Mbunge Bahi, Omary Badweli, Ashinda Kesi ya Kuomba RUSHWA
10:11 | No Comments |
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru Mbunge wa Jimbo la Bahi mkoani Dodoma, Omary Badweli, aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka mawili ya kuomba na kupokea rushwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Mkuranga.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Hellen Riwa, alisema mahakama imemwachia huru mshtakiwa huyo kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa huyo.
Alisema katika ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haioneshi wazi kwamba mbunge huyo aliomba na kupokea kiasi hicho cha fedha.
Alisema kwa hadhi aliyokuwa nayo mbunge hawezi kuchukua wala kuomba rushwa sh. milioni moja na kuhoji kama mbunge anafanya hivyo na watu wa chini wafanyaje.
Mbali na kumwachia huru mshtakiwa huyo pia, hakimu alimuonya mshtakiwa huyo awapo jimboni kwake kujihadhari na kuepuka kushika vitu vya watu ili aweze kujilinda na vitu kama hivyo.
"Kama una tofauti na watu katika jimbo lako kuwa makini na ujihadhari pamoja na kujirekebisha kama una tabia ya kuombaomba jirekebishe na kuepuka kugusa vitu vya watu," alisema hakimu.
Alisema mahakama hiyo haikutia shaka pale mshtakiwa alipojitetea mwenyewe na kukana kufanya makosa hayo.
"Kutokana na ushahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kuithibitishia mahakama pasipo shaka kwamba mbunge huyo ametenda makosa hayo, mshtakiwa upo huru kuanzia sasa," alisema.
Badwel alikuwa akabiliwa na shitaka la rushwa ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Mei 30 na Juni 2, 2012, katika maeneo tofauti mkoani Dar es Salaam ambapo alishawishi apewe rushwa ya shilingi milioni 1 kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Sipora Liana.
Kesi hiyo ambayo imedumu kwa takriban miaka mitatu sasa ilifikia tamati jana kwa mbunge huyo kuachiwa huru.
Awali wakati kesi hiyo ikiendelea kunguruma mahakamani hapo mshtakiwa huyo katika utetezi wake alidai hajawahi kuomba wala kupokea rushwa ya sh. milioni 1 kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Sipora Liana wala kuwa na nia kama hiyo.
Wakati huo huo, Mahakama hiyo imeahirisha kesi ya mauaji inayowakabili washtakiwa 11 wanaokabiliwa na shtaka la kumuua kwa kukusudia aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi kutokana na upepelezi kutokamilika.
Mbele ya Hakimu, Thomas Simba, wakili wa Serikali Honolina Munisi, aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa upelelezi haujakamilika.
Hata hivyo, Hakimu Simba, aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 12, mwaka huu.
Washtakiwa hao ni Chibago Magozi (32), Juma Kangungu (29), Msungwa Matonya (30) na Mianda Mlewa (40) wote wakazi wa Vingunguti, Dar es Salaam na John Mayunga (56) mkazi wa Kiwalani.
Wengine ni aliyekuwa mlinzi wa marehemu Dkt. Mvungi, Longishu Losingo (29), dereva na mkazi wa Kitunda, Masunga Makenza (40), mkazi wa Tabata Darajani, Paulo Mdonondo (30), mkazi wa Buguruni, Zacharia Msese (33) na mkazi wa Mwananyamala, Ahmad Kitabu (30)
0 comments:
Post a Comment