GWAJIMA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI JIJINI DAR ES SALAAM
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amejitokeza leo na kujibu tuhuma zilizotolewa dhidi yake na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa wiki moja iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Askofu Gwajima amekanusha tuhuma za kuwa alimwambia Dk Slaa kuwa wapo maaskofu ambao walihongwa na mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa na kuitwa mshenga wa mgombea huyo.
Askofu huyo amesema kuwa hajawahi kumwambia Dk Slaa kuwa maaskofu wa Kikatoliki wamehongwa na Lowassa ili wamchague hivyo aliyoyasema Dk Slaa ni kuwachafua viongozi hao wa dini.
Wakati Dk Slaa anatangaza kustaafu siasa Septemba Mosi, alimwita kiongozi huyo wa Kiroho kuwa ni mshenga wa Edward Lowassa kwa Chadema na kusema kuwa askofu huyo alimwambia kuwa wapo maaskofu 30 wa Katoliki wamehongwa na Edward Lowassa.
Licha ya kukanusha tuhuma hizo, Akofu Gwajima amesema kuwa kuna watu wanawatumia Dk Slaa na mchumba wake, Josephine, na kuwaonya waache kutumika.
Pia Askofu Gwajima ametoa tuhuma kwa Usalama wa Taifa kuwa wanatumika pamoja na Dk Slaa.
“Mimi najua wapo Usalama wa Taifa ambao wanamlinda Dk Slaa lakini nawaomba sana Usalama wa Taifa walinde nchi ikae kwa amani, wasijiingize kwenye siasa au kulinda kikundi flani’’ alisisitiza Gwajima.
Aidha askofu huyo amesema kuwa kama Dk Slaa atajitokeza kumjibu kwenye vyombo vya habari, na yeye atajitokeza kuelezea mambo aliyoyafanya Dk Slaa Afrika ya Kusini akiwa na vijana wa Usalama wa Taifa siku chache kabla ya kutangaza kuachana na siasa.
Kiongozi huyo wa Kiroho amewataka wananchi waangalie ni mtu yupi anayefaa na wasije wakagawanywa na harakati zinazoendelea.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment