SAMWEL SITTA ASISITIZA KUWA BUNGE LA KATIBA LITATUMIA MUDA ULIOPANGWA
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amewataka wajumbe wa Bunge hilo kutambua kuwa muda wa kuwapo kwa Bunge hilo umewekwa kisheria, hivyo inabidi kazi ya kutunga Katiba imalizike ndani ya muda uliopangwa.
Sitta aliyasema hayo jana baada ya baadhi ya wajumbe kuonyesha kutoridhishwa na kauli yake ya kutaka baadhi ya sura zaidi ya moja za Rasimu ya Katiba ambazo siyo muhimu kujadiliwa kwa siku moja. "Waheshimiwa wajumbe tuelewe kwamba muda wetu wa kuwa hapa bungeni umepangwa kisheria kwamba ni siku 70 tu, zitakapokwisha inabidi tumalize ili taifa liendelee na shughuli nyingine," alisema Sitta
.
.
Awali Sitta aliwaeleza wabunge kuwa baadhi ya Sura za Rasimu ya Katiba ambazo hazihitaji marekebisho makubwa itabidi zijadiliwe mbili au tatu kwa pamoja katika siku moja, ili kuokoa muda, kauli ambayo iliibua minong'ono kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, wakidhani kuwa Mwenyekiti anataka kuwaburuza.
Kwa mujibu wa Sheria namba nane ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 Bunge Maalum la Katiba limepangiwa siku 70 ambazo zinaweza kuongezwa hadi kufikia siku 90 muda ambao Bunge hilo linatakiwa kuwa limekamilisha kazi yake.
Hata hivyo, bado kuna mkanganyiko wa lini Bunge Maalum lilianza kwa mujibu wa sheria, hali ambayo limfanya Mjumbe wa Bunge hilo, Ezekiel Oluoch kuomba mwongozo wa Mwenyekiti akitaka aelezwe kama siku za uhai wa Bunge hilo zilianza kuhesabiwa baada ya kuchaguliwa kwa Mwenyekiti wa kudumu au tangu wakati ule wa Mwenyekiti wa Muda, Amer Pandu Kificho, aliyekuwa akisimamia uandaaji wa Kanuni za Bunge hilo.
Akimjibu Oluoch, Sitta alisema atatoa mwongozo huo baada ya kuwasiliana na wanasheria wakuu wa Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar ili kupata uhakika wa muda rasmi wa Bunge hilo.
0 comments:
Post a Comment