Tuesday, 1 September 2015

DALILI ZA KISUKARI NA JINSI YA KUJIKINGA NACHO

KISUKARI ni moja ya magonjwa yanayoathiri watu wengi siku hizi nchini mwetu na hata nje.

Kati ya hao, wengi huishi na ugonjwa huo kwa muda mrefu na kuja kugundua kwamba wana
kisukari baada ya muda wa kama miaka mitano hivi, baada ya mwili kuanza kuonesha dalili kuu za kisukari.

Ndani ya kipindi hicho cha miaka mitano, tayari mwili unakuwa umepoteza baadhi ya uwezo wake katika macho, figo, fizi na neva za fahamu. Kisukari hakina dawa ya kutibu kabisa, bali vipo vichocheo (hormone) na dawa zinazosaidia kurekebisha kiwango cha sukari mwilini.
Image result for Kisukari
Kipimo cha ugonjwa wa kisukari


Je, vipi mtu aweza kutambua kuwa na kisukari mwilini? Zipo dalili kadhaa zinazotokea kwa
wenye kisukari. Baadhi ya hizo ni kiu ya maji isiyoisha, njaa kali, kwenda haja ndogo mara kwa mara na vidonda au michubuko kuchukua muda mrefu kupona.

Nyingine ni ngozi kuwa kavu na kuwasha, mgonjwa kupoteza uzito bila sababu, kuwa na ukungu machoni, kuchoka kusiko kwa kawaida, hisia kupungua katika vidole na viganja
mikononi na miguuni na kuwa na ukungu katika fizi, ngozi na kibofu cha mkojo.

Hatua za mwanzo za kisukari huwa na dalili chache sana, hivyo inawezekana kabisa mtu asifahamu kuwa ana kisukari, ingawaje madhara yanaweza kuwa yameshatokea katika macho, figo na mfumo wa usukumaji damu mwilini.

Watu wengi wanaopatwa na kisukari huangukia katika makundi ya wenye umri unaozidi miaka 30, uzito mkubwa na uzito uliokithiri (uwiano kati ya uzito na urefu zaidi ya 25 na 30),
kadhalika, watu wasiofanya shughuli za kuupa mwili mazoezi huwa katika hatari hiyo, kama
ilivyo kwa wale wanaozaliwa katika familia ambayo mmoja kati ya wanandugu wa karibu ana kisukari. Mwanamke kujifungua mtoto mwenye uzito wa zaidi ya kilo nne na aliyekuwa na kisukari cha ujauzito anaangukia pia kwenye kundi hilo, sawa na wale wanaokuwa wamepata ajali na kuumia sehemu za tumboni au kula chakula chenye sumu ambacho kinaweza kuumiza
kongosho.

Upo umuhimu wa kupima kisukari mapema basi, ili kuepuka mtu kuishi nacho kwa muda mrefu pasipo kujua, na kusababisha madhara kusambaa mwilini na kumwathiri mwathirika.
Ni muhimu kuzingatia mazoezi, uzito, lishe na ushauri wa wataalamu wa afya, kwa sababu husaidia kupunguza makali na madhara yatokanayo na kisukari.

Watu wenye kisukari wapo katika hatari zaidi ya kupatwa na magonjwa ya moyo, kiharusi, matatizo na kuharibika kwa kibofu cha mkojo, shinikizo la juu la damu, upofu, kufa neva za fahamu, uharibifu katika fizi na ugonjwa wa fangasi.

Mtu anapokuwa na kisukari, mzunguko wa damu miguuni hupungua na hii ndiyo sababu kubwa ya kufa kwa neva za fahamu na hivyo mtu kukosa hisia katika eneo hilo la mwili.
Matokeo ya hali hiyo ya kutohisi punde mtu anapodhurika na kusababisha kidonda ambacho mara nyingi mhusika anakuwa hafahamu hadi anapofahamishwa na mtu wa karibu au atakapokagua miguu yake.

Hii ndiyo sababu kubwa ya watu kushauriwa kukagua miguu yao kila siku kabla ya kulala kuona kama kuna mchubuko wa aina yoyote au ukucha unaoweza kuchimba ngozi. Kutokuzingatia masharti ya kujikagua huweza kusababisha kidonda kukua, kutotibika na hatimaye mgonjwa kuishia kupoteza kidole, unyayo au hata mguu.

Vile vile, kutokuzingatia masharti ya kujua kiwango cha sukari mwilini huweza kusababisha mtu akapoteza fahamu kutokana na mwili kuzidiwa sukari asidi (diabetic ketoacidosis), na hii huweza kusababisha kifo mara moja.

Mgonjwa anaweza kuzuia madhara yatokanayo na kisukari kwa kuzingatia maelekezo, masharti na ushauri wa wahudumu wa afya, hasa kuhusu chakula na mazoezi na maelekezo ya utumiaji sahihi wa dawa au insulin.

Mgonjwa hatakiwi kuvuta sigara, awe anapima kiwango chake cha shinikizo la damu mara kwa mara na kuhakikisha kiwango chake cha lehemu kipo katika uwiano unaotakiwa. Takwimu zinaonesha kuwa uzingatiaji wa hayo yaliyotajwa umesaidia watu wengi kupunguza madhara
ya kisukari kwa asilimia 75.

Lishe mahsusi kwa mtu mwenye kisukari ni mlo wenye kiwango kidogo sana cha mafuta, kiwango kidogo cha chumvi na kiwango kidogo cha sukari. Mlo uwe na mchanganyiko wa
nyuzinyuzi kama vile dona (unga wa mahindi yasiyokobolewa), nafaka, tambi, ndizi za kupika, mtama, uwele nk.

Vile vile matunda machachu na mboga za majani zilimwazo na zile za porini ziliwazo kama mchunga, tembele, majani ya maboga, majani ya kunde na mbilimbi. Ni vyema kujitahidi kula kiasi kidogo cha chakula walau mara tano kwa siku kuliko mlo mkubwa mara mbili au tatu kwa siku.

Isipokuwa kwa sababu zisizozuilika, mgonjwa asiache kula, kwani ni mbaya kwa utendaji kazi wa mwili. Katika kudhibiti kiwango cha sukari mwilini, ni muhimu mwathirika kupata maelekezo yahusuyo njia na jinsi ya kupima na kujua kiwango cha kawaida cha sukari mwilini.

Watu wengi wenye kisukari huwapasa kutumia aina ya insulin kabla ya kula chakula kulingana na kiasi cha wanga ulio kwenye chakula anachotarajia kula. Kupima wingi wa wanga katika
chakula husaidia kupanga mlo.

Kujitambua wakati kiwango cha sukari kikiwa juu kupindukia ni kwa kupima damu angalau mara tatu kwa siku, ikiwa ni pamoja na kabla ya kwenda kulala. Mara nyingi watu hupima asubuhi au alfajiri wanapoamka, mchana wa adhuhuri au alasiri na jioni au usiku kabla ya kulala.

Ikiwa sukari mwilini ni nyingi kupindukia, inaweza kumlazimu mgonjwa kutumia insulin ya ziada inayofanya kazi ndani ya muda mfupi (short acting insulin) ili kurejesha kiasi cha sukari
katika kiwango cha kawaida.

Mgonjwa atafahamishwa na mhudumu wa afya au daktari kuhusu kiwango cha insulin cha kutumia kulingana na wingi wa sukari aliyo nayo mwilini kwa wakati huo. Licha ya kuwapo wingi wa sukari mwilini, kuna kisukari ambacho mgonjwa huwa na upungufu wake pia.

Matumizi yasiyo sahihi ya insulin au kutokula chakula husababisha kiwango cha sukari kwenye
damu kupungua kuliko kawaida na hivyo mwili kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo.

Dalili za hali hiyo ni kuhisi uchovu bila sababu, kupiga miayo kupindukia, kushindwa kuzungumza au kufikiri vyema, kupoteza stamina, kutoka jasho, kupata vichomi, degedege karibu na kuzimia, kuhisi kuishiwa nguvu au pamoja na kuzimia na mwili kupauka.

Mtu akipatwa dalili hizo inabidi atafute kinywaji kitamu anywe. Aina ya vinywaji vifaavyo ni kama juisi ya matunda (nanasi, zabibu, tufaa, papai ) vile vile soda (si diet soda) au alambe kiasi cha sukari nyepesi (glucose) au pipi.

Baadhi ya maeneo huuza vidonge vya glucagon, ambavyo ni vizuri kubebwa na kuhifadhiwa nyumbani kwa matumizi ya nyakati kama hizo. Glucagon pia hupatikana katika njia ya sindano na hii inaweza kutolewa na mtaalamu au mtu aliyeruhusiwa kuitoa kupitia kwenye mishipa ya
damu (intravenous glucagon injection).

Inawezekana kuishi maisha ya kawaida kabisa ikiwa mhusika atakuwa makini kulinda afya yake
kwa kuzingatia ushauri na mafundisho ya wataalamu wa afya.



0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA