TEMESA YATAKIWA KUZALIWA UPYA
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Balozi Aisha Amour, ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), kujipanga upya ili kukidhi matarajio ya Taasisi hiyo kwa Serikali.
Akizungumza mara baada ya kukutana na Menejimenti na Mameneja wa TEMESA wa mikoa, Balozi Amour amewataka watendaji hao kuleta mabadiliko makubwa ya utendaji na hivyo kuvutia Taasisi za Serikali na wadau wote kutumia huduma za TEMESA.
“kila mtumishi awajibike kikamilifu kuanzia leo, boresheni huduma zenu na muangalie upya gharama za utengenezaji wa magari ili kuwavuta wateja wengi kutumia huduma zenu”, amesema Balozi Amour.
Amewataka TEMESA kutathimini upya gharama zao katika utengenezaji wa magari na kuhakikisha wanaboresha kitengo cha huduma kwa wateja.
Kuhusu vivuko amewataka Mameneja wanaosimamia vivuko nchini kuhakikisha vivuko hivyo vinatoa huduma bora na kwa wakati ili kuepuka udanganyifu katika ukusanyaji wa mapato. “Simamieni uadilifu wa watumishi wenu kwa kufuata taratibu, kanuni na miongozo katika mazingira yenu ya kazi”, amesisitiza Balozi Amour.
Aidha, amewataka watendaji wote wa Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Ujenzi kuthibiti utoro na kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao kwa wakati ili kuwajengea motisha ya kufanya kazi kwa bidii.
Naye Mtendaji Mkuu wa TEMESA Bw. Lazaro Kilahala, amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa TEMESA imeandaa mkakati wa mabadiliko utakaotekelezwa hivi karibuni ili kupunguza changamoto na malalamiko mengi kwa watumiaji wa huduma za TEMESA.
Amesema mkakati huo pia utawezesha wataalamu wa TEMESA kupata mafunzo ya mara mara ili kuwawezesha kumudu kutengeneza magari ya kisasa yanayotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu.
Katibu Mkuu Balozi Aisha Amour yupo katika ziara ya kukagua miradi na kukutana na watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Ujenzi, ambapo ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Bw. Ludovick Nduhiye.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
0 comments:
Post a Comment