Ziara ya Mhe. Dessalegn inakuja kufuatia mkutano kati yake na Mhe. Dkt. Magufuli uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Kawaida wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mapema mwaka huu.
Mhe. Dessalegn anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 31 Machi, 2017 asubuhi na atapokelewa na Mhe. Rais Magufuli.
Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Ethiopia pamoja na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara.
Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Dessalegn atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili. Aidha, Viongozi hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari.
Jioni ya siku hiyo, Mhe. Dessalegn na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
Tarehe 01 Aprili, 2017 Mhe. Dessalegn ataendelea na ziara yake kwa kutembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kujionea shughuli mbalimbali Bandarini hapo. Mhe. Dessalegn na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Ethiopia.
Mahusiano ya Tanzania na Ethiopia
Mahusiano ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri. Ethiopia imeonesha nia ya kufungua Ubalozi wake hapa nchini hivi karibuni. Kwa sasa Ethiopia inawakilishwa nchini na Balozi wake aliyepo Nairobi, Kenya.
Aidha, kumekuwa na ziara za viongozi wa ngazi mbalimbali wa nchi hizi mbili ili kukuza na kudumisha mahusiano. Ziara hizo ni pamoja na ile ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin Mkapa nchini Ethiopia mwaka 2005. Wakati wa ziara hii Mhe. Mkapa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia wakati huo, Hayati Meles Zenawi walisaini Mkataba wa Jumla wa Ushirikiano.
Vile vile, mwaka 2015 Mhe. Dessalegn alitembelea Tanzania na kushiriki uzinduzi wa Kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wanaoeneza Malaria kilichojengwa Kibaha, Pwani kwa ufadhili wa Serikali ya Cuba. Pia, Mhe. Dessalegn alishiriki sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Mhe. Rais Magufuli zilizofanyika mwezi Novemba, 2015 Jijini Dar es Salaam.
-Mwisho-
0 comments:
Post a Comment