Wednesday 19 January 2022

Prof MBARAWA: "FANYENI KAZI KWA MALENGO ILI KUFIKIA TIJA"

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa watumishi wa taasisi za Wizara Mkoani Kigoma (hawapo pichani), alipokutana na kuzungumza nao wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani hapo.

Sehemu ya Mameneja wa Taasisi za Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, wakimsikiliza Waziri wa Wizara hiyo (hayupo pichani), alipokutana nao wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani Kigoma.

Muonekano wa hatua ya ujenzi wa barabara ya Chankere-Kagunga KM 45 barabara hiyo iko kwenye mipango ya Serikali ya kujengwa kwa kiwango cha Lami mkoani Kigoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Mwigulu Nchemba, akizungumza na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, walipotembelea barabara ya Chankere-Kagunga KM 45 kuangalia hali ya barabara hiyo, iliyopo Jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani Kigoma.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wakazi wa Mnanila, Wilayani Buhigwe, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo Mkoani Kigoma.

Mhandisi Mshauri, Mhandisi Tadesse Diriiba akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa barabara ya Kanyani-Mvuge KM 70.50 kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alipotembelea mradi huo Mkoani Kigoma.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa Mhandisi Mshauri Tadesse Diriba inayosimamia ujenzi wa barabara ya Kanyani-Mvuge KM 70.50 Mkoani Kigoma.

Muonekano wa hatua ya ujenzi wa barabara ya Mvugwe-Nduta KM 59.35 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Kasulu Mkoani Kigoma.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amewataka watumishi wa taasisi zilizo chini ya sekta ya ujenzi na uchukuzi kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ili kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali kwa wakati.

Akizungumza na wafanyakazi wa sekta za ujenzi na uchukuzi mjini  Kigoma Prof. Mbarawa amesema Serikali imetenga fedha nyingi kutekeleza miradi katika maeneo mbalimbali nchini hivyo kuwataka wafanyakazi hao kufanya kazi zinazopimika na zinazoleta tija kwa wananchi.

“Kila taasisi iliyo chini ya Wizara hii kuanzia sasa ijiwekee malengo yanayopimika na kutoa taarifa kwangu kila wakati ili kuacha kufanya kazi kwa mazoea, tunataka mabadiliko chanya kwa haraka,’ Amesisitiza Prof. Mbarawa.

Amezungumzia umuhimu wa taasisi zinazokusanya mapato katika huduma zake kuongeza mapato na kutoa huduma za viwango vya juu kwa wananchi huku akisisitiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), na Shirika la Reli Tanzania (TRC), zianze kubadilika.

Aidha, amewataka mamenenja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wanaosimamia viwanja visivyo na taa kuweka mikakati ya kuweka taa kwa kutumia fedha za ndani ili kuboresha utoaji wa huduma katika viwanja hivyo.

Amewataka watumishi hao kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali katika miradi yote nchini zinatumika kwa wakati na kuwiana na thamani ya miradi hiyo.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba wamekagua ujenzi wa barabara ya Chankere-Kagunga katika jimbo la Kigoma Kaskazini na kusisitiza barabara hiyo itajengwa ili kuweza kupitika wakati wote wa mwaka.

 “Tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 30 kuboresha barabara hii ambayo ni muhimu katika kukuza utalii katika hifadhi ya Gombe pia ni muhimu kwa usafirishaji wa bidhaa mbalimbali’ amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba amesema wizara yake itatoa fedha hususani kwa maeneo ambayo hayajafunguliwa toka uhuru ili kuwawezesha watanzania wote katika maeneo hayo kunufaika na matunda ya uhuru.

‘Mkoa wa Kigoma una uchumi mkubwa katika nyanja za kilimo na utalii hiyo tutashirikiana na wizara ya ujenzi na uchukuzi katika miradi ya barabara, reli, vivuko na meli ili kuufungua mkoa huo’ amesisitiza Dkt. Mwigulu.

Prof. Mbarawa pia amekagua ujenzi wa Barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa KM 260.6 inayojengwa kwa kiwango cha lami na kuwataka wakandarasi wote wanaojenga barabara hiyo kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuwa Serikali haitakubali visingizio.

‘Ujenzi wa barabara hii tumeugawa katika sehemu nne ili kurahisisha ujenzi wake hivyo hatutakubali visingizo vyovyote ambavyo vitajitokeza.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kigoma Mhandisi Narcis Choma amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kwamba pamoja na changamoto za mvua kasi ya ujenzi iliyofikiwa inaendana na muda hivyo ujenzi huo utakamilika kwa wakati.

Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu kukagua maendeleo ya miradi ya Wizara inayotekelezwa mkoani humo.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI, WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI.

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA