Wednesday 27 May 2015

TUSITUMIE PLASTIKI KUHIFADHIA VYAKULA HASA VYA MOTO

Uki-google online madhara ya kutumia plastiki katika kubeba ama kuhifadhia vyakula, utakutana nayo mengi ikiwa ni pamoja na kansa. Pamoja na hilo, pia wanasayansi wametahadharisha kuhusu matumizi ya vyombo vya aluminium kama vile foil papers na kontena, vinavyotumika kufungashia, kubebea na kulia vyakula mathalan mishikaki inayofungashwa hivyo al maarufu 'nyama ya foil' (bofya hapa kurejea) au chips, wali, ugali, mihogo nk. Vile vile tumeaswa kuhusu matumizi ya vyombo vilivyopakwa dawa maalumu ili kuzuia kunata, kuganda na kuungulia 'non stick' (bofya hapa kurejea).
Kwa kuwa bado haijafahamika moja kwa moja kinachosababisha baadhi ya aina ya saratani (cancer) ni vyema kuchukua tahadhari ili kujizuia tusijiweke katika hali rahisi ya kupata ugonjwa huo kwa kutumia vitu ambavyo vimeshachunguzwa na kuonekana na walakini.
 Habari ifuatayo kuhusu plastiki imechapishwa jana katika gazeti la MwanaHALISI Online...
WANANCHI wameshauriwa kutotumia mifuko ya plastiki na vifungio vyake kwa ajili ya kuwekea au kuifadhi chakula na badala yake watumie vifungashio vya glasi na chuma isiyoshika kutu na vyombo vingine vya asili.
Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Stephen Maselle, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mkiwa Kimwanga (CUF).
Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inasema nini kuhusu tatizo kubwa la uchafuzi wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki.
Pia, alitaka kujua kama kuna madhara yanayoweza kusababishwa na uwekaji wa chakula cha moto kwenye mifuko hiyo.
Akijibu swali hilo, Maselle amesema madhara yanayoweza kusababishwa na uwekaji wa chakula cha moto katika mifuko ya plastiki ni pamoja na kuwepo kwa uwezekano wa kemikali zilizotumika kutengeneza mifuko hiyo kuingia kwenye chakula na kukifanya kuwa na sumu.
“Sumu hii yaweza kusababisha saratani, kuharibu ukuaji wa mfumo wa uzazi hususani kwa watoto ambao bado kuzaliwa, mabadiliko ya kijenetiki, matatizo ya kushindwa kuona, uyeyushaji wa chakula tumboni kuwa wa tabu au kutokamilika na ini kushindwa kufanyakazi vizuri,” alisema.
Ametaja magonjwa mengine yanayoweza kusababishwa na mifuko hiyo kuwa ni pamoja na kuharibika kwa mfumo wa utendaji wa figo na magonjwa yanayaohusiana na mfumo wa kupumulia.
Kuhusu uchafuzi wa mazingira, amesema serikali inatambua kuwepo kwa uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.
Maselle amefafanua kuwa, ili kukabiliana na tatizo hilo, serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo yenye unene wa chini ya maikroni 30 na kuhamasisha matumizi ya mifuko mbadala.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA