KUELEKEA MIAKA 53 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR, BALOZI SEIF ASHUHUDIA MATAYARISHO YA VIKOSI VYA ULINZI NA USALAMA UWANJA WA AMAN
Kikosi cha Bendera cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikikamilisha mazoezi ya mwisho kwa ajili ya kilele cha sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo uwanja wa Aman Mjini Zanzibar.
Makamanda wa JWTZ Wanawake wakati walipotoa heshima yao kwa mwendo wa pole kwenye zoezi la mwisho la matayarisho ya kilele cha sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Vikosi vya ulinzi na usalama vikienda mwendo wa hatua 15 katika Uwanja wa Aman wakikamilisha mazoezi yao ya mwisho kwa ajili ya Kilele cha sherehe za Mapinduzi Januari 12, 2017.
Vijana wa Dr. John Pombe Magufuli (Makomandoo) wakifanya vitu vyao wakati wa mazoezi yao ya mwisho wakijiandaa na kilele cha sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiiongoza Kamati yake katika kufanya tathmini ya Gwaride la maandalizi ya sherehe za Mapinduzi kutumia miaka 53.
Wajumbe wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa wakiendelea na kikao chao hapo ukumbi wa watu mwashuhuri { VIP }Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kushoto akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Nd. Omar Hassan Omar wakikagua ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi hapo Kikiwajuni ulioandaliwa kwa ajili ya Taarab Rasmi ya Kukamilisha sherehe za Mapinduzi.
Balozi Seif akielezea matumaini yake ya kukamilishwa kwa wakati matayarisho ya ukumbi huo. Picha na OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Wakati shamra shamra za sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar zikikaribia hatua ya ukingoni katika maeneo mbali mbali hapa Nchini, matayarisho ya mwisho ya kilele cha maadhimisho hayo kwa upande wa Vikosi vya ulinzi na usalama yamekamilika.
Matayarisho hayo ya mwisho yalijumuisha gwaride rasmi la Vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Polisi, Mafunzo, KMKM, JKU, Magereza, Valantia na Zimamoto na Uokozi yakiambatana na vikundi vya Utamaduni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Balozi Seif Ali Iddi alijumuika pamoja na Makamanda wa Vikosi na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kushuhudia matayarisho ya vikosi hivyo kwenye uwanja wa Aman Mjini Zanzibar.
Askari wa Vikosi hivyo wakiwa makini na hali ya Ukakamavu waliweza kupita mbele ya Mwenyekiti huyo na wajumbe wake kwa mwendo wa pole na ule wa haraka ulioleta burdani safi kwa watazamaji hao.
Wazanzibar na Watanzania wote mwaka huu watashuhudia Kwata maalum ya kimya kimya iliyoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambayo ilikuwa gumzo wakati wa mazoezi yao ya mwisho wakijiandaa na Kilele cha maadhimisho hayo ya kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya maandalizi hayo hapo ukumbi wa Watu mashuhuri Uwanja wa Aman Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Balozi Seif Ali Iddi amepongeza kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Wananchi, Viongozi pamoja na Vikosi vya ulinzi katika maandalizi ya sherehe za mwaka huu.
Balozi Seif alisema Viongozi wa Serikali wanazidi kufarajika kuona kwamba ushiriki wa Wananchi katika kuziendeleza sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 unazidi kuongezeka mara dufu.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliangalia Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar kuangalia matayarisho ya mwisho kwa ajili ya Taarab rasmi na kukamilisha maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 53.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Nd. Omar Hassam Omar alimueleza Balozi Seif kwamba watendaji wa idara ya Sanaa na Utamaduni wanasubiri maelekezo ya wataalamu wa mapambo kukamilisha kazi iliyobaki ya upambaji Ukumbi huo.
Nd. Omar alisema licha ya udogo wa Ukumbi huo lakini mipango iliyoandaliwa kwa ajili ya Taarab hiyo inakwenda vyema ikiwemo kadi maalum zilizoandaliwa kwa burdani hiyo ya Taarab.
Kilele cha sherehe za maadhimisho ya kutimia miaka 53 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 zinatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Aman asubuhi ya Alhamisi ya Tarehe 12 Januari 2017.
0 comments:
Post a Comment