Monday 1 February 2016

Umoja wa Afrika: Walinda amani kutotumwa Burundi

Umoja wa Afrika: Walinda amani kutotumwa Burundi
Umoja wa Afrika AU umetangaza kuwa, hautatuma kikosi cha kusimamia amani katika nchi ya Burundi inayokabiliwa na mgogoro wa kisiasa na machafuko mpaka pale serikali ya Rais Pierre Nkurunziza itakaporidhia hilo.
Kamishna Mkuu wa Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika Smail Chergui amesema kuwa, Umoja wa Afrika AU, hautatuma majeshi ya kulinda amani nchini Burundi hadi pale watakapopokea mwaliko kutoka kwa taifa hilo la kanda ya Afrika Mashariki. Uamuzi huo umechukuliwa jana na wakuu wa Afrika katika siku ya mwisho ya mkutano wao mjini Addis Ababa Ethiopia. Kauli hiyo ni kinyume na pendekezo la awali la umoja huo ambal uliibua taharuki kuhusu uhalali wake na wajibu wake wa kulinda maisha ya wananchi.
Awali Baraza la Usalama la Amani la Umoja wa Afrika lilikuwa limependekeza kutumwa kikosi cha askari 5,000 nchini Burundi kwa ajili ya kwenda kusimamia amani na utulivu kutokana na nchi hiyo kukabiliwa na machafuko. Inaelezwa kuwa uamuzi huo umechukuliwa baada ya baadhi ya nchi wanachama kupinga mpango wa kutumwa kikosi hicho nchini Burundi.
Burundi inashuhudia mgogoro mbaya zaidi tangu vilipomalizika vita vya ndani vilivyochochewa na ukabila mwaka 2005. Mgogoro huo uliosababishwa na Rais Pierre Nkurunziza kuwania tena urais kwa muhula wa tatu umesababisha mamia ya watu kuuawa na mamia ya maelfu kuihama nchi na kuwa wakimbizi katika nchi jirani. 
-IRAN SWAHILI

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA