Wednesday 20 May 2015

ZAIDI YA 6,000 WAGOMA UDSM

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala (katikati) akizungumzia moja ya migomo ya wanafunzi wa chuo hicho.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala (katikati) akizungumzia moja ya migomo ya wanafunzi wa chuo hicho.
ZAIDI ya wanafunzi 6,000 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya Mlimani, wanaodai fedha za kujikimu kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini (HESLB), jana waligoma kuingia darasani wakishinikiza kulipwa fedha zao.
Kwa ujumla, wanafunzi hao wanaosomea fani mbalimbali, wanadai zaidi ya Sh bilioni 2.8. Makamu Mkuu wa chuo hicho kikongwe zaidi nchini na maarufu barani Afrika, Profesa Rwekaza Mukandala alikiri kuwepo kwa mgomo huo.
Alithibitisha kuwa wanafunzi wawili walijeruhiwa na kulazwa katika zahanati ya chuo hicho, kutokana na vurugu za hapa na pale.
Alisema kutokana na vurugu hizo, kumetokea uharibifu katika hosteli za chuo hicho, ikiwemo ya Mabibo kutokana na wanafunzi hao kugoma kuhudhuria masomo, badala yake wakaanza kufanya uharibifu.
Aliongeza kuwa wanafunzi wanaokaa katika hosteli ya Mabibo, walifanya uharibifu asubuhi na uongozi umefanya ufuatiliaji na kubaini kuwa baadhi yao hawakuingia darasani, na badala yake kujikusanya katika vikundi na wengine wakijikusanya katika bwalo la chakula chuoni hapo.
"Wanafunzi walikuwa wanategemea malipo kuanzia wiki iliyopita. Ilipoanza jana (juzi) wakaleta malalamiko yao tukafanya jitihada nyingi, tukaamua chuo kitawasaidia fedha kidogo mpaka watakapopata," alisema.
Aliongeza kuwa kufikia jana Hazina (Wizara ya Fedha) waliuhakikishia uongozi wa chuo hicho fedha hizo zingelipwa kufikia jana jioni.
Katika maeneo ya chuo, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutoka Jeshi la Polisi walifurika kwa lengo la kuchukua tahadhari za kiusalama chuoni hapo.
Waziri wa Mikopo katika Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo, Shitindi Venance alisema fedha za kujikimu wamekuwa wakipatiwa kila baada ya wiki nane, sawa na miezi miwili, lakini hadi sasa wamevumilia na kuchoka.
Kila mwanafunzi anastahili kulipwa Sh 450,000. Mbali na fedha za kujikimu, pia alisema zipo dalili za kucheleweshewa ama kutopatiwa fedha za mafunzo kwa vitendo kwa kuwa muda wa kupewa fedha hiyo umekaribia huku dalili zikiwa hazionekani.
Wanafunzi hao waligoma jana kuingia madarasani huku wengi wao wakibaki wakiwa wamejikusanya vikundi katika eneo la karibu na bwalo la kulia chakula huku wakiimba njaa inawasumbua.
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisoba alikiri kuwapo kwa tatizo hilo. Aliwataka walioathirika na ucheleweshaji huo, kuwa na subira kwa kuwa taratibu za kuwalipa, zilikuwa zinafanywa.CHANZO:HABARI LEO

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA