Friday, 2 June 2017

KAULI YA RAIS JAMAL MALINZI KWA UMMA




MAENDELEO YA TIMU ZA VIJANA. 

Ndugu zangu, leo nimewakaribisheni ili kwa niaba ya Shikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) niweze kutoa shukrani zetu, pongezi na pia kutoa mwelekeo wa timu zetu za vijana kuelekea Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 (FIFA WORLD CUP 2026). 
 
SHUKRANI. 

Kama tunavyofahamu timu yetu ya vijana umri chini ya miaka 17 ilishiriki kwa mara ya kwanza katika Fainali za Afrika (Afcon U17) nchini Gabon, fainali hizi zilichezwa kuanzia tarehe 14-28 mwezi Mei mwaka huu. 
 
Timu yetu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys ilishiriki katika fainali hizi na kutolewa hatua ya makundi. Katika hatua hii ilitoa sare ya 0-0 dhidi ya Mali, ikaifunga Angola bao 2-1 na kutolewa kwa sheria ya uwiano wa matokeo (head to head) baada ya kufungwa bao moja kwa bila na Niger. 
 
Ni jambo la kutia moyo kuwa bingwa wa mashindano haya Mali timu pekee ambayo hawakuweza kuifunga ni Tanzania na timu nyingine zote walizokutana nazo walizifunga ikiwemo na Ghana ambayo Serengeti Boys walitokana nayo sare hapa Dar es salaam. 

Hakika mashindano haya yameonyesha kuwa kumbe Tanzania tunao uwezo mkubwa wa kushindana katika mashindano makubwa. 

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania linapenda kutoa shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu, Waziri Mkuu Mh Kassim Majaliwa ambao kwa umoja wao walihakikisha timu inawezeshwa kikamilifu na kuwa na nguvu kubwa ya kushindana. 
 
Tunamshukuru sana Mh Dk Harrison Mwakyembe Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na watumishi wa Wizara kwa ushirikiano na jitihada kubwa walizozifanya kuhakikisha timu inapata maandalizi mazuri. 

Tunawapa hongera na kuwashukuru wachezaji wa Serengeti Boys kwa jitihada na ukomavu wao katika kipindi cha maandalizi na cha fainali zenyewe. Pongezi nyingi na shukrani kwa benchi la ufundi la timu na uongozi wa timu unaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF Ndugu Ayoub Nyenzi, Kamati ya Utendaji ya TFF wakati wote ilikuwa karibu naye na ilimpa nguvu sana. Hongera pia kwa wafanyakazi wa TFF waliohakikisha wanaratibu shughuli za timu kwa ufanisi mkubwa. 

TFF inawashukuru sana wajumbe wote wa Kamati ya Uhamasishaji ya Serengeti Boys iliyoongozwa na Bw Charles Hilary. Uhamishaji wao ulikuwa ni mkubwa sana na uliamsha ari ya Watanzania kuhamasika na kushangilia timu. Shukrani sana kwa wadau wote waliochangia timu na shukrani sana kwa waandishi wa habari na wasimamizi wa blogu mbalimbali na ma admin wa makundi mbalimbali ya mitandao waliohamasisha na kuichangia timu. 
 
MPANGO WA BAADAYE WA SERENGETI BOYS. 

Kikosi hiki cha Serengeti Boys kilichoshiriki fainali hizi sasa kimebadilika na kuwa rasmi timu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 20 NGORONGORO HEROES. Timu hii mwaka kesho itashiriki katika hatua hatua za kufuzu kucheza fainali za Afrika umri chini ya miaka 20 Afcon U20. Fainali hizi zitafanyika mwaka 2019. Benchi la ufundi la timu hii linaandaa program ya maandalizi ya kikosi hiki ambayo itahusisha kambi na mechi za majaribio ndani na nje ya nchi. 
 
FAINALI ZA AFRIKA ZA VIJANA UMRI CHINI YA MIAKA 17(AFCON U17) MWAKA 2019. 

Tanzania itakuwa mwenyeji wa fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tarehe 28 Mei 2017 baada ya mchezo wa fainali za Afcon U17 Rais wa CAF Bw Ahmed aliikabidhi rasmi Tanzania uenyeji huu kwa njia ya ishara ya kumkabidhi Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa Selestine bendera ya CAF, tukio ambalo lilishuhudiwa na dunia nzima. Tunamshukuru. 
 
Taratibu za kuandaa fainali hizi zitaratibiwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya TFF na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo. Ni Imani ya Shirikisho kuwa Tanzania itaandaa fainali nzuri na za kihistoria. TFF inatoa rai kwa wadau wote wa mpira wa miguu Tanzania tushirikiane ili tuzitumie fainali hizi kujenga jina la nchi yetu kimichezo, kiutamaduni, kiutalii na kiuchumi. 

Kwa kuwa Tanzania itakuwa ni mwenyeji wa mashindano haya moja kwa moja imefaulu kucheza fainali za mashindano, hivyo Tanzania tutacheza fainali hizi za Afrika mara mbili mfululizo, jitihada zitafanyika kuhakikisha kombe hili linabakia nyumbani. 

Maandalizi ya timu itakayoshiriki fainali hizi yalianza mwaka 2015 ambapo TFF iliandaa mashindano ya kitaifa ya vijana umri chini ya miaka 13 (U13). Katika awamu ya kwanza ya maandalizi haya Vijana 22 bora waliopatikana kwenye mashindano haya walikusanywa pamoja na kwa ruhusa ya wazazi wao walipatiwa shule ya kusoma pamoja ambapo wanapata fursa ya kusoma na kufanya mazoezi ya pamoja. 

Shule hii iko mjini Mwanza. Awamu ya pili itakayoanza mwezi Julai itahusisha vijana hawa kuongeza kasi ya mazoezi na hivyo itabidi wasome katika shule iliyokaribu na benchi la ufundi la timu hii ambayo sasa ndiyo rasmi SERENGETI BOYS. Shule hii tayari imekwisha patikana hapa Dar es salaam na taratibu za masomo yao zinaandaliwa. 

Tunawashukuru wazazi wa watoto hawa kwa kutoa ushirikiano kwetu, pia tunaishukuru shule ambayo wamekuwa wakisomea kwa ushirikiano wao. Mwezi Julai timu hii itacheza mechi mbili za majaribio za kimataifa. Imani ya TFF ni kuwa tutajenga kikosi imara cha Serengeti Boys mpya ambacho kitatoa ushindani na kunyakua kombe la Afcon U17 mwaka 2019. 
 
MFUKO WA MAENDELEO YA MPIRA WA MIGUU 

(TFF FOOTBALL DEVELOPMENT FUND). 
 
Mfuko huu ulianzishwa mahsusi na Mkutano Mkuu wa TFF mwaka 2015 kwa ajili ya kukusanya rasilimali za kuendeshea program za mpira wa vijana na wanawake. Mfuko huu unajiendesha wenyewe chini ya Bodi yake inayoongozwa na Mwenyekiti Bw. Tido Mhando. Hivi sasa mfuko huu unaandaa mpango kazi wa miaka kumi 2017-2027 ambao utahakikisha kuwa kuna rasilimali za kutosha za kuhakikisha: 
 
1. Timu zetu za Taifa za vijana Serengeti Boys,Ngorongoro Heroes na Kilimanjaro Warriors zinaandaliwa vyema. 
 
2. Timu yetu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars inaandaliwa na inafuzu kucheza fainali za Afrika za Wanawake mwaka 2018 huko Ghana na hatimae kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2019 huko Ufaransa. 

Imani ya Shirikisho ni kuwa kutokana na jitihada hizi za kujenga vikosi imara vya vijana vya Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za Afrika huko Gabon, Serengeti Boys itakayoshiriki Fainali za Vijana za Afrika nchini Tanzania mwaka 2019 na Kilimanjaro Warriors (U23) itakayoshiriki hatua ya kufuzu kucheza Olimpiki Tokyo mwaka 2020 kwa pamoja kuanzia mwaka 2020 kikosi kipya cha Taifa (Taifa stars) kitaanza kuonyesha uhalisia wa sura yake, kitalelewa na kitakomaa tayari kushiriki hatua za kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026, hatua hizi za kufuzu kucheza hizi fainali zitaanza mwaka 2024. Shime Watanzania tuunge mkono jitihada hizi, kwa pamoja inawezekana, fainali za Gabon zimetudhibitishia hivyo! 

Mungu ibariki Tanzania. 

Mungu ibariki timu zetu zote zaTaifa. 

Ahsanteni sana. 
 
Jamal Malinzi 
RAIS WA TFF 
DAR ES SALAAM 
02 Juni 2017.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA