MOI YASAIDIA WATOTO WENYE TATIZO LA KUPINDA MGONGO
Madaktari wakiendelea na kazi ya upasuaji wakati wa kambi maalum ya mafunzo na upasuaji inayofanyika katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa siku tano kwa kushirikiana na Hospitali ya Chuo Kikuu cha WellCornell ya nchini Marekani.
Na Mwandishi wetu- MOI
Watoto 10 wenye tatizo la kupinda mgongo (scoliosis) wanatarajia kuhudumiwa katika kambi maalum ya mafunzo na upasuaji inayofanyika katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa siku tano kwa kushirikiana na Hospitali ya Chuo Kikuu cha WellCornell ya nchini Marekani.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respecious Boniface amesema kambi na mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo madaktari wa Tanzania na nchi nyingine Barani Afrika ili waweze kuwahudumia wagonjwa kwa ufanisi mkubwa.
" Hii ni kambi yetu ya pili, tulifanya kambi ya kwanza mwaka 2019 na mwaka 2020 hatukufanya kwasababu ya changamoto ya Uviko 19. Sasa ndio tumeanza tena na lengo letu ni wataalam hawa wakiondoka tuendelee kutoa huduma hizi hapa hapa bila ya mgonjwa kulazimika kwenda nje ya nchi kufuata huduma hii". Alisema Dkt. Boniface.
Dkt. Boniface amesema watoto 10 watapata huduma ambapo 5 watahudumiwa kwa njia ya kisasa ya P.O.P na wengine watano watahudumiwa kwa kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kunyooshamgongo.
Kwa upande wake, mkufunzi wa mafunzo hayo Prof. Alaa Ahmad kutoka nchini Palestine amesema ni heshima kubwa kupata nafasi ya kuja Tanzania kutoa mafunzo kwa madaktari ili waweze kuwahudumia wagonjwa kwa wakati.
Prof. Alaa amesema ana imani kubwa kwamba mafunzo haya yatawasaidia madaktari wa Tanzania na mataifa mengine na huduma zitaendelea kutolewa hapa hapa barani Afrika.
Washiriki wa mafunzo hayo wanatoka nchi za Tanzania, Malawi na Kenya ambapo Kambi na mafunzo hayo yameratibiwa na Taasisi ya MOI kwa kushirikiana na Hospitali ya Chuo Kikuu cha WellCornell ya nchini Marekani.
0 comments:
Post a Comment