Tuesday, 6 July 2021

MKE MWEMA NI YUPI..?? SOMO LIKO HAPA


Kijana unataka kuoa, …?’ hili lilikuwa swali la mwalimu mmoja wa chuo kikuu, aliyekuwa kapanga nyumba moja na kaka yangu. Niliwasikia wakiongea na kaka yangu akiwa katika mpangilio wa kuoa, nilikuwa nafika kwa kaka yangu huyo kupata mahitaji ya shule, kwahiyo naweza kulala siku mbili hata wiki na nilikuwa napenda kukutana na huyo mwalimu kwani alikuwa mwepesi kusaidia watu hasa kielimu.

‘Mwalimu ndio lengo langu hilo, ila nashindwa kujua ni nani atakaye nifaa kama mke mwema…’ akamjibu kaka yangu.

‘Najua hilo sana, lnataka kukushauri kwa hilo huenda ikawa hazina yake ya baadaye…’ akasema , huku akionyesha kuwa na furaha kuliko safari ya kwanza  nilipofika na kumkuta kashika shavu kajiinamia, na niliogopa hata kumsogela kwa kipindi hicho, halafu ukizingatia kuwa mtu mwenyewe  ni mwalimu, tena mwalimu wa chuo kikuu. Leo namuona anafuraha kuliko wakati wa mwanzo.

‘Kijana ukitaka kuoa, uwe na mambo mawili makubwa ya kufikiri kichwani mwako, kwanza kabla ya hayo mambo mawili unatakiwa ujijue wewe mwenyewe upo katika ngazi gani, kielimu na kimaisha. Kielimu nikiwa na maana wewe mwenyewe umesoma hadi ngazi ipi, kimaisha je upo katika hali gani, ya juu au ya kati au ya chini. Ni muhimu sana kujijua wewe mwenyewe kwanza, kabla ya kumtafuta mwenzako!

‘Nachukulia wewe kama mfano wa hili ninalotaka kukushauri, najua  umesoma hadi chuo kikuu, kwahiyo wewe unatakiwa ukitaka kuoa uangalie mke mwenye sifa mbili, awe na mojawapo au zote mbili. Kwanza angalia `imani yake ya dini’ Kama ni mcha mungu wa kweli utapata faida kubwa sana, kwasababu huyu mke ana elimu ya kiroho, na wakati wote ataishi na wewe akisimamia miongozo ya dini. Inaambiwa kuwa , mke hataweza kuupata ufalme wa mbingu kama hana radhi ya mumewe, au sio. Kwahiyo ukimpata  mke mcha mungu, huyo atayajua msharti ya ndoa, na  hata kukusaidia wewe, na pia  kukilea kizazi chako katika msingi huo wa kiimani ya dini yake.

`Jambo la pili ni Mke mwenye elimu , …huyu ni mbunifu, mawazo yake yanaona mbali, hayaishii kwa kuangalia  ya leo-leo, huyu atakusaidia sana katika maisha yako kwani utakuwa umepata jembe la pili, wewe ukiwa jembe la kwanza, na naomba sana uangalie tofauti yako ya kielimu na huyo utakayemuoa, msipishane sana, kwani mkipisha sana hata mawazo yetu yatapishana sana, leo unaongea hili mwenzako analitafsiri vingine, kwasababu elimu yake haijampanua kimwazo.

 ‘Hili nikuambialo ni uzoefu nilioupata, nafikiri ulishangaa ulipoona mabadiliko niliyo nayo. Kwanza nilimuoa binti wa darasa la saba toka kijijini. Niliishi naye kwa shida sana, kwanza nilijaribu kumvuta kielimu akawa havutiki, nilijaribu kumuelimisha kimazingira, kiutendaji, kinamna nitakavyo kwasababu ya shughuli zangu za shule, akawa haelewi…mimi natakiwa niwe na vitabu wakati wote, yeye anadai namtenga, vitabu ndio mke wangu… unajua kazi yangu chumba na kila kitu kinatakiwa kiwe kielumu elimu, lakini ilikuwa vigumu sana.Siku moja nikajikuta nimemtamkia neno moja ambalo lilitibua ndoa yangu. Lilinitoka tu na sikuwa na maana hiyo aliyoifikiria yeye. Nilimwambia kuwa; `hajui mapenzi..’ ikawa nongwa.

 Ikafikia mpaka tukakosana kabisa, kwani toka siku hiyo akawa kaninunia hawajibiki kwa vyovyote vile nikimuuliza kisa nini anasema `mtafute mke anayejua mapenzi, mimi sijui mapenzi.’ Ikawa ndio kauli yake hata pale nilipojaribu kumuelimisha kuwa sikuwa na nia mbaya, lakini wapi, akafikia mpaka tukakosana kabisa, …hakuna cha usuluhishi wala nini… mpaka nikaona heri tuachane kwa heri…kweli tukaachana .Nilikaa kidogo , baadaye nikapata mtu, niliyeona ananifaa, nikiwa nimefanyia kazi nani anayenifaa, kwa vigezo vyangu, kwasasa nikaoa mke wa kidato cha sita,ambaye sasa namwandaa kwenda chuo kikuu. Sio kwamba nakuambia kuwa wanawake wasiosoma hawafai, ila naangalia katika swala la kuelewana na kukwepa migogoro isiyo na lazima…

 ‘Siku moja nikataka kufanya majaribio na huyu mke mpya, lakini nikiwa na machale…kwasababu nilishamjua, lakini mikataka kuhakiki. Mke huyu alinipendezesha kila kitu, kama nitakavyo, anajua mimi ni nani na nataka nini kwa wakati gani. Nikaamua tu kumwambia kama nilivyomwambia yule wa kwanza, nikasema `wewe hujui mapenzi…’ akasema eti nini, haiwezekani.Ooh, nikaona nimelikoroga kama yule wa kwanza.

 Kesho yake nyumba ikaanza kujaa vitabu , vijarida, mara kanda za video, na ukiziangalia zote zina kichwa cha habari kizungumziacho mapenzi, ..nini maana ya mapenzi, mapenzi kati ya mke na mume,…na kadhalika, nikashangaa na kumuuliza mke wangu , vipi unataka kufungua shule ya mapenzi humu ndani , hutaamini jinsi alivyonijibu, alisema hivi.

‘Wewe niache tu, …mmmh, nataka kujifunza mapenzi  ni nini… kwasababu naona sijayajua hayo mapenzi kwa kauli yako, sasa nataka kukudhihirishia kuwa kweli najua mapenzi , na kama nisipofanya hivyo nitakuwa sina baraka za mume…, Basi mwalimu alisema alimfuata pale mke wake lipokaa na kumkumbatia huku machozi yakimlenga lenga na baadaye akatoka mle ndani huku anashukuru mungu kuwa kweli nimempata mke mwema, mke niliyekuwa nikimtaka.

‘Kwahiyo kijana nakupa maneno haya huenda siku moja yatakusaidia.

 Jamani mimi nimeona niliweke hili kama wazo langu la Ijumaa ya leo hasa kwa wale wanaotaraji kuoa, au kuolewa tuangalie hayo maneno ya mwalimu. Sijui yana ukweli gani kwako katika maisha ya ufahamu, sijui yatakusaidia vipi, ila langu nikuweka kile nilichojifunza, kama kitakusaidia nitashukuru.

Na kama mumeshaoana, au mpo katika idara nyeti, uongozi nakadhalika ni vyema tukajifunza,  huo ushauri, kwanii hauishii tu kwenye mke na mume. Lakini unakwenda hadi kwa mtawala na mtawaliwa, kiongozi na muongozwa,  huyu na yule …pale tunapokoselewa, tutafakari kwanza, tusichukulie jaziba, na hisia zetu kwa haraka haraka, na sio busara tukakimbilia kulaumu na kumchukia yule aliyetushauri, Kwanza tujiulize kwanini `nikaambiwa hivyo..sijui, au siwezi, au…nimeshindwa madaraka nk.., na tujiulize  kwa kusoma ili kukijua kile nilichokosolewa nacho kina ukweli gani, kwasababu kama binadamu hatuwezi kujua kila kitu…kuambiwa hujui sio dhambi…dhambi ni kutotaka kujua, na huwezi kujua bila kusoma.

 Huwa najiuliza mara nyingi, ukitaka kuwa dakitari, au mhasibu, au nani vile, utaenda shule, utasoma, lakini mbona `hatutakii kuyasoma mapenzi kabla ya ndoa, ukijua kuwa hayo ni nusu ya maisha yako…linasikitisha sana ukiona migongano ya ndoa na ukichunguza sana ni kwasababu tumelichukulia hili kama `lipolipo tu, kiasili…’ fanyeni utafiti wa kina ilimyafaidi mapenzi yenu ya usoni…,Jamani huenda kweli ukaambiwa hujui na kweli hujui, kwanini usiifunze ukajua, unakimbilia limbwata, unakimbilia kuhukumu, unakimbilia kuweka ndani, …mabavu nk. Kama  unajua ulichoshutumiwa nacho soma, tafiti, utajua zaidi na utamsaidia huyo aliyesema hukijuikwa kumuelekeza  kwa tafiti yakinifu, lakini fanya hivyo baada ya kusoma, au kufanya utafiti uliokubalika!

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA