Thursday, 20 April 2017

RAIS MAGUFULI KUFUNGUA KONGAMANO LA MAADILI

RAIS Dk. John Magufuli anatarajiwa kufungua kongamano la maadili  lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Akizungumza kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Aboubakar Zuberi Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka, alisema kongamano hilo litafanyika Aprili 24.

Alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili mmomonyoko wa maadili uliopo ndani ya jamii hivi sasa.

“Kongamano hili limeandaliwa na Bakwata ambapo litahudhuriwa na masheikh mbalimbali pamoja na viongozi wa kidini kutoka mikoa mbalimbali, lengo likiwa ni kuangalia jinsi maadili yalivyoporomoka na kutafuta mbinu ya kuijenga jamii iliyo bora,” alisema Sheikh Mataka.

Alisema kongamano hilo la siku moja litafungwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Alisema wengine watakaohudhuria kongamano hilo ni wajumbe wa Ulamaa Taifa, masheikh kutoka taasisi mbalimbali, viongozi wa kidini kanda, mabalozi, wakuu wa vyombo vya usalama na wananchi walioalikwa.

Sheikh Mataka alisisitiza kuwa maadili ni muhimu ndani ya jamii na kwamba kwa sasa nchi inakabiliwa na mmomonyoko wa maadili.

“Ukiona jamii inazungukwa na walevi, watumiaji dawa za kulevya, binadamu wengine wanafurahia wenzao wakiuawa au kupata ajali, ni hali ya kupoteza mwelekeo wa maadili,” alisema Sheikh Mataka.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA