TCAA YAWAPIGA MSASA WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI KUHUSU MATUMIZI SAHIHI YA ARDHI KWENYE MAENEO YANAYOZUNGUKA VIWANJA VYA NDEGE NCHINI
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetoa elimu kwa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kuhusu matumizi sahihi ya ardhi kwenye maeneo yanayozunguka viwanja vya ndege nchini.
Elimu hiyo imetolewa na Mkaguzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege Tanzania Mhandisi. Bernard Kavishe kwa kupitia mada aliyoiwasilisha katika mkutano mkuu wa pili wa mwaka wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB)uliofanyika tarehe 07 mpaka 08 Oktoba, 2021 junguliwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa jijini Arusha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi,Mh. Waziri Mbarawa ameeleza kufurahishwa kwake na uwepo wa mada hiyo ambayo ana amini itakayowafumbua macho wadau hawa kuhusu matumizi bora ya rasilimali ardhi kuzunguka viwanja vya ndege.
Hafla hiyo ya ufunguzi ilihudhuriwa na viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Sofia Mjema na Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe.Frank Mwaisumbe.
“Sote ni mashahidi kuwa miaka ya hivi karibuni serikali imeamua kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege hivyo ni vyema sote tukawa na uelewa wa pamoja ili kulinda, kuepusha madhara na kufanya mipango endelevu ya sekta hii kwa pamoja” alisema Waziri Mbarawa.
Waziri Mbarawa amebainisha miongoni mwa matumizi hayo yasiyo sahihi ni pamoja na ujenzi holela wa minara na majengo marefu karibu na viwanja vya ndege ambayo yanakuwa ni vikwazo vya kiusalama katika shughuli za Usafiri wa Anga hususan ndege.
“Ni muhimu tukafahamu kuwa hata shughuli za kijamii zilizopo kwenye maeneo yanayozunguka viwanja vya ndege zinaweza kuathiriwa. Mfano, uwepo wa shughuli za shule na hospitali karibu kabisa na kiwanja cha ndege zinaathiriwa na kelele za milio ya ndege hivyo kusababisha usumbufu wakati mwingi”amesititiza Mhe.Mbarawa.
Aidha wa upande wake Mhandisi Kavishe ameongeza kuwa matumizi ya ardhi yasiyo sahihi yanaweza kuleta hatarishi ya ajali kwa ndege akitolea mfano uwepo wa jalala au madimbwi makubwa ya maji ni kivutio cha wanyama na makundi makubwa ya ndege ambapo kwa wingi wao wanapoivamia ndege ni hatari siyo tu inayoweza kuleta hitilafu kwenye ndege bali hata kusababisha ajali.
Ni wazi kuwa changamoto hii inakuwa kwa haraka na ni matoke ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ndio maana tuko hapa tupate uelewa wa pamoja ili wakati wa kupanga matumizi ya ardhi basi tujitahidi kuepuka kutengeneza athari zaidi alisema Mhandisi Kavishe.
Bodi ya Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) iliyoko chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inajukumu la kuratibu na kusimamia ujenzi kwa kusajili wataalam na makampuni ya ujenzi, kukagua miradi ya ujenzi na kutoa mafunzo kwa vitendo kwa watalaam wa ujenzi hapa nchini ambapo zaidi ya Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi 1520 wamesajiliwa.
0 comments:
Post a Comment