WATANZANIA WATAKIWA KUTUNZA MAZINGIRA KWA FAIDA YAO
WAKATI mvua zikiendelea kunyesha ndani na nje ya jiji la Dar es salaam, Watanzania wametakiwa kutunza mazingira yanayowazunguka ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kuhatarisha maisha yao.
Akizungumza na Funguka live blog jijini jana, Mwenyekiti wa mtaa wa Kigogo darajani, Bakari Nnyange, alisema kuwa kijiografia wakazi wengi bado hawana elimu kuhusu utunzaji wa mazingira katika kipindi hiki.
Aliwataka wananchi kuwa makini na utupaji taka hovyo kwani imebainika kuwa ni chimbuko la magonjwa hatarishi hasa kwa watoto ambao wanaishi na kulelewa kwenye mazingira yasiyo salama.
“Kuna haja ya wananchi wenyewe kuangalia njia ya kuepukana na magonjwa ya mlipuko, sio kila kitu mnasubiri kufanyiwa na serikali, usafi ni jukumu la kila mtu, na usafi wa mtu uanzia nyumbani kwake” alisema Nnyange.
Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Kheri Kessy alisema asilimia 70 ya makazi ya wananchi wa Dar es Salaam, yamejengwa kiholela.
Aliongeza kuwa kutokana na jiografia hiyo asilimia 30 tu ya makazi ndiyo yaliyojengwa katika mfumo rasmi, jambo ambalo linailazimu serikali kwa sasa na baadaye kutumia kiasi kikubwa cha fedha cha kutafuta eneo mbadala kwa ajili ya wananchi wake.
“Mwito wangu kwa taasisi za serikali na binafsi kutumia kila fursa zinayopatikana , katika kubadili maisha ya Watanzania, pia wananchi waelewe kuwa serikali ina changamoto kubwa ya kukabiliana na tatizo hilo” alisema Kessy.
0 comments:
Post a Comment