tabia ya kuvamia maeneo”, Alieleza Mwanri.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA