Wednesday, 27 January 2016

RAIA WA KENYA ADAIWA KUITEKA MANISPAA YA ILALA


Mjane Tabu Salum Tambwe


Na Dotto Mwaibale,

MTU mmoja ambaye ametajwa kuwa ni raia wa Kenya anadaiwa kuiteka Manispaa ya Ilala kwa kushiriana na watendaji wasio waaminifu wa manispaa hiyo kudhulumu viwanja vya watu eneo la Pugu Mwakanga.


Raia huyo wa Kenya ametajwa kuwa ni Phinians Otieno ambaye amefungua ofisi yake eneo la Pugu Kinyamwezi Chanika ili kuwa jirani na viwanja ambavyo inadaiwa anaviuza kiujanjajanja kwa kushirikiana na watendaji wa manispaa hiyo wasio waaminifu akiwemo ofisa ardhi mwandamizi mmoja na ofisa mwingine wa manispaa hiyo ambao majina yao yanahifadhi.

Imeelezwa kuwa katika manispaa hiyo mkenya huyo ana ndugu zake watano ambao wameajiriwa hapo akiwepo shemeji yake ambao wanampa siri ya viwanja vilipo na kukamilisha udhulumaji wa viwanja vya wananchi hasa katika maeneo ambayo hayajapimwa na amekuwa akitamba kuwa hakuna mtu wa kumbabaisha kwani hata waziri Lukuvi anafahamiana naye.

Imedaiwa kuwa raia huyo wa kenya aliingizwa katika mchongo huo wa viwanja na kigogo mmoja wa manispaa hiyo ambaye alitimuliwa kutokana na kujihusisha na vitendo vya rushwa ambaye alimpa tenda ya kuwapimia viwanja wananchi waliohamishwa Kipawa kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege katika eneo hilo la Pugu Mwakanga na baada ya kupima viwanja hivyo ameingia eneo la wakazi wa Mwakanga akidai ni lake.

Katika tukio la aina yake ni jaribio la mkenya huyo la kutaka kumpora viwanja mjane mmoja wa eneo hilo Tabu Salum Tambwe (pichani) akidai ni vyake kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wa manispaa hiyo.

Viwanja vya mjane huyo ambavyo anataka kudhulumiwa na mkenya huyo ni 869-876 vilivyopo Kitalu 'N' Pugu Mwakanga ambavyo mjane huyo amekuwa akivilipia kodi tangu avinunue lakini kutokana na mchezo mchafu unaofanywa kwa ajili ya kutaka kumdhulumu amekuwa akipigwa chenga ya kumilikishwa licha ya kutoa zaidi ya sh.milioni 21.

Akizungumza na gazeti hili Tambwe alisema amepoteza fedha nyingi kwa ajili ya kupata umilikishwaji wa viwanja hivyo ambavyo anataka kudhurumiwa.

Tambwe alisema kuwa tangu avinunue viwanja hivyo mwaka 2007 amekuwa akivilipia kodi na mara ya mwisho kuvilipia ilikuwa mwaka juzi ambapo alilipa sh.640,000 na kukabidhiwa stakabadhi namba 356568, 356569, 356570, 356565, 356567, 356565, 356563.

Mjane huyo alisema changamoto kuwa iliyopo ni kuhusu umilikishwaji wa viwanja hivyo ambapo aliambiwa ni lazima alipie kabla ya kupewa ofa ambapo katika kiwanja namba 872 alilipa sh.224,402.80, 876 alilipa sh.281,118.40, 870 alilipa sh. 247,964.80, 874 alilipa sh. 244, 567.20, 875 alilipa sh. 303,668.40, 873 alilipa sh.270,350.40 na kiwanja namba 871 alilipa sh.270,131 jumla ikiwa ni sh.milioni 21.2 fedha alizolipa kwa mkabidhi keshia mmoja ambaye yupo dirisha la malipo aliyemtaja kwa jina moja la Fatuma lakini hadi leo hii bado hajamilikishwa.

Hata hivyo baadhi ya maofisa wa manispaa hiyo wameoneshwa kukerwa na vitendo vinavyofanywa na mkenya huyo kwa kushiriana na wenzao na wamesema kuwa wapo tayari kutoa ushirikiano kwa Waziri Lukuvi ili kumsaidia mjane huyo apate haki yake kwani katika manispaa hiyo  wao wanaonekana kama ni takataka na mkenya huyo anaonekana ni mungu mtu.

"Tunawaombeni wanahabari mutusaidie katika jambo ili kwani watu wengi wanaendelea kuumizwa na watendaji wenzetu wasio waaminifu wakishirikiana na mkenya huyo ambaye si raia hapa nchini lakini amekuwa milionea kwa kuuza ardhi kiujanjaujanja sisi tupo tayari kusema ukweli" alisema ofisa mmoja wa manispaa hiyo kwa uchungu.

Imeelezwa kuwa mkenya huyo kwa wakazi wote aliyewauzia viwanja katika eneo hilo amekuwa akiwatoza kodi ambayo ilipaswa kulipwa serikalini lakini uichukua na kuitia mfukoni mwake.

Mjane huyo anamuomba Waziri Lukuvi kumsaidia ili apate haki yake ambayo ipo hatarini kupotea kupitia watumishi wa waliochini ya wizara yake wanaoshirikiana na raia huyo wa Kenya.

Akitoa ufafanuzi wa madai hayo mkenya huyo alidai kuwa mama huyo alitapeliwa kwa kuuziwa viwanja hivyo ambavyo si vyake na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Dullah na kwamba yeye alikuwa akimsaidia ili kupata haki yake.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA