TAASISI YA TANZANIA WOMEN OF ACHIEVEMENT (TWA) YAZINDUA KAMPENI YA UWIANO WA KIJINSIA
Rais
wa Taasisi ya TANZANIA WOMEN OF ACHIEVEMENT (TWA) (TWA), Irene Kiwia
(katikati ) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani )
kuhusu uzinduzi wa kampeni ya uwiano wa kijinsia ambayo ni kauli mbiu
kuelekea kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani, kushoto kwake ni
Balozi wa kampeni ya uwiano sawa kijinsia Inspk.Prisca Komba na kulia
kwake ni Mwenyekiti wa TWA, Sadaka Gandi kwenye mkutano uliofanyika
mapema leo jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti
wa Taasisi ya TANZANIA WOMEN OF ACHIEVEMENT (TWA), Sadaka Gandi
akifafanua jambo kuhusu uzinduzi wa kampeni ya usawa wa kijinsia
kwenye mkutano na waaandishi wa habari uliofanyika mapema leo jijini Dar
es salaam.
Waandishi
wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakisikiliza kwa makini
maelezo kutoka kwa Rais wa TWA Irene Kiwia kuhusu uzinduzi wa kampeni
ya usawa wa kijinsia katika mkutano uliofanyika mapema leo Jijini Dar es
salaam .
Dar es Salaam, Februari 17, 2016
Taasisi
ya TANZANIA WOMEN OF ACHIEVEMENT (TWA) imetangaza uzinduzi wa kampeni
ya uwiano wa kijinsia kwenye kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani ya
Wanawake inayotoa wito kwa kila mtu kuchukua hatua za dhati kusaidia
upatikanaji wa usawa wa jinsia kwa kasi zaidi ili kuwasaidia wanawake na
wasichana kufikia malengo yao.
Hali
kadhalika inatoa wito kwa jamii kuwa na uongozi ulio na usawa wa
kijinsia, kuheshimu na kuthamini tofauti bainia ya jinsia, kuanzisha
utamaduni jumuishi na kuondoa upendeleo kwenye sehemu za kazi.
Akizungumza
leo kwenye mkutano wa waandishi wa habari kwenye ofisi za TWA jijini
Dar es Salaam Rais wa TWA, Bi. Irene Kiwia alisema kuwa lengo la
Kampeni ya Uwiano wa Kijinsia ni kutoa wito kwa wanawake na wanaume
kuungana pamoja kusaidia wanawake kufikia hali ya usawa kwa idadi kubwa
na kutambua mchango wao usio na ukomo wanaoutoa kwenye uchumi duniani
kote kwa ujumla hususani nchini kwetu Tanzania.
“Kampeni
ya Uwiano wa Kijinsia inamaanisha kutoa wito kwa wadau wote vikiwemo
vyombo vya habari, watu binafsi, serikali na mashirika yote kutambua na
kujenga uelewa kuhusu mianya inayozuia mchakato wa kuwepo usawa wa
kijinsia na kutaka kuchukua hatua za dhati kuharakisha mabadiliko,”
alisema Kiwia.
“Mwaka
2014 Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum -WEF) lilitabiri
kuwa usawa wa jinsia duniani utafikiwa mwaka 2095. Lakini mwaka mmoja
baadaye, yaani 2015 lilikadiria kuporomoka kwa hatua husika na kupunguza
kasi ya kufikia uwiano kuwa pengo la kijinsia linaweza kuzibwa ifikapo
mwaka 2133. Hii inamaanisha kusubiri kwa miaka 117 ambayo ni mingi sana.
Kutokana na hali hiyo TWA inaungana na wito wa dunia wa kuitaka kila
nchi kuliweka suala la jinsia kwenye ajenda zake na kuharakisha kasi ya
kufikia lengo la usawa wa kijinsia .” alisema Kiwia.
Akitoa
wito kwa watu binafsi, mashirika na wadau wengine kushiriki kwenye
kampeni hiyo Mwenyekiti wa TWA Bi. Sadaka Gandi alisema Kampeni
itahusisha matembezi ya kilomita sita asubuhi ya siku ya tarehe Tano
mwezi March kuanzia kwenye `Viwanja vya Mbio za Mbuzi´ maarufu kama
‘Uwanja wa Farasi’ kupitia kwenye makutano ya Shule ya Kimataifa ya
Tanganyika (IST), kuelekea Kanisa Katoliki la Mt. Petro na kupitia
Ubalozi wa Kenya nchini na kurudia sehemu yalipoanzia.
Bi.
Sadaka Gandi aliendelea kusema kuwa matembezi hayo yatafuatiwa na
mkutano wa kusherehekea siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani ambao
utafanyika Machi 6, 2016 kwenye Hoteli ya Regency Kilimanjaro.
Bibi
Gandi alisema, “Mkutano huu utawakutanisha wanawake na wanaume kutoka
sehemu tofauti ambao watashirikiana na kushawishiana kuungana na
harakati hizi, vile vile tutaonyesha mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa
kutoka Mkutano wa Beijing miaka 21 iliyopita, na hali kadhalika ni
kasoro gani ambazo bado zipo na ni kwa namna gani ushirikiano wa pamoja
unaweza kuharakisha mabadiliko.
Tunaamini mchango wako sio tu kwamba
utachangia msingi wa maendeleo ya wanawake bali pia utaonesha ni jinsi
gani kampuni yako inachangia kwenye upatikanani wa usawa wa kijinsia
kwa ujumla”.
Bibi
Gandi alisema kuwa mkutano huo utazungumzia masuala mbalimbali
yanayomhusu mwanamke kwa kuzingatia elimu, afya, uongozi, haki na sheria
na uchumi.
“Usawa wa jinsia ni muhimu kwa sababu umefungamana na kukua kwa uchumi
kwani maendeleo ya wanawake na uongozi ni nguzo ya ufanisi kwenye
biashara na ustawi wa uchumi”, alihitimisha.
0 comments:
Post a Comment