MAMBO MUHIMU YANAYOMFANYA MTU AYACHUKIE MAPENZI
SIJUI wewe ulikuwa una malengo gani wakati unafikiria kuwa na ambaye unaye; wapo ambao walikuwa na malengo kwamba akiwa na mwanaume, maana yake awe ndio sawa na mashine ya kutolewa fedha maarufu kama ATM.
Ikiwa ulichokuwa unatafuta ni mwanaume au mwanamke ambaye kwako atakuwa ni ATM, kwamba ndiye awe anakupa kila kitu unachotaka, ikiwa hatakuwa na fedha si rahisi mkaendelea kuwa na uhusiano mzuri, kwa kuwa mpango wako haukuwa mapenzi, bali kuchuma fedha na kula raha.
Mwanamke yeyote ambaye anafikiri yuko na mwanaume maana yake ni kwamba awe anamnunulia kila kitu, kwamba kwake mwanaume ni kila kitu, kinywaji anunuliwe, chips anunuliwe nk...kwamba yeye ni mtu wa kupewa tu ofa, maana yake ni kwamba akili yake imekufa.
Kufikiri kwamba kuoana na fulani maana yake ni sasa yeye atakuwa anakusaidia kila kitu milele na kwamba asipofanya hivyo utamdharau, si kitu sahihi.
USIWE NA MATARAJIO MAKUBWA UNAPOINGIA KWENYE NDOA
Unapoingia kwenye ndoa, usiwe na matarajio makubwa sana mazuri. Jambo unalopaswa kufahamu ni kuwa uhusiano ni suala la kawaida, kwamba unakuwa na mtu kwa lengo la kuwa nae kama timu moja kusaidiana katika kuleta maendeleo.Kati ya mambo yanayofanya watu kutofurahia mapenzi, ni pale anapotishwa kwamba labda asipofanya hiki kwa mfano kukusaidia, basi uhusiano wenu utaharibika.
Kuna wanawake utasikia aaah sasa kuna maana gani ya kuwa na mwanaume ikiwa namwomba fedha hawezi kunisaidia? Fikra kama hii ni ya kipuuzi. Wewe kwanini huna fedha? Ndoa ni kusaidiana, sio kugeuzana ATM.
YUKO BIZE NA SIMU, KOMPYUTA NK
Kati ya mambo yenye kutiana ‘kichefuchefu’ katika mapenzi ni pale kwamba uko na mwenzi wako, lakini ni kama wewe ni tambala la deki; yaani yuko bize na simu yake au kompyuta au kitu kingine chochote.
Wengine unakuta labda anawasiliana na wengine kwa mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter nk, kumaanisha kwamba wewe ni muhimu, walio muhimu ni wale ambao anawasiliana nao huko.
KUKOSOANA MBELE ZA WATU AU HATA KUPIGANA
Wapo watu wamekuwa na tabia ya kukosoana au hata kupigana mbele za watu. Kati ya makosa yenye kukera na huenda ukasababisha uhusiano ukabaki historia ni hii...ni vizuri ndugu yangu kujifunza namna ya kuachana na hasira kali.
MATUMIZI MABAYA YA FEDHA NA KUTOKUWA NA MIKAKATI KATIKA MAISHA
Kila mtu Duniani anataka maisha bora, kwa maana hiyo ni furaha ya kila mtu kuona mwenzi wake anakuwa mwenye mikakati imara katika kuimarisha maisha yao.
HUDUMA KWA WATOTO NA FAMILIA
Ukiwa kama baba au mama, unapaswa kutafakari vizuri nafasi yako katika malezi ya familia. Ni furaha ya mke na mume, kuona mwenzi wake anajali watoto na familia kwa ujumla. Je, wewe ukoje? Pata muda kufakari hali ya maisha yako, chukua hatua.
UCHAFU NA KUTOWAJIBIKA
Kuna watu wamekuwa wachafu kupindukia, hata kuoga kabla ya kulala ni shida, wengine kuvaa nguo mpya ya ndani hadi awe na ahadi ya kuonana na nesi au daktari.
Lakini zaidi ya yote, ni muhimu wanaume na wanawake wakafahamu kila upande kwa kawaida huwa na nafasi yake ya kuwajibika.
Hata kama wote mna ajira au fedha, mume anapaswa kuangalia namna ya kumfanyia mkewe mambo kama kununua nguo, chakula ndani nk...kuna wanaume hawa hawajui wake zao wamevaa nini wala hawajui ndani chakula kinanunuliwaje...hili ni kosa. Ndoa ni kusaidiana, kila upande uwajibike, ni nzuri kuwa na vikao vya namna ya kuendesha ndoa yenu.