Monday, 11 October 2021

WAZAZI,WAFUNDISHENI WATOTO MATUMIZI BORA YA MITANDAO ILI KUWALINDA


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiangalia baadhi ya shughuli zinazofanywa na vikundi vya wasichana katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike yaliyofanyika Jijini Dar es salaam


Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watoto Nancy Kasebo akipokea cheti cha umahiri katika uongozi wa Baraza la Taifa la watoto Tanzania, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike yaliyofanyika Jijini Dar es salaam.


 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya mtoto Sebastian Kitiku akizungumza na washiriki wa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike Jijini Dar es salaam


Wazazi na Walezi wametakiwa kuwafundisha watoto hususani wa kike matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuwalinda  na ukatili wa kijinsia  ikiwemo udhalilishaji wa kimtandao.


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ametoa wito huo akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike yaliyofanyika Kitaifa Jijini dar es salaam Leo tarehe 11/10/2021.

Mhe. Mwanaidi amesema wazazi wana wajibu wa kuhakikisha watoto wa kike wananufaika na matumizi ya teknolojia na kufahamu umuhimu na mipaka ya yake.

"Hakikisha unakuwa karibu na mtoto na kufuatilia anapotumia mtandao, kuwa makini na kutambua dalili za ukatili wa mtandaoni na kuwahamasisha kutoa taarifa wanapoona au kufanyiwa vitendo hivyo".

Akizungumzia hali ya ukatili mtandaoni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya mtoto Sebastian Kitiku amesema Serikali tayari imeunda kikosi kazi cha Taifa cha kuzuia ukatili wa watoto katika mtandao.

"Kikosi kazi hiki kinajumuisha wataalamu kutoka Serikali na Wadau na kinajadili mara kwa mara masuala ya ukatili kwa watoto na kuyashughulikia mara moja" amesema Kitiku.

Aidha ametoa nasaha kwa wazazi na watoto kukabiliana na ukatili mtandaoni kwa kuhakikisha wanaweka mipaka ikiwa ni pamoja na kuepuka kuwa waraibu wa mitandao hiyo hivyo kutoharibu malezi na makuzi yao.

Kwa upande wao watoto wa kike wakiwakilishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watoto Nancy Kasebo wamesema kaulimbiu ya mwaka huu inatambua kwa kiasi kikubwa ukuaji wa Matumizi ya Dijitali katika sekta zote muhimu.

"Sisi watoto tunashuhudia jitihada za Serikali za kuboresha miundombinu ya teknolojia, habari na mawasiliano inayokidhi viwango pia inatambua uwezo na ubora wa Mawasiliano katika kujifunza na ndiyo maana ikaanzisha Somo la Teknolojia ya habari" amesema Nancy.
 
Wamesema pamoja na mafanikio hayo ongezeko la Matumizi ya Dijitali yameambatana udhalilishaji wa watoto wa kike mtandaoni hivyo wameiomba Serikali iendelee kuboresha matumizi hayo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la bright Jamii Irene Fugara kwa niaba ya Wadau wa Maendeleo amesema wanatambua kuwa moja ya changamoto ni watoto wa kike kutokuwa na fursa sawa ya manufaa ya Teknolojia.

Ameongeza kuwa Wadau wataendeleza jitihada za Serikali za kuwasaidia watoto wa kike kuweza kufikia fursa hizo kwa kuwawezesha  kusoma masomo ya sayansi.

Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike mwaka huu imeadhimishwa Mkoani Dar es salaam ikiwa na Kauli mbiu isemayo " Kizazi Cha Kidijitali ni kizazi chetu".

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA