WANAMGAMBO 17 WA AL-SHABAAB WAKAMATWA MKOANI ARUSHA.....WANATUHUMIWA KULIPUA BOMU ARUSHA NIGHT PARK, WAWILI WASOMEWA KESI HOSPITALINI
Polisi imesema imekamata watu 17, wanaotuhumiwa kuhusika na ulipuaji wa mabomu jijini Arusha na usajili wa vijana kwa lengo la kuwasafirisha kwenda nje ya nchi, kujiunga na vikundi vya kigaidi ikiwemo Al shabab.
Pia, watu hao wanatuhumiwa kutaka kulipua maeneo mengine, hasa taasisi za Serikali na maeneo ya mikusanyiko ya watu.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI), Isaya Mungula alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari jijini Arusha, muda mfupi kabla ya watuhumiwa kufikishwa na kusomewa mashitaka hayo mahakamani.
Mungula alisema kukamatwa kwa watu hao, kunatokana na tukio la Aprili 13 mwaka huu saa 1.30 usiku katika baa ya Arusha Night Park .
Katika mlipuko huo, unaosadikiwa kuwa ni wa bomu, watu 14 walijeruhiwa na mmoja, Sudi Ramadhani, alifariki mwezi mmoja baada ya tukio hilo.
DCI Mungula alisema siku hiyo ya Aprili 13 mwaka huu saa 4.28 usiku, bomu lingine lililotengenezwa kienyeji, lilibainika kutegwa katika baa ya Washington, lakini liliondolewa eneo hilo bila kuleta madhara.
Kwa mujibu wa Mungula, baada ya matukio hayo, upelelezi ulianza mara moja. Kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama, sanjari na kupata maelezo ya mashuhuda wa tukio na katika upelelezi, ilibainika bomu la Arusha Night Park na baa ya Washington, yanafanana na yametengenezwa kienyeji.
Kwa upande wa mabomu yaliyotokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasiti jijini Arusha na katika mkutano wa kampeni wa Chadema eneo la Soweto, ni mabomu yaliyotengenezwa kiwandani.
Alisema watuhumiwa hao, pia imebainika wanahusika kufanya mikakati ya mashambulizi katika maeneo mengine na sehemu mbalimbali nchini, ambazo ni taasisi za Serikali na sehemu za mikusanyiko ya watu.
Alitaja waliokamatwa, wakituhumiwa kuhusika na matukio hayo ya ulipuaji mabomu ni Abdallah Labia (34), maarufu kwa jina la Bro Mohamedi , mkazi wa Mang’ola wilayani Karatu Mkoa wa Arusha.
Wengine ni Abdulkarim Hasia (32) mkazi wa Nguselo jijini Arusha, Hassani Said (23) mkazi wa Tengeru wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Pia, wamo wakazi watatu wa Magugu wilayani Babati mkoani Manyara, ambao ni Rajabu Hemedi (28), Ally Kidaanya (32) na Shabani Wawa (22).
Watuhumiwa wengine ni Abdallah Wambura (40) mkazi wa Mromboo –Murriet jijini Arusha, Ally Jumanne (25) mkazi wa Matufa Babati mkoani Manyara na Yassini Sanga (26) mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga.
Watu nane wanaotuhumiwa kukusanya vijana na kuwasafirisha kwenda nje ya nchi, kujiunga na vikundi vya kihalifu ni Swalehe Hamisi (51) mkazi wa Sombetini jijini Arusha, Abdallah Yassini (33) mkazi wa Tunduru, Sudi Nasibu Lusuma (18) mkazi wa mkoani Mwanza na Abdallah Nyakwela (46), mkazi wa Sakina, jijini Arusha.
Watuhumiwa wengine ni Maka Gewa (19) mkazi wa Bunda mkoani Mara, Abdulrazak Mohamed (25) wa Tunduru, Abdallah Labia ‘Bro Mohamedi’ na Hassani Said (23) mkazi wa Tengeru wilayani Arumeru, Arusha.
Mungula alisema Polisi inaendelea kusaka watu wengine 25, wanaotiliwa shaka kuhusika katika matukio ya mwaka jana ya milipuko ya mabomu ya Olasiti na Soweto.
Alitaka wananchi kuendelea kutoa taarifa na ushirikiano kwa jeshi hilo, kufichua wahalifu wa ndani na nje wa matukio hayo.
Watuhumiwa 15 wa mlipuko wa bomu katika baa ya Arusha Night Park waliofikishwa mahakamani jana, walisomewa mashitaka 16.
Miongoni mwa mashitaka waliyosomewa ni kuua, kukusudia kuua, kusafirisha binadamu na kusajili vijana kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab.
Waendesha mashitaka wa Serikali, Khalili Muda na Marcelino Mwamunyange, walidai watuhumiwa waliua na kukusudia kuua Aprili 13 mwaka huu saa 1.30 usiku katika baa ya Arusha Night Park .
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Mustapha Siani, ilidaiwa washitakiwa waliua mtu mmoja na kujeruhi watu 14.
Mwendesha Mashitaka, Muna alisoma mashitaka kwa washitakiwa 13, kati ya 15, waliokuwa kizimbani. Washitakiwa wawili hawakusomewa mashitaka, kwani walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, wakipata matibabu.
Vile vile Mahakama ilihamia katika hospitali hiyo, kusomea washitakiwa hao wawili mashitaka ya kuua, kukusudia kuua, kusafirisha binadamu na kusajili vijana kujiunga na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab
Waliolazwa hospitalini hapo ni Abdulkarimu Hasia (32), mkazi wa Ngusero jijini Arusha na Rajabu Hemed (28), mkazi wa Magugu wilayani Babati.
Walioshitakiwa kusafirisha vijana na kujiunga na kikundi cha kigaidi ni Athumani Labia (34), Ally Kidaanya(32), Abdallah Thabit (32) na Abdallah Wambura (40) . Wengine ni Hassani Saidi (23), Ally Jumanne (25), Yassini Sanga (26) na Shabani Wawa(22).
Washitakiwa sita waliosomewa mashitaka ya kuua na kukusudia kuua ni Swalehe Hamisi (51), Abdallah Yasini (33), Sudi Lusumu (18), Abdallah Nyakwela (46), Maka Gewe (19) na Abdulrazak Mohamed (25).
Wote hawakutakiwa kujibu chochote, kwani mahakama hiyo kisheria haiwezi kusikiliza kesi hiyo, ambayo itatajwa tena Juni 11 na 12 mwaka huu.
NA MATUKIO NA VIJANA
0 comments:
Post a Comment