TCRA KUSHIRIKIANA NA TBN KUSADIA KUZALISHA MAUDHUI YENYE TIJA
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeahidi kufanyakazi na Mtandao wa Wana Blogu Tanzania (TBN), pamoja na vyama vingine vya waandishi wa habari ambavyo vinawakilisha mahitaji na matakwa ya wanachama wao.
Kauli hiyo imetolewa Machi 19, 2025 Jijini Dar es Salaam na Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, alipokutana na ujumbe wa TBN ofisini kwake, katika kikao cha kujadiliana changamoto mbalimbali zinazowakabili Bloga nchini.
“Sisi huwa tunapenda kufanya kazi na vyama ambavyo vinawakilisha mahitaji na matakwa ya wanachama wao, badala ya kufanyakazi na mwaandishi mmoja mmoja…tunafurahi sana kufanyakazi na waandishi kupitia vyama vyao,” amesema Mhandisi Kisaka.
Mhandisi Kisaka amesema kuwa TCRA imefurahi kukutana na TBN kwa kuwa wanafahamu kuwa Bloga wanasehemu kubwa sana kwenye maudhui ya ndani, na hata kwenye usajili wa TCRA Bloga wanachukua nafasi kubwa sana katika maudhui ya mtandaoni.
“Kwa hiyo TBN mtakuwa silaha moja wapo nzuri sana yakutuwezesha sisi kama Mamlaka ya Mawasiliano nchini, tunao simamia utangazaji pamoja na maudhui ya mtandaoni kuwa karibu na nyinyi na kuhakikisha maudhui ya mtandaoni yanaleta tija na maendeleo kwa wananchi,” amesema Mhandisi Kisaka.
0 comments:
Post a Comment