Showing posts with label ujenzi. Show all posts
Showing posts with label ujenzi. Show all posts

Monday, 16 May 2022

PROF. MBARAWA ASISITIZA UMUHIMU WA WATALAAM WA UJENZI KUJENGEWA UWEZO

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akisisitiza jambo katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Ujenzi lililofanyika mkoani Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Burian, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), (hawapo pichani) katika mkutano wao ulioanyika mkoani Tabora.
Naibu Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Bw. Ludovick Nduhiye, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Ujenzi, mkoani Tabora. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Burian na Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Bw. Eric Lengama.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Burian, Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Balozi, Eng. Aisha Amour, pamoja na viongozi wengine wa Baraza la Wafanyakazi wakiimba wimbo wa mshikamano katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika mkoani Tabora.
Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Balozi, Eng. Aisha Amour, akizungumza mbele ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, ambaye ni mgeni rasmi mara baada ya kufungua kikao cha Baraza la Wafanayakazi lililofanyika mkoani Tabora.
Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Balozi, Eng. Aisha Amour, akiteta jambo na Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta hiyo, Bw. Fanuel Muhoza, katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi, mkoani Tabora.
Katibu wa TUGHE Tawi la Sekta ya Ujenzi, Bw. Mussa Sillas, akiongoza wimbo wa mshikamano (Solidarity Forever), kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Ujenzi, mkoani Tabora.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Ujenzi, wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), mkoani Tabora.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Ujenzi, wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), mkoani Tabora.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Ujenzi, wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), mkoani Tabora.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesisitiza umuhimu wa watumishi wa (Sekta ya Ujenzi), kujengewa uwezo na ujuzi katika utekelezaji na usimamizi wa miradi inayoendelea ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Prof. Mbarawa amesema hayo mjini Tabora, wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekta hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza umuhimu wa wataalam wa usanifu wa barabara, madaraja na majengo kujiimarisha na kupata uzoefu ili kuboresha utendaji kazi na kupunguza gharama zinazoongezeka katika miradi kutokana na kukosewa kwa usanifu.

“Hakikisheni mnawapa ujuzi wa kutosha watalaamu wote ili waweze kuwa wabunifu, wanaojiamini na wenye uwezo mkubwa wa kusimamia miradi”, amesema Prof. Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa ameitaka Wizara pamoja na Wakala wa Barabara (TANROADS), kusimamia kwa karibu malalamiko katika vituo vya mizani ili kuhakikisha mizani zote nchini zinakuwa katika ubora wakati wote na kutoa huduma nzuri kwa wadau wa usafirishaji.

Amesisitiza umuhimu wa watumishi wa Sekta ya ujenzi kufanya mazoezi kila wakati ili kujiepusha na maradhi yasiyoambukizwa na hivyo kuwa na rasilimali watu kubwa yenye afya njema katika utekelezaji wa miradi.
Naye, Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo Balozi Eng. Aisha Amour, amemhakikisha Waziri Prof. Mbarawa kuwa watumishi wa Sekta hiyo wamejipanga kuhakikisha wanasimamia miradi yote ya ujenzi iliyopitishwa kwenye Bajeti kikamilifu na hivyo kufikia malengo yaliyopangwa na Wizara.

Balozi Aisha amesema wamejipanga kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wataalam ili kuwajengea uwezo wa kuendana na mabadiliko ya mara kwa mara ya teknolojia na hivyo kuleta tija na ufanisi mahali pa kazi.

Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Ujenzi pamoja na mambo mengine umepitisha rasimu ya bajeti ya Sekta hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Sunday, 1 May 2022

NAIBU WAZIRI KASEKENYA AKAGUA ATHARI ZA MIUNDOMBINU YA BARABARA SONGWE

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (aliyevaa kofia nyeusi) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Songwe, Mhandisi  Suleiman Bishanga, alipotembelea na kukagua barabara inayounganisha kata ya Isongole,Ibungu, Katengele,Lubanda kwenda Keikei, zilizopo wilaya ya Ileje, mkoani humo.

Baadhi ya Vijana wakitengeneza barabara ya dharula kwa ajili ya kupitisha magari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika kata ya Isongole na kuharibu miundombinu ya barabara,mkoani Songwe.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na Wananchi wa  kata ya Sange, Wilayani Ileje, mkoani Songwe, mara baada ya kukagua miundombinu ya barabara iliyoharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha Wilayani humo.



Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali imekata mawasiliano ya miundombinu ya barabara katika  eneo la Bujundo, Wilayani Ileje, mkoani Songwe, hali inayosababisha wakazi wa maeneo hayo kushindwa kupata huduma muhimu kama shule na hospitali.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amekagua athari zilizotokana na mvua hizo kwenye miundombinu ya barabara hiyo  ambayo imeharibika kufuatia magema kuporomoka  barabarani na kusababisha kufunga kwa barabara.

“Barabara hii inaunganisha wilaya ya ileje na wilaya ya Rugwe, na ndiyo barabara muhimu kwa mawasiliano baina ya Mikoa ya Songwe na Mbeya na eneo ambalo barabara hizi zimeharibika ni maeneo ya miinuko na kuna  maporomoko mengi sana kutokana na asili ya udongo wa eneo hili hasa katika kipindi cha mvua,”amefafanua Mhandisi Kasekenya.

Amesema kuwa Serikali itahakikisha maeneo yote yaliyopata athari za mvua yanarekebishwa kwa haraka ili shughuli za kibinadamu ziweze kurejea.

Aidha, Mhandisi kasekenya ametoa pole kwa familia zilizopata na maafa ikiwepo ya vifo vya wananchi watano, nyumba kubomoka, mazao kuharibika pamoja na mifugo kufa kutokana na kuporomokewa na udongo.

“Tunatoa pole kwa wananchi wote wa Wilaya ya Ileje na  vijiji vya Sange na kisesi, kwa kuwapoteza ndugu zao waliofariki pamoja na wengine waliopoteza mifugo, na mazao yao kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani,”amesema Mhandisi Kasekenya.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Songwe Mhandisi Suleimani Bishanga, amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya ndani ya wiki moja barabara na madaraja yaliyopata athari yataimarishwa na kuendelea kutumika.

Kwa upande wa wananchi wa wilaya ya ileje, wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuweza kuwasaidia kufungua barabara na madaraja yaliyoharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo ili waweze kuendelea na shughuli zao za kibinadamu.

Monday, 14 March 2022

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAKAGUA UJENZI WA KIWANDA CHA MATARUMA CHA SGR WILAYANI KISHAPU, MKOANI SHINYANGA


Mkurugenzi wa Miundombinu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Faustine Kataraiya, akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Selemani Kakoso (wa tatu Kulia) pamoja na wajumbe, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Kiwanda cha mataruma cha reli ya Kisasa ya SGR, Sehem



Meneja Mradi wa Mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR, Sehemu ya Mwanza-Isaka (KM 341), Mhandisi Masanja Machibya akifafanua kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Selemani Kakoso (Kulia) na wajumbe kuhusu Kiwanda cha mataruma cha reli ya Kisasa ya SGR kupitia michoro, kinachojengwa Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga, wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi huo mwishoni mwa wiki.



Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), wakati Kamati hiyo ilipotembelea Mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR, sehemu ya Mwanza-Isaka (KM 341) eneo la Seke, Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga.




Muonekano wa kipande cha Reli ya Kisasa ya SGR, Sehemu ya Mwanza-Isaka (KM 341) kilichotandikwa katika eneo la Seke, Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga.



Muonekano wa hatua za awali za ujenzi wa Kiwanda cha mataruma cha reli ya Kisasa ya SGR, kinachojengwa Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga. Kiwanda hicho ni sehemu ya mradi wa Mwanza-Isaka (KM 341) ambapo ujenzi wake mradi umefikia asilimia 4.






 

Tuesday, 8 March 2022

PROF. MBARAWA AWAFUNDA WADAU WA UJENZI WA BARABARA NA DARAJA LA PANGANI

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, mara baada kuzindua rasmi mradi wa ujenzi wa barabara ya Mkange-Tungamaa-Pangani yenye urefu wa kilomita 120.8 inayojengwa kwa kiwango cha Lami na daraja la Pangani lenye urefu wa Mita 525, uliofanyika jijini Tanga.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akimsikiliza Mkurugenzi wa Miundombinu wa Jumuiya Afrika Mashariki (EAC), Dkt. Kamugisha Kazaura kabla ya Uzinduzi rasmi mradi wa ujenzi wa barabara ya Mkange-Tungamaa-Pangani yenye urefu wa kilomita 120.8 inayojengewa kwa kiwango cha lami na daraja la Pangani lenye urefu wa Mita 525, uliofanyika jijini Tanga.

Sehemu ya Viongozi wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), wakimsikilisha Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani) wakati wa Uzinduzi rasmi mradi wa ujenzi wa barabara ya Mkange-Tungamaa-Pangani yenye urefu wa kilomita 120.8 inayojengwa kwa kiwango cha lami na daraja la Pangani lenye urefu wa Mita  525, uliofanyika jijini Tanga.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wadau mbalimbali wa Serikali wakati  wa Uzinduzi rasmi mradi wa ujenzi wa barabara ya Mkange-Tungamaa-Pangani yenye urefu wa kilomita 120.8 inayoejngwa kwa kiwango cha Lami na daraja la Pangani lenye urefu wa Mita 525, uliofanyika jijini Tanga.

Waziiri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Sekta ya Ujenzi, Mkoa wa Tanga na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) baada ya uzinduzi rasmi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mkange-Tungamaa-Pangani yenye urefu wa kilomita 120.8 inayojengwa kwa kiwango cha lami na daraja la Pangani lenye urefu wa Mita  525, uliofanyika jijini Tanga.


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amewataka wadau wote wanaoshiriki katika ujenzi wa mradi wa barabara  ya Mkange-Tungamaa-Pangani yenye urefu wa Kilomita 120.8  inayojengwa kwa kiwango cha lami na daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 kujenga uelewa wa pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano ili mradi huo uanze mara moja na kukamilika kwa wakati.

Akizugumza mara baada ya kuzindua rasmi warsha ya maandalizi ya ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni Prof. Mbarawa amesema wananchi wa mikoa ya Pwani na Tanga watanufaika wakati wa ujenzi na mradi huo utakapokamilika.

“Hakikisheni changamoto zote za fidia na uhamishaji wa miundombinu iliyopko katika hifadhi ya barabara inaondolewa mara moja ili kazi inapoanza kusiwe na malalamiko wala athari kwa wananchi “amesema Prof Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kutoa mkopo wa gharama nafuu utakaogharamia mradi huu na kuwataka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kusimamia kwa ukamilifu ili mradi ukamilike kulingana na mkataba.

Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Rogatus Mativila amesema ujenzi wa barabara  ya Mkange-Tungamaa hadi Pangani ni sehemu ya barabara kuu inayoanzia Malindi-Mombasa-Lungalunga-Horohoro-Tanga-Pangani hadi Bagamoyo yenye urefu wa KM 452 ambayo ni barabara ya Afrika Mashariki na taratibu zote za mradi huu zimekamilika.

Naye Muwakilishi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye ni Mkurugenzi wa Miudmbonu wa Jumuiya hiyo Dkt. Kamugisha Kazaura amesema  mradi huo ni wa kipaumbele katika Jumuiya kwakuwa utakuza bishara katika kanda na hivyo kukuza uchumi wa kanda kwa jumuiya hiyo na watu wake.

Dkt. Kazaura Amesema EAC itashirikiana kikamilifu na Nchi wanachama ili kuhakikisha miradi ya vipaumbele inafanikiwa ili kuchochea uchumi wan chi wanachama.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Aboubak Kunenge amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa maeneo ya mradi unapotekelezwa yatasimamiwa kikamilifu ili kukamilika kwa wakati na kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa za mradi huo.

Katika hatua nyingine amekagua mradi wa upanuzi wa bandari ya Tanga na kuutaka uongozi wa bandari mkoani humo kumsimamia mkandarasi kikamilifu ili upanuzi huo ukamilike kwa wakati.

Amesema upanuzi wa awali wa mita 150 na kina cha mita 14 unaofanywa na Kampuni ya China Harbour Enginering Company (CHEC) ukamilike ifikapo mwezi mei mwaka huu.

“Serikali imejipanga kufanya upanuzi wa mita 450 katika bandari ya Tanga ili kuifanya ya kisasa, hivyo hakikisheni mita 150 zinazojengwa sasa zinakamilika ili Kurusu shehena ya mizigo kuanza kushushwa na kupakiwa katika bandari hii’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. amesisitiza umuhimu wa TPA kuongeza wanafunzi walio katika mazoezi kwa vitendo kutoka vyuo mbalimbali ili kuwajengea uwezo kufuatia miradi  ya ujenzi inayotekelezwa nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Adam Malima amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa kufatilia kwa karibu maendeleo  ya miradi inayotekelezwa chini ya Wizara na kusema kukamilika kwa miradi ya barabara, bandari na madaraja kutahuisha uchumi wa Mkoa wa Tanga na watu wake kwa ujumla..

 

(IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI, WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI)}

Wednesday, 2 February 2022

TEMESA YATAKIWA KUZALIWA UPYA

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Balozi Aisha Amour, akitoa maelekezo kwa Mameneja wa TEMESA wa Mikoa (hawapo pichani), wakati wa kikao kazi chao, jijini Dodoma. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa TEMESA Bw. Lazaro Kilahala na kulia Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi, Bw Ludovick Nduhiye.


Baadhi ya Mameneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kutoka Mikoa mbalimbali nchini, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Balozi, Aisha Amour (hayupo pichani), katika kikao kazi chao, jijini Dodoma.


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Balozi Aisha Amour, ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), kujipanga upya ili kukidhi matarajio ya Taasisi hiyo kwa Serikali.

Akizungumza mara baada ya kukutana na Menejimenti na Mameneja wa TEMESA wa mikoa, Balozi Amour amewataka watendaji hao kuleta mabadiliko makubwa ya utendaji na hivyo kuvutia Taasisi za Serikali na wadau wote kutumia huduma za TEMESA.

“kila mtumishi awajibike kikamilifu kuanzia leo, boresheni huduma zenu na muangalie upya gharama za utengenezaji wa magari ili kuwavuta wateja wengi kutumia huduma zenu”, amesema Balozi Amour.

Amewataka TEMESA kutathimini upya gharama zao katika utengenezaji wa magari na kuhakikisha wanaboresha kitengo cha huduma kwa wateja.

Kuhusu vivuko amewataka Mameneja wanaosimamia vivuko nchini kuhakikisha vivuko hivyo vinatoa huduma bora na kwa wakati ili kuepuka udanganyifu katika ukusanyaji wa mapato. “Simamieni uadilifu wa watumishi wenu kwa kufuata taratibu, kanuni na miongozo katika mazingira yenu ya kazi”, amesisitiza Balozi Amour.

Aidha, amewataka watendaji wote wa Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Ujenzi kuthibiti utoro na kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao kwa wakati ili kuwajengea motisha ya kufanya kazi kwa bidii.

Naye Mtendaji Mkuu wa TEMESA Bw. Lazaro Kilahala, amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa TEMESA imeandaa mkakati wa mabadiliko utakaotekelezwa hivi karibuni ili kupunguza changamoto na malalamiko mengi kwa watumiaji wa huduma za TEMESA.

Amesema mkakati huo pia utawezesha wataalamu wa TEMESA kupata mafunzo ya mara mara ili kuwawezesha kumudu kutengeneza magari ya kisasa yanayotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu.

Katibu Mkuu Balozi Aisha Amour yupo katika ziara ya kukagua miradi na kukutana na watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Ujenzi, ambapo ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Bw. Ludovick Nduhiye.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Tuesday, 25 January 2022

BARABARA YA RUANGWA-NAGANGA KM 53 KUKAMILIKA NOVEMBA



Mmoja wa Wananchi wa Kata ya Nanganga, akimshukuru Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kwa  uamuzi wa Serikali wa kuijenga barabara Naganga-Ruangwa KM 53.2 kwa kiwango cha lami mkoani Lindi.



Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa wananchi wa Kata ya Naganga Mkoani Lindi, alipokagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Naganga-Ruangwa KM 53 kwa kiwango cha lami mkoani Lindi.



Eng. Simoni Makala akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alipokagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Naganga-Ruangwa KM 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Lindi. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoani humo Eng. Andrea Kasamwa akifuatilia.



Muonekano wa Barabara ya Naganga-Ruangwa Km 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Lindi.





Imeelezwa kuwa barabara ya Ruangwa-Nanganga yenye urefu wa KM 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Lindi itakamilika Novemba mwaka wa huu.

Barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara ya Nachingwea-Ruangwa-Nanganga yenye urefu wa KM 106 inatarajiwa kuufungua mkoa wa Lindi kiuchumi kwa kuwa itaunganisha Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Masasi kwa urahisi na hivyo kuhamasisha shughuli za maendeleo kwa wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Lindi Eng. Andrea Kasamwa amemweleza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo leo. 

Eng. Kasamwa amesema Ujenzi huo unahusisha ujenzi wa daraja  kubwa moja la Mto Lukuledi, makalvati makubwa 31 na makalvati madogo 68 ambayo yako katika hatua mbalimbali za ujenzi.


Kwa upande wake Waziri Prof. Mbarawa amesema zaidi ya shilingi bilioni 59 zinatarajiwa kutumika katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo sehemu ya Nanganga-Ruangwa hivyo kumtaka Msimamizi wa ujenzi huo kampuni ya TECU na wafanyakazi wa TANROADS mkoa wa Lindi kuhakikisha ujenzi wake unaendana na thamani ya fedha na kuharakisha usanifu wa kina kwa haraka sehemu iiliyobaki ya Nachingwea-Ruangwa KM 52.8.

Prof. Mbarawa amemtaka Msimamizi wa mradi huo TECU kuhakikisha anazingatia viwango vilivyokubaliwa katika  mkataba ili kuwezesha barabara kudumu kwa muda mrefu na kuchochea maendeleo ya wakazi wa mkoa wa Lindi.

“Barabara hii itapitisha mzigo mkubwa kuupeleka kwenye bandari ya Mtwara na maeneo mengine ya nchi hivyo simamieni kikamilifu na muweke alama zote za barabara zinazohitajika ikiwemo taa na alama za usalama barabarani” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Amemtaka Meneja TANROADS Mkoa wa Lindi kuhakikisha wananchi wanaelimishwa ili kupisha eneo la mradi na kumuwezesha Mkandarasi kufanya kazi na wananchi wenye malalamiko yapatiwe ufumbuzi kwa haraka.

Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu katika Mkoa wa LIndi kukagua miradi ya miundombinu ya Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

 

Sunday, 23 January 2022

BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA KUENDELEZA USHIRIKIANO UJENZI WA MIUNDOMBINU NCHINI



Waziri wa ujenzi na uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amekutana na Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB), Bw, Amos Cheptoo na kumhakikishia kuwa Tanzania itasimamia kikamilifu utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu yote inayopata fedha toka benki hiyo kwa kuzingatia thamani  ya fedha.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Waziri Prof Mbarawa amesema mazungumzo hayo yataongeza kasi ya utoaji fedha kutoka katika bank hiyo hasa kwa miradi ya viwanja vya Ndege ambayo imechelewa kutokana na changamoto mbalimbali. 

Ameitaja baadhi ya miradi inayoendelea kujengwa kupitia fedha za AfDB ni pamoja na barabara na viwanja vya ndege katika mikoa mbalimbali nchini.

"Tumejipanga kuunganisha mikoa yote ya Tanzania  na maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao kwa barabara za lami ill kukuza uchumu",amesema Prof. Mbarawa.

Mkurugenzi mtendaji huyo wa AfDB Bw, Cheptoo amesema benki hiyo  itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha adhma ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa hususan barabara na viwanja vya ndege inatekelezeka.

Baadhi ya miradi hiyo ni barabara za Kabingo-Kasulu-Manyovu km 260.6 km mkoani Kigoma, Mnivata-Newala-Masasi km 160 mkoani Mtwara na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma.

Friday, 21 January 2022

UJENZI WA DARAJA LA KITENGULE NA BARABARA UNGANISHI KUKAMILIKA MEI

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisiza jambo kwa Wasimamizi wa ujenzi wa Daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 40 alipokagua maendeleo ya ujenzi wake mkoani Kagera.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akiangalia mtambo wa kuunganisha mabomba katika shamba la Miwa la kiwanda cha sukari cha Kagera

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akishuka katika moja ya magari yanayotumika kuandaa mashamba ya miwa katika kiwanda cha sukari Kagera, alipokagua miundombinu ya barabara katika kiwanda hicho.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya awali katika Kiwanda cha Sukari mkoani Kagera, alipotembelea shule hiyo.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akimsikiliza Mhandisi Umwagiliaji  Neema Senyael  wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera, alipokagua miundombinu ya kiwanda hicho.

  

Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya daraja la Kitengule lenye urefu wa Mita 40 linalounganisha Wilaya za Misenyi na Karagwe, mkoani Kagera.

 


Imeelezwa kuwa kufanikiwa kwa miradi ya kiuchumi na uzalishaji katika mkoa wa Kagera kutategemea kukamilika kwa haraka kwa miundombinu ya barabara na madaraja mkoani humo.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema hayo alipokagua ujenzi wa daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 140 na barabara unganishi za daraja hilo zenye urefu wa KM 18.

Amesema kukamilika kwa darala hilo na barabara unganishi kutahuisha shughuli za kilimo, biashara na kuongeza uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha Kagera. 

“Kutokana na kazi kubwa inayofanyika hapa ya ujenzi wa daraja na barabara ni Dhahiri kutachangia uzalishaji mkubwa wa miwa na mazao mengine ya kilimo hivyo nakuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Kagera kuanza usanifu wa barabara hii sehemu iliyobaki ya Kitengule-Bunazi KM 24 ili kuziunganisha Wilaya za Misenyi na Karagwe kwa lami’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Amekipongeza kiwanda cha sukari cha Kagera kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya maji itakayokiwezesha kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.

Naye Meneja TANROADS mkoa wa Kagera Eng. Yudas Msangi amesema ujenzi wa daraja la Kitengule umesanifiwa kupitisha uzito wa tani mia moja na kwa sasa umefikia asilimia 90 kukamilika na barabara unganishi zenye urefu wa KM 18 zinatarajiwa kukamilika mwezi mei mwaka huu. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Sukari Kagera Bw. Seif Seif amesema Ujenzi wa daraja la Kitengule lenye urefu mita 40 na barabara unganishi zenye urefu wa KM 18 zinazounganisha Wilaya ya Misenyi na Karagwe ukikamilika utarahishisha kazi ya uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho na kuibua fursa nyingi za ajira ambapo tumejipanga kuongeza ukubwa wa mashamba ili kutatua changamoto ya upungufu wa sukari nchini.

Aidha, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara katika Wilaya za Misenyi na Karagwe na kusisitiza kwamba kiwanda hicho kitatoa ushirikiano wote unaohitajika katika kuhakikisha malengo ya Serikali katika kuongeza uzalishaji wa sukari, kutoa ajira kwa wahitimu wa kada zinazohitajika katika kiwanda hicho yanafikiwa kwa wakati.

Amesema kwa sasa kiwanda kinazalisha sukari tani elfu tisini na nne ila kutokana na kukamilika kwa miundombinu na daraja la Kitengule kunatoa fursa ya kuongeza mashamba na katika miaka mitatu ijayo kiwanda kimejipanga kuzalisha tani 170,000/- kwa mwaka.

Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Kanali Wilson Sakulu ameipongeza Serikali kwa kuziunganisha Wilaya ya Misenyi na Karagwe kwa barabara ya lami na daraja la uhakika kwani kutainua uchumi na kuongeza usalama kwa wakazi wa Wilaya hizo.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu kukagua maendeleo ya miradi ya Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi na kuhamasisha wadau wa mbalimbali kuibua fursa za uchumi mkoani Kagera.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI, WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI.

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA