SERIKALI YAZIAGIZA TAASISI ZA FEDHA KUWAWEZESHA WAFANYABIASHARA VIJIJINI
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua taarifa ya utekelezaji wa sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2004 kwa mwaka 2021/21 iliyozinduliwa leo wakati wa kongamano la tano la uwezeshaji wananchi kiuchumi Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Geofrey Mwambe akimkabidhi Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa nakala ya taarifa ya utekelezaji wa sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2004 kwa mwaka 2021/21mara baada ya kuizindua leo jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa akibonyeza kitufe kuzindua Kanzidata ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi wakati wa kongamano la tano la uwezeshaji wananchi kiuchumi lilifanyika leo Jijini Dodoma.
Baadhi ya wakuu wa mikoa wakifuatilia hotuba ya Waziri Mkuu, Kassima Majaliwa(hayupo pichani) wakati wa Kongamano la tano la uwezeshaji lilifanyika leo Jijini Dodoma.
Na Ahmed Sagaff - MAELEZO
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imezungumza na taasisi za fedha na zile zinazosaidia kuwezesha wananchi kiuchumi ili kuwawezesha wafanyabiashara wa vijijini.
Hatua hiyo itatatua changamoto ya upatikanaji wa kiwango kidogo cha fedha katika maeneo hayo hivyo kuwawezesha wafanyabishara wanaowekeza vijijini kuendelea.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa alipokuwa akifungua Kongamano la Tano la Uwezeshaji lililozikutanisha taasisi za Serikali na wadau wa uwekezaji kutoka sekta binafsi.
“Tumeshazungumza na vyombo vya fedha ili kuhakikisha wote wanaohitaji mitaji ili waendeshe shughuli zao za kiuchumi wapewe masharti nafuu ya upatikanaji wa mikopo ikiwemo riba nafuu, ikiwezekana mikopo isio na riba,” amefahamisha Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia Uwekezaji, Mhe. Dkt. Geoffrey Mwambe amehabarisha kuwa Serikali imedhamiria kujenga uchumi wa mtu mmojammoja ili kutengeneza mabilionea wa kitanzania.
“Sisi kama watumishi wa serikali kwa nafasi zetu mbalimbali, tuwe chachu ya kufungua fursa kwa watu wetu, tuwe chache ya kuendeleza watu wetu, ni imani yangu kuwa tutafanikiwa katika hilo,” ameeleza Mhe. Mwambe.
Aidha, amefahamisha kwamba Serikali imedhamiria kuzalisha bidhaa nyingi ili kuuza nchini, Marekani, Ulaya na katika nchi 54 za Bara la Afrika ambazo zimeamua kuwa na soko la pamoja.
“Tumedhamiria kama nchi kuhakikisha tunazalisha bidhaa nyingi ambazo tumekuwa tukiziagiza kutoka nje kwa kutumia fedha nyingi za kigeni, lakini tunazo rasilimali na fursa nyingi tunazoweza kuzitumia kuzalisha bidhaa hizo nchini,” amedokeza Dkt. Mwambe.
Tangu alipoingi amadarakani Machi 2021, Rais Samia ameendeleza jitihada za kuwainua Watanzania wenye uchumi wa chini kwa kuwapatia mafunzo, mikopo na kutengea maeneo ya kufanyiabiashara yanayoinua heshima ya wafanyabiashara wadogo.
0 comments:
Post a Comment