Friday 14 April 2017

RIPOTI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI (CAG) YAIBUA MADUDU

Ripoti  ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2015/16 imeanika madudu kila kona, huku deni la Taifa likizidi kupaa.

Pamoja na hali hiyo ripoti hiyo imeeleza kwa kina namna vitendo vya ukwepaji kodi katika taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo migodi ya dhahabu ambayo haijalipa kodi kwa kipindi cha miaka 10.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa baada ya kuwasilisha ripoti hiyo bungeni, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, alisema ukaguzi huo umehusisha taasisi 543 kati yake 222  zikiwa za Serikali kuu, 171 Serikali za mitaa na 150 ni mashirika ya umma kati ya 200 yaliyopo.

Pamoja na hali hiyo Prof. Assad, aligusia pia suala la bajeti iliyopita jinsi ilivyotekelezwa  ambapo aliishauri Serikali kupanga bajeti inayoweza kuitekeleza badala ya kupanga kiasi kikubwa ambacho hakina uhalisia.

Hata hivyo ripoti hiyo haina tofauti na ripoti nyingine za nyuma zilizotolewa na CAG, ambapo madudu mengi yamekuwa yakiripotiwa, lakini hakuna mabadiliko katika kudhibiti ubadhirifu huo.

Ripoti hiyo pia inaonesha hati zilizotolewa kwa Serikali, Bunge na Mahakama ni 505, kati yake 436 sawa na asilimia 86.34 ni hati safi, 60 sawa na asilimia 11.88 ni  zenye shaka na nne sawa na asilimia 0.79 haziridhishi na tano sawa na asilimia 0.99 ni mbaya.

Mchanganuo wa hati zilizotolewa, unaonesha mamlaka ya Serikali za Mitaa ilikuwa na jumla ya hati 171, kati yake hati inayoridhisha ni 138, hati yenye shaka ni 32, hati isiyoridhisha ni moja huku kukiwa hakuna hati mbaya.

Msahama wa kodi tishio
Ripoti hiyo inaonyesha, taarifa ya uchunguzi ya Mei, 2016 ilibaini matumizi mabaya ya msamaha wa kodi wa Sh bilioni 3.46 ambao ulitolewa kwa walengwa wawili walioagiza magari 238.

Alisema magari hayo yalisajiliwa kwa majina tofauti na wale waliopewa msamaha huo.

“Walengwa wote waliopewa misamaha hiyo walikana kuhusika na magari hayo, hali inayoonyesha kuwa bado kuna uhitaji wa kuboresha udhibiti na ufuatiliaji wa masuala ya misamaha ya kodi,” alisema.

Misahama kwa migodi
Kuhusu tathimini ya misamaha ya mafuta yanayoingizwa nchini kwa ajili ya matumizi ya migodi, alisema ukaguzi ulibaini lita za mafuta 4,248,802 yaliyosafirishwa kutoka Dar es Salaam kati ya Oktoba, 2014 na Desemba 2015 kwa ajili ya matumizi katika migodi ya Buzwagi, Bulyankulu na Geita.

 Prof. Assad, alisema ukaguzi huo ulibaini kuwa lita 20,791,072 za mafuta yenye msamaha wa kodi wa Sh bilioni 10.17 kwa ajili ya Mgodi wa Buzwagi kwa kipindi cha miezi 18 yalisafirishwa kwenda kwa Kampuni ya M/S Aggreko na  mkandarasi msaidizi ambaye hakuwa muhusika katika msamaha huo.

 “Naishauri Serikali pamoja na TRA kufanya uchunguzi wa mafuta yote ambayo hayana ushahidi kama yamesafirishwa katika vituo vya uchimbaji madini na kukusanya kodi inayodaiwa kiasi cha Sh bilioni 1.599,” alisema.

Alisema ni lazima Serikali ihakikishe kodi ya Sh bilioni 10.17 katika mafuta yote yaliyosamehewa kodi na kupelekwa kwa wakandarasi wasiohusika na msamaha huo kama M/S Aggreko inakusanywa.

“Serikali pia ihakikishe kuwa usimamizi unaimarishwa juu ya matumizi ya misamaha inayotolewa kwa mujibu wa sheria ili kuepusha hasara kwa serikali kutokana na matumizi mabaya ya misamaha ya kodi hizo,” alisema.

Licha ya hali hiyo alisema ukaguzi ulibaini kuwa kiasi cha lita 3,874,263 chenye kodi ya Sh bilioni 2.45 kilichoingizwa nchini pasipo ushahidi wa taarifa za malipo ya kodi husika.

“Katika nyakati tofauti, sikupatiwa nyaraka za ukusanyaji wa kodi kiasi cha Shilingi bilioni 2.42 kutoka kwenye lita 3,234,420 za mafuta yaliyoingizwa nchini na kampuni 24 za mafuta na kuchukuliwa na wamiliki kati ya Januari Mosi hadi Juni 30, 2016. Hii inaonesha upungufu katika ukusanyaji kodi zitokanazo na uingizwaji wa mafuta,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, aliishauri Serikali ifanye uchunguzi ili kubaini usahihi wa matumizi ya mafuta hayo na ikibainika hayakutumika ipasavyo, kodi husika zitozwe pamoja na riba.

“Pia serikali iboreshe mifumo ya kusimamia uagizaji wa mafuta ili kuzuia matatizo haya kujitokeza katika siku zijazo,” alisema.

Akizungumzia usimamizi na ufuatiliaji usioridhisha wa madeni ya kodi na tozo, alisema baada ya kupitia orodha ya madeni ya Idara ya uchunguzi, kodi za ndani na walipa kodi wakubwa pamoja na vielelezo vingine na kugundua kuwa Sh bilioni 588.83 (Tax Investigation Sh bilioni 92.03, DRD Sh bilioni 425.83 na Ltd  Sh bilioni 70.97) kilikuwa hakijakusanywa na mamlaka kutoka kwa walipakodi mbalimbali.

 “Hii inaonyesha udhaifu katika ufuatiliaji na ukusanyaji wa madeni ya kodi na tozo.

“Nilipitia pia sampuli ya majalada ya walipa kodi na kubaini kodi iliyokadiriwa na kukusanywa na TRA ilikuwa pungufu kwa Sh bilioni 9.45,” alisema.

CAG alisema hiyo inaashiria kuwa mamlaka haikufanya uchambuzi na upitiaji wa taarifa ya mapato ya walipakodi na vielelezo vyake ipasavyo.“Hivyo, kutoa mwanya kwa wakadiriaji kufanya tathmini ndogo kwa walipa kodi na kuikosesha Serikali mapato,” alisema.

Alisema ukaguzi wa ukusanyaji wa kodi ya forodha umebaini mamlaka haikukusanya tozo ya maendeleo ya reli Sh bilioni 9.27, kodi ya bidhaa na mafuta na riba ya ucheleweshaji malipo Sh bilioni 3.3, ushuru wa forodha Sh bilioni 9.3 kutokana na bidhaa 9,942,810 ambazo hazikuwepo kwenye maghala ya forodha na utokusanywa kwa kodi ya ongezeko la Thamani (VAT) kwenye maziwa yaliyosindikwa Sh bilioni 2.96 ambayo yaliingizwa nchini.

“Hivyo, jumla ya Shilingi bilioni 613.6 hazikukusanywa na mamlaka ingawa tathmini ya kodi ilifanyika kwa hoja zote zilizoeleza hapo juu,” alisema.

Madudu Tanzanite
Profesa Assad alisema katika ukaguzi huo wamebaini kuwa kampuni ya Sky Associates ambayo ilinunua hisa za umiliki wa Kampuni TML inayoendesha Mgodi wa Tanzanite One kutoka kwa Kampuni ya Richland Januari 30 mwaka 2015 imekuwa ikiuzia madini Tanzanite Kampuni Tanzu ya Sky Associates bila kumshirikisha mbia mwenzake ambaye ni Stamico.

Pia imebaini kuwa TML inatafuta masoko na kuuza Tanzanite bila kupata kibali cha mshirika wake STAMICO ambayo ni kinyume cha kifungu cha 15.1 (b-d) cha makubaliano ya ubia kati ya Stamico na TML.

Ufisadi NIDA
Profesa Assad alisema ukaguzi umejiridhisha kuwa uongozi na watoa huduma na wazabuni wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika ubadhirifu na udanganyifu kwenye matumizi ya fedha katika mradi wa kuboresha vitambulisho vya Taifa.

“Mradi huu unajumuisha mikataba ya manunuzi ya vifaa vya kuboresha vitambulisho vya Taifa, ununuzi wa vifaa vya Tehama kama vile IPad, programu na vifaa vya kompyuta, upatikanaji wa vibarua, bima za magari na gharama za kusafirisha na kufunga vifaa vya kusajili ambapo Sh bilioni  4.5 zilikuwa na udanganyifu,”alisema.

Alisema kutokana na hali ya usajili na kutoa vitambulisho vya Taifa kuwa mpya hali hiyo ilisababishwa na maandalizi hafifu kwa uongozi wa mamlaka ya juu ya kuamua jinsi mfumo ambao ungeweza kutumika vizurio

Alisema hali hiyo ilisababisha mabadiliko ya maelekezo yaliyogharimu Serikali kupitia manunuzi yasiyona tija na wakati huo huo wadanganyifu kutumia mianya iliyopo kujinufaisha wenyewe kinyume na taratibu.

Michango ya mifuko ya jamii
Profesa Assad alisema uhakiki wake amebaini kuwa makato ya kisheria yenye jumla ya Sh bilioni 284 yanayolipwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya yalicheleweshwa kati ya siku 30 hadi siku 90 baada ya malipo ya mishahara ya mwezi.

“Ucheleweshaji huu ulihusisha madai ya Mfuko wa Pesheni wa Watumishi wa Umma PSFPF kwa Serikali michango ya kabla ya mwaka 1999 pamoja na madai ya miaka ya nyuma kwa mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii.

“Matokeo yake nimebaini ucheleweshaji wa mkubwa wa ulipaji wa mafa kwa wastaafu waliokuwa wakichangia kwenye mifuko wa pesheni kwa watumishi wa umma mwaka huu,”alisema.

Aliishauri Serikali kulipa malimbikizo ya madeni na michango yake kwa wakati kwa mifuko ili kuiwezesha mifuko ya hifadhi ya jamii kuiwezesha mifuko ya hifadhi ya jamii kutimiza majukumu yake ipasavyo na wastaafukupata stahili zao kwa wakati.

Tanesco hasara
Kwa upande wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), ukaguzi umebaini shirika lina madeni katika manunuzi ya umeme kutoka kwa watengenezaji huru wa nishati  (IPPs), na watengenezaji wa dharura wa nishati (EPPs).

Inaonesha madeni hayo yamesababishwa na Tanesco kununua uniti moja ya umeme kwa wastani wa Sh 544.65 kutoka kwa  IPPs na EPPs na kuuzia wateja umeme kwa Sh 279.35 hivyo shirika kupata hasara ya Sh 265,30 kwa kila uniti.

Ili kumaliza hali hiyo, ripoti inashauri jitihada zaidi zifanyike katika kuongeza vyanzo vya umeme wa maji na gesi na kuachana na ule wa wazalishaji binafsi wanaozalisha nishati hiyo kwa mafuta.

Uwekezaji mifuko ya pensheni
Ripoti hiyo inasema, ukaguzi umebaini kushuka kwa mapato ya uwekezaji kwa kiasi kikubwa kwenye mifuko pensheni, NSSF, PPF, PSPF, na LAPF.

Alisema hali hiyo inatokana na kutokuwepo kwa ufanisi wa menejmenti katika kusimamia mikopo iliyotolewa kwa vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa.

Mbali na hilo ilielezwa kwamba usimamizi hafifu wa kuratibu shughuli za uwekezaji, umechangia kutokusanywa madeni ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na Sh trilioni 1.6 kutoka serikalini.

Ushuru wa bilioni 15 wayeyuka bandari
 Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ukaguzi Maalum kuhusu ushuru wa bandari (Wharfage), katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ambao ulilenga kubaini waliohusika na ukwepaji kodi bandarini, ulibaini ushuru wa Sh bilioni 15.02 haukukusanywa na TPA kutokana na ubadhirifu wa makampuni ya kutoa mizigo bandarini, wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na watumishi wa mabenki.

Usimamizi wa rasilimali watu
Profesa Assad alisema udhaifu katika usimamizi wa rasilimali watu umeendelea kujitokeza, ambapo malipo ya mishahara ya Sh bilioni 7.3 na makato ya kisheria ya Sh bilioni 2.5 yalifanyika kwa watumishi walioacha kazi au kufariki.

“Ukaguzi wangu umebaini kuwa mishahara ya watumishi walioacha kazi, waliofariki au waliostaafu wameendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao. Vilevile fedha za makato ya mishahara ya watumishi hao zimeendelea kupelekwa kwenye taasisi husika.

“Jumla ya Sh bilioni 1.2 kililipwa kwa sampuli ya watumishi 260 katika taasisi 919 za Serikali Kuu na Sh bilioni 6.1 zililipwa kwa watumishi katika Halmashauri 108 zilizokaguliwa,”alisema Profesa Assad.

 Alisema udhaifu mwingine uliojitokeza katika usimamizi wa rasilimali ni kushindwa kujiridhisha kuhusu urejeshwaji wa mishahara katika akaunti ya Hazina Sh bilioni 4.33.

Alifafanua kuwa katika sampuli ya taasisi 8 za Serikali Kuu na mamlaka za serikali za mitaa 53, ofisi yake ilibaini jumla ya Sh bilioni 4.33 hazikulipwa kwa wafanyakazi.

Kutokana na hili, aliishauri serikali kuweka mfumo wa mrejesho ambapo mamlaka za serikali za mitaa wakati wote zitakuwa na uwezo wa kupata taarifa za zuio la malipo.

Alitaja udhaifu mwingine kuwa ni malimbikizo ya madai ya wafanyakazi Sh bilioni 14.4, ambapo katika sampuli 7 ofisi yake ilibaini malimbikizo ya madai ya wafanyakazi yanayofikia Sh bilioni 8.2 kwa kipindi cha kuanzia mwaka mmoja hadi kumi.

Usimamizi wa mali, madeni
Alisema ukaguzi wake umebaini ongezeko la idadi ya magari yaliyotelekezwa katika taasisi mbalimbali za Serikali Kuu kutoka magari 675 mwaka 2014/15 hadi kufikia magari 1,272 mwaka 2015/16 sawa na ongezeko la asilimia 88.

Kwa upande wa Serikali za Mitaa, alisema jumla ya magari, pikipiki na mitambo inayofikia 652 yalitelekezwa pasipo hatua zozote kuchukuliwa na menejimenti.

“Kwa upande wa idara na wakala wa Serikali jumla ya magari 92 yalitelekezwa. Hata hivyo, menejimenti ya taasisi husika haikuchukua hatua yoyote. Uwepo wa mali hizi kwa muda mrefu pasipo kuuzwa, unaweza kusababisha hasara itokanayo na wizi wa vifaa na uchakavu,”alisema Profesa Assad.

Alisema kwa upande wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo, uhakiki wa dawa zilizonunuliwa kupitia fedha za mfuko wa kimataifa wa kupambana na Malaria, Ukimwi na Kifua Kikuu uliofanyika kwenye ghala la Bohari Kuu ya Dawa, umegundua uwepo wa dawa zilizokwisha muda wake zenye thamani ya Sh bilioni 10.19.

Ofisi za Ubalozi
Alisema kama alivyobaini katika ukaguzi wake uliopita, serikali haijachukua hatua zozote kufanya ukarabati wa baadhi ya nyumba katika Balozi za Tanzania nje ya nchi.

“Kati ya balozi 34, balozi 12 zinamiliki nyumba 37 zilizo katika hali mbaya na zinahitaji marekebisho. Wakati huo huo serikali inamiliki viwanja 10 katika balozi mbalimbali ambavyo havijaendelezwa hivyo viko katika hatari ya kunyang’anywa,”alisema.

Profesa Assad alisema uhakiki wa matumizi ya miradi ya maendeleo iliyokamilika kwa baadhi ya halmashauri ulibaini miradi yenye thamani ya Sh bilioni 4.2 ambayo haijaanza kutumika kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.

“Walengwa waliokusudiwa hawakupata faida iliyotarajiwa. Mfano wa miradi hiyo ni ya maji ya visima na bomba ambayo ilikamilika tangu mwaka 2013/14,”alisema.

Bil 24/-  bila ushindani
Profesa Assad alisema ukaguzi wake umebaini manunuzi yaliyofanyika bila ushindani kwa Serikali Kuu Sh bilioni 24.2.

“Manunuzi yaliyofanyika bila mkataba kwa Serikali Kuu kwa taasisi kumi Shilingi  bilioni 11.2, manunuzi kufanyika kwa  wazabuni wasioidhinishwa na mamlaka husika kwa Serikali Kuu kwa taasisi 14 Shilingi  bilioni 7.3.

“Manunuzi yaliyofanyika bila ushindani kwa Serikali za Mitaa Shilingi bilioni 2.1, manunuzi kufanyika kwa wazabuni wasiodhinishwa na mamlaka husika kwa serikali za mitaa halmashauri 28 Sh bilioni 1.2,”alisema Profesa Assad.

Mafuta na gesi
Profesa Assad alisema ukaguzi wake ulibaini kuwa matumizi ya bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni kiwango cha chini cha ujazo kwa asilimia 94 huku Tanesco akiwa ndiye mteja pekee akitumia wastani wa futi za ujazo milioni 46.61.

“Futi hizo za ujazo ni sawa na asilimia 6 tu ya ujazo wa bomba husika licha ya kuwepo makubaliano kati ya TPDC na Tanesco ya kusambaza futi za ujazo milioni  138.8 katika vituo sita vya kuzalisha umeme vya Tanesco.

“Pia nilibaini, mkataba wa Ubia wa Uzalishaji Gesi (PSA) baina ya TPDS na Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Limited (PAET) umetengenezwa kwa namna ambayo gawio la Serikali kutoka kwenye mauzo ya gesi asilia litakuwa linapungua kadiri uzalishaji unavyoongezeka,”alisema.

Kutokana na hilo, alipendekeza kufanyika upya kwa makubaliano ya mgawanyo wa uzalishaji (PSA) ili kuiwezesha serikali kunufaika zaidi pindi uzalishaji unapoongezeka.

Pamoja na hilo, alisema ukaguzi ulibaini kifungu cha 13.1 (a) cha ibara ya XIII ya mkataba wa ushirikiano wa uchimbaji gesi ya eneo la Songosongo kinaitaka PAET kulipa kodi ya ziada ya faida.

  “Sambasamba na hayo, nilibaini PAET haijawahi kuwasilisha ripoti ya kodi ya zaidi ya faida (statements of additional profit tax).

“Hata hivyo, Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 haikuwa na kipengele cha kodi la ongezeko la faida, mawasiliano na uongozi wa TRA yameonyesha kuwa sheria hii bado inaandaliwa,”alisema Profesa Assad.

Vyama vya Siasa
Profesa Assad alisema katika ukaguzi wa vyama vya siasa vinne kati ya 19 vilivyosajiliwa havikuwa na taarifa za fedha na hivyo kumfanya ashindwe kujiridhisha kuhusu usahihi wa taarifa hizo.

Alivitaja vyama hivyo ambavyo havikuwasilisha taarifa hizo kama kifungu cha 14(1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa inavyoeleza kuwa ni NRA, UPDP, Chauma na UMD.

Alisema wafanyakazi wa vyama vya siasa walibainika kuwa hawana mikataba huku vyama vitatu vikibainika kutokuwa na akaunti benki.

Alivitaja vyama ambavyo vilikosa akaunti benki kuwa ni Demokrasia Makini, Alliance for Democracy na Chama cha Kijamii (CCK).

Pia alisema vyama vinne havikuandaa taarifa ya fedha kwa ajili ya ukaguzi kama kifungu cha 14(1) cha sheriaya vyam avya siasa ambapo alivitaja kuwa ni NRA, UPDP na Chauma na UMD.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA