Showing posts with label TCAA. Show all posts
Showing posts with label TCAA. Show all posts

Friday, 4 September 2026

TCAA NA UMOJA WA ULAYA WATHIBITISHA DHAMIRA YA KUIMARISHA USIMAMIZI WA USALAMA WA USAFIRI WA ANGA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri K. Bakari, amethibitisha dhamira ya Mamlaka hiyo ya kujenga Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya kiwango cha kimataifa barani Afrika, yenye matarajio ya kufikia viwango vinavyolingana na mamlaka za usafiri wa anga za Ulaya katika ubora wa udhibiti, umahiri wa kitaalamu, ufanisi wa kiutendaji na usimamizi wa usalama wa anga.

Alitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha kuhitimisha ujumbe wa wataalamu wa msaada wa kujengeana uwezo kutoka Shirika la Usalama wa Anga la Umoja wa Ulaya (EASA), kilichofanyika tarehe 3 Septemba 2026 katika Makao Makuu ya TCAA jijini Dar es Salaam. Dkt. Bakari aliushukuru Umoja wa Ulaya kwa kuendelea kutoa msaada na kuonyesha imani katika maendeleo ya Tanzania. Pia alieleza juhudi zinazofanywa na TCAA kuimarisha mifumo yake ya usimamizi, ikiwemo uundaji na utekelezaji wa Mfumo wake wa ndani wa TCAA wa Huduma za Usafiri wa Anga (Civil Aviation Services Portal – CASP), ambao ulipewa pongezi na timu ya EASA.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri K. Bakari akizungumza   wakati wa kikao cha kuhitimisha ujumbe wa timu wataalam kutoka  Shirika la Usalama wa Anga la Umoja wa Ulaya (EASA)


Timu ya EASA ilieleza kuridhishwa kwake na maendeleo na juhudi zilizooneshwa na TCAA wakati wa ziara hiyo ya siku tatu. Aidha, timu hiyo ilitambua maendeleo yaliyofikiwa na kuhimiza TCAA kuendeleza kasi katika kushughulikia masuala yote muhimu ya usimamizi wa usalama wa anga.

Kwa upande wake Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya alithibitisha dhamira ya EU ya kuendelea kuisaidia Tanzania kupitia msaada wa kitaalamu, mbinu za utekelezaji wa vitendo na kubadilishana ujuzi. Aidha, alieleza kuwa Umoja wa Ulaya umetenga Euro milioni 2 kwa ajili ya msaada unaohusiana na kuboresha zaidi Masuala ya usafiri wa anga nchini. 




Kiongozi wa Ujumbe wa EASA Bw. Jose Miguel Manso Angulo akizungumza wakati wa kikao hicho

Ujumbe wa EASA uliongozwa na Bw. Jose Miguel Manso Angulo akiambatana na Bw. Gustavo Juan Roman Barba na Bw. Antonio Portales Pelaez.

Ujumbe huo, uliopo nchini kwa siku tatu kuanzia tarehe 1 hadi 3 Septemba 2026, ulifuatilia maendeleo ya Nchi (State) katika utekelezaji wa hatua za marekebisho pamoja na kuimarisha usimamizi wa usalama wa Usafiri wa anga. Majadiliano yalihusu maeneo ya ki sheria, muundo wa taasisi, uchunguzi wa ajali ndege, utoaji wa leseni kwa eneo la rasilimali watu la Usafiri wa anga, ubora wa ndege kwa matumizi (airworthiness) na uendeshaji wa ndege, pamoja na kufanya vikao na waendeshaji wa mashirika ya ndege kuhusu hoja zilizobainishwa, Mipango ya Hatua za Marekebisho (Corrective Action Plans) na ufuatiliaji wa utekelezaji wake.

Ujumbe huo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za Tanzania za kuimarisha usimamizi wa usalama wa Usafiri wa anga na kuonesha maendeleo endelevu kuelekea kutimiza matakwa ya kuondolewa kwenye Orodha ya Usalama wa Anga ya Umoja wa Ulaya (European Union Air Safety List).

Monday, 13 July 2026

TCAA KUWAHUDUMIA WATEJA WAKE KIMKAKATI

 Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau kupitia Dawati la Huduma kwa Wateja, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kupokea maoni na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haraka na kwa ufanisi.

Akizungumza katika Banda la TCAA kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa wa Dawati la Huduma kwa Wateja, Bw. Rashid Mngoya, alisema dawati hilo limeanzishwa ili kuwa kiungo kati ya Mamlaka na wananchi kwa kuwapatia taarifa sahihi kuhusu huduma mbalimbali za usafiri wa anga.

Alieleza kuwa kupitia dawati hilo, wadau wanaweza kuuliza maswali, kuwasilisha maoni, kutoa mapendekezo au changamoto wanazokutana nazo, pamoja na kupata mwongozo kuhusu taratibu mbalimbali zinazosimamiwa na TCAA.




Kwa mujibu wa Bw. Mngoya, uwepo wa dawati hilo unaimarisha mawasiliano kati ya TCAA na wateja wake, huku ukihakikisha hoja na malalamiko yanashughulikiwa kwa wakati ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.

Alisisitiza kuwa TCAA itaendelea kuboresha huduma zake kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa katika usalama, ulinzi na utoaji wa huduma bora kwa wadau wote wa sekta ya usafiri wa anga.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa TCAA, Bw. Ally Changwila, alisema Mamlaka imefanya maboresho mbalimbali katika mifumo yake ya mawasiliano ili kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi. Alitaja mojawapo ya maboresho hayo kuwa ni tovuti ya TCAA ambayo sasa inapatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, ikiwa na taarifa zilizoboreshwa na sehemu maalum ya Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs) ili kuwasaidia watumiaji kupata majibu ya haraka kuhusu huduma mbalimbali.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Sabasaba, TCAA inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake ya kiudhibiti, haki na wajibu wa abiria, matumizi salama ya ndege zisizo na rubani (drones), pamoja na huduma nyingine zinazohusiana na sekta ya usafiri wa anga.


Hatua hizi zinaonyesha dhamira ya TCAA ya kuendelea kuboresha huduma kwa wateja, kuimarisha mawasiliano na wadau na kuongeza uelewa wa umma kuhusu mchango wa Mamlaka katika kuhakikisha sekta ya usafiri wa anga nchini inaendelea kuwa salama, yenye ufanisi na kuendana na viwango vya kimataifa.

Sunday, 24 March 2024

TCAA YATOA MKONO WA PASAKA KITUO CHA KULELEA WATOTO CHA ZILI

 

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imekabidhi mahitaji kwa kituo cha kulea watoto cha ZILI kilichopo Kipawa Jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kurejesha kwa jamii inayowazunguka.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mahitaji hayo yaliyogharimu kiasi cha Shilingi (TSHS) Milioni Moja, Afisa Habari na Mawasiliano wa TCAA Bi. Maureen Swai amesema Mamlaka imeguswa kutoa mkono wa Pasaka kwa kituo hiki ambacho kinalea watoto kumi kwa sasa.

Mkurugenzi wa kituo cha ZILI Bw.  Emanuel Zadock ameishukuru TCAA kwa kuguswa kuwashika mkono wakati huu na kuwaomba wadau wengine kuendelea kuvishika mkono vituo vinavyowatunza watoto wenye mahitaji kwani ni baraka kubwa sana. 

Afisa Uhusiano na Mawasiliano - TCAA Maureen Peter Swai(kushoto) akikabidhi msaada kwa Mkurugenzi wa Kituo cha kulelea watoto cha Zili House Bw.  Emanuel Zadock (kulia) ikiwa ni kurudisha kwenye jamii kwakusambaza upendo na tabasamu kwa watoto yatima wa kituo hicho kilichopo eneo la Kipawa jijini Dar es Salaam. Msaada uliotolewa na TCAA ni mchele, Unga, mafuta ya kula, Taulo za Kike, sabuni, ngano nk.

Afisa Uhusiano na Mawasiliano - TCAA Bi. Maureen  Swai akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi msaada katika kituo cha kulelea watoto cha Zili ikiwa ni kurudisha kwenye jamii kwakusambaza upendo na tabasamu kwa watoto yatima wa kituo hicho hasa kwa kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka.
Mkurugenzi wa Kituo cha kulelea watoto cha Zili House Bw. Emanuel Zadock akizungumzia historia pamoja na kutoa shukrani kwa viongozi pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kuweza kutoa msaada kwenye kituo hicho kilichopo eneo la Kipawa jijini Dar es Salaam.
Dorethea  Daniel akitoa neno la shukrani wa viongozi pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kuweza kuwapatia msaada kituo hicho kilichopo eneo la Kipawa jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) pamoja na watoto  wakisikiliza historia ya Kituo cha kulelea watoto cha Zili House wakati wa hafla ya kutoa msaada  katika kituo hicho
 Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)  wakiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi wa Kituo cha Zili House pamoja na watoto wanaolelewa kwenye kituo hicho mara baada ya kukabidhi msaada ikiwa ni kurudisha kwenye jamii kwakusambaza upendo na tabasamu kwa watoto yatima wa kituo katika kituo hichokilichopo eneo la Kipawa jijini Dar es Salaam.

Friday, 29 December 2023

WASHINDI WA TCAA FUN RUN WAAGWA UWANJA WA NDEGE WA JNIA WAKIELEKEA DUBAI



Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini imeratibu zoezi la kuwaaga washindi watano wa mbio za kujifurahisha (FUN RUN) zilizofanyika Oktoba 29 jijini Dar es salaam zikiwa  sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 tangu kuundwa kwa TCAA.

Washindi hao walipata zawadi za tikteki kutoka kwa wadau wa Usafiri wa Anga ambao ni mashirika ya ndege ya Ethiopian Airlines, Kenya Airways na Fly Dubai ambapo wataelekea Dubai kwa mapumziko ya siku tano.
 
Akizungumza wakati wa kuwaaga, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya miaka 20 ya TCAA ambaye pia ni Meneja Mipango wa Mamlaka hiyo Bi. Mellania Kasese aliwapongeza washindi hao na kuyashukuru Mashirika yaliyotoa tiketi hizo kwa kutimiza ahadi hiyo na kuishukuru TCAA kwa kugharamia fedha za kujikimu kwa washindi hao wawapo katika mapumziko hayo.

"Ni siku ya sote kufurahia utimilifu wa zoezi hili kwa washindi wetu hawa watano ambao walipatikana miongoni mwa zaidi ya washiriki 300. Nawatakia safari njema na hii iendelee kuwa chachu ya kujali afya zenu lakini ikawe hamasa kwa wengine ili wajikite katika kuimarisha afya zao kwa mazoezi" alisema Mellania.

Meneja wa Shirika la Ndege la Ethiopia Bi. Seble Woldemariam amewapongeza washindi na kuwataka kutumia fursa hii kufanya utalii na kujifunza mengi mema na mazuri watakayojionea huko waendako. 



Meneja Mipango TCAA  Melania Kasese akizungumza na wanahabari wakati wa tukio la kuwaaga washindi wa TCAA FUN RUN waliojishindia tiketi za kuelekea Dubai ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)

Bw. Samuel Makalla mtumishi wa TCAA akielezea maandalizi aliyofanya kuelekea safari ya Dubai mara baada kuibuka mshindi  wa TCAA FUN RUN  kwenye Maadhimisho ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)

Mtumishi wa TCAA Bw. Aidan Adrian ambaye ni miongoni mwa washindi akitoa shukrani kwa wote waliofanikisha zoezi hilo wakati TCAA FUN RUN iliyofanyika katika maadhimisho ya Miaka 20 ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) iliyopelekea kutangazwa mshindi wa mashindano hayo.
Mtumishi wa LATRA  Bw. Lugano Mwasomola ambaye ni miongoni mwa washindi akitoa shukrani kwa wote waliofanikisha zoezi hilo pamoja nasafari hiyo ya kwenda Dubai wakati wa hafla ya kuondoka hapa nchini kuelekea Dubai.


Meneja wa Shirika la Ndege la Ethiopia Bi. Seble Woldemariam (katikati) akizungumza wakati wa kuwaaga washindi wa tiketi ya kuelekea Dubai ambapo Shirika hilo ni miongoni mwa wadau waliotoa tiketi moja wapo kwa mshindi.

Meneja Mipango kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Melania Kasese akiwa kwenye picha ya pamoja na  washindi wa tiketi ya kuelekea Dubai  pamoja na viongozi wa Shirika la Ndege la Ethiopia  pamoja na Emirate wakati wa kuondoka nchini kwa ajili ya kwenda kutembea Dubai.

Wednesday, 6 December 2023

TCAA YAIBUKA MSHINDI WA PILI NA KUPEWA TUZO YA UTENDAJI BORA WIZARA YA UCHUKUZI 2023


Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)  Bw. Hamza Johari tuzo ya mshindi wa pili ya kiutendaji miongoni mwa taasisi chini ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2023. 


Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)  Bw. Hamza Johari akifurahia tuzo ya mshindi wa pili ya kiutendaji miongoni mwa taasisi chini ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2023 mara baada ya kukabidhiwa.




Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)  Bw. Hamza Johari akiwa timu ya maonesho ya TCAA wakifurahia tuzo hiyo.


Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) yaibuka mshindi wa pili na kupokea tuzo ya kiutendaji miongoni mwa taasisi chini ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2023. 

Tuzo hiyo imekabidhiwa na Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akizindua Mkutano wa 16 wa Tathimini ya Utekelezaji katika Uchukuzi na Usafirishaji jijini Arusha na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari.

Thursday, 23 November 2023

WATUMISHI WA TCAA WAPONGEZWA KWA UTENDAJI KAZI KWA WELEDI




Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza S. Johari (katikati) akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TCAA wakati wa kufungua kikao hicho. Kulia ni Bi. Massa K. Mumburi Katibu Msaidizi wa Baraza, Kushoto ni Katibu wa Baraza Bw. Dedacus Mweya






Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Sara Rwezaula akitoa pongezi wakati wa kikao cha Baraza


Katibu wa Baraza Bw. Mweya Dedacus akiwasilisha mrejesho wakati wa Baraza


Afisa Uchunguzi, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Bw. Silvanus Njenga akiwasilisha mada kuhusu Maadili ya Utumishi wa Umma


Menejimenti ya TCAA ikifuatia wasilisho la maadili.





Wajumbe wa Baraza wakiendelea kufuatilia mada hiyo


Watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), wamepongezwa kwa kuendelea kufanya Baraza la Wafanyakazi lenye tija lililofanya mamuzi makubwa yenye tija kwa kutuoa huduma bora na kukuza sekta ya usafiri wa anga nchini.


Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari wakati wa ufunguzi wa Baraza la wafanyakazi la TCAA uliofanyika Novemba 23,2023 makao makuu ya Mamlaka Banana jijini Dar es salaam.


Bw. Johari  amewasifu wajumbe wa baraza kwa kufanya kuweka mbele maslahi ya taasisi na kuwasilisha hoja zinazoichochea menejimenti kutekeleza majukumu yake vyema. Pia ameongeza kuwa vikao hivyo vya Baraza ni njia bora ya kuimarisha demokrasia mahala pa kazi,na kuwataka wajumbe wa Baraza hilo kurudisha mrejesho kwa watumishi wenzao.


”Kama tunavyofahamu Mamlaka imetekeleza na inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ukiwemo wa Ununuzi wa Rada nne za kuongozea ndege, kuboresha Mfumo wa Masafa ya Mawasiliano wa Sauti baina ya rubani na waongozaji ndege katika vituo vyote vya kuongozea ndege nchini na Mradi wa kuimarisha na kuboresha utoaji taarifa za anga kuwa dijitali na yote hii ni mazao ya mawazo na hoja muhimu mnazoleta hapa na kwa pamoja tunapata ufumbuzi” alisema Bw. Johari.

Awali akiwasilisha salamu kwa niaba ya Chama cha Wafanyakazi Mkoa wa Dar es Salaam (TUGHE) Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Sara Rwezaula ameupongeza uongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania kwa kuteleza majukumu yake kwa namna shirikishi kwani inafanya kila mtumishi kujisikia sehemu ya Mamlaka na hivyo kuongeza ari ya utendaji kazi.

Akitoa maelezo ya jumla, Katibu wa Baraza hilo Bw. Mweya Dedacus amesema hichi ni kikao cha sita cha Baraza ambacho dhima kuu ni kuwasilisha mrejesho wa yale yaliyokuwa yamejadiliwa na kuazimiwa wakati wa kikao kilichopita cha Baraza kilichofanyika mwezi Aprili.

Monday, 25 September 2023

PICHA YA SIKU

 Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw.Hamza Johari (kushoto) akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara (kulia) wakati wakimsubiria Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ukaguzi wa maboresho ya uwanja wa Ndege wa Mtwara.

Friday, 22 September 2023

TANZANIA KUBORESHA MFUMO WA USIMAMIZI NA UTOAJI WA TAARIFA ZA ANGA 

 

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari (katikati) akisaini Kandarasi ya Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Taarifa za Anga na Kampuni ya Indra Avitech wenye thamani ya Tsh. Bilioni 9. Bw. Simon Masike alisaini kwa upande wa kampuni ya Indra Avitech. Hafla hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya TCAA Septemba 22, 2023.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesaini kandarasi ya mfumo wa usimamizi wa taarifa za anga na Kampuni ya Indra Avitech kwa ajili ya kuboresha usalama wa safari angani katika anga ya Tanzania kupitia utoaji wa taarifa za anga zenye ubora wa hali ya juu, salama na muhimu kwa wakati sahihi kwa wadau mbalimbali wa usafiri wa anga.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari leo Mamlaka hiyo imesaini mkataba wenye thamani ya Shilingi Bilioni Tisa kwa ajili ya kubuni, kusambaza, kusanikisha, kuunganisha, na kuzindua Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Anga ambapo Mradi huu utatekelezwa kwa miezi 18.

Amesema sehemu ya mpango thabiti wa Usimamizi wa Taarifa za Anga (AIM) wa kuboresha mfumo wake wa taarifa za anga kwa kutoa usimamizi wa taarifa za anga kwa njia ya kisasa zaidi kwa kutoa na kubadilishana taarifa za anga za dijitali zenye ubora na kushirikiana na pande zote hivyo kuhakikisha usalama, utaratibu, na ufanisi wa urambazaji wa anga wa kitaifa na kimataifa.

“Lengo la utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Anga ni kuboresha mfumo wa AIM katika kuboresha usahihi wa data, upatikanaji, na ufanisi kwa kuzingatia mahitaji ya Upandishaji wa Mfumo wa Anga wa Usafiri (ASBU), na kufuata viwango vya kitaifa na kimataifa.” Alisema Johari


Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari (katikati), Mkurugenzi Huduma za Sheria TCAA,  Maria Makala (wa pili kulia), Mwakilishi wa Kampuni ya Indra Avitech , Bw. Simon Masike(wa pili kushoto) wakisani Kandarasi ya Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Taarifa za Anga na Kampuni ya Indra Avitech wenye thamani ya Tsh. Bilioni 9 iliyofanyika Makao Makuu ya TCAA Septemba 22, 2023.



Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari (wa pili kushoto) akikabidhiana mkataba na Mwakilishi wa Kampuni ya Indra Avitech, Bw. Simon Masike mara baada ya kusaini Kandarasi ya Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Taarifa za Anga na Kampuni ya Indra Avitech wenye thamani ya Tsh. Bilioni 9 iliyofanyika Makao Makuu ya TCAA Septemba 22, 2023. Mkurugenzi Huduma za Sheria TCAA,  Maria Makala (wa pili kulia).

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari (katikati) pamoja na Mwakilishi wa Kampuni ya Indra Avitech, Bw. Simon Masike ( wa pili kushoto) wakionesha mkataba mara  baada ya kusaini Kandarasi ya Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Taarifa za Anga na Kampuni ya Indra Avitech wenye thamani ya Tsh. Bilioni 9 iliyofanyika Makao Makuu ya TCAA Septemba 22, 2023.Wa pili kulia ni Mkurugenzi Huduma za Sheria TCAA,  Maria Makala 

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari (katikati) akizungumza wakati wa kusaini Kandarasi ya Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Taarifa za Anga na Kampuni ya Indra Avitech wenye thamani ya Tsh. Bilioni 9 iliyofanyika Makao Makuu ya TCAA Septemba 22, 2023. 


Mwakilishi wa Kampuni ya Indra Avitech, Bw. Simon Masike  akizungumza wakati Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) waliposaini Kandarasi ya Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Taarifa za Anga na Kampuni ya Indra Avitech wenye thamani ya Tsh. Bilioni 9 iliyofanyika Makao Makuu ya TCAA Septemba 22, 2023. 


Kaimu Mkurugenzi Wa Huduma Za Uongozaji Ndege TCAA, Hamis Kisesa akizungumza wakati Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) waliposaini Kandarasi ya Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Taarifa za Anga na Kampuni ya Indra Avitech wenye thamani ya Tsh. Bilioni 9 iliyofanyika Makao Makuu ya TCAA Septemba 22, 2023.

Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Uchumi TCAA,Bw. Daniel Malanga(katikati), Mkurugenzi wa Huduma za Mamlaka Bw. Teophory Mbilinyi (kushoto) na Mkurugenzi Huduma za Sheria TCAA,  Maria Makala wakiwa kwenye hafla ya kusaini Kandarasi ya Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Taarifa za Anga. 

Meneja Uhusiano na Mawasiliano TCAA, Yessaya Mwakifulefule(kushoto), Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) kinachomilikiwa na TCAA, Aristid Kanje (katikati) na Afisa Mtoa Taarifa za Anga Mwandamizi (TCAA) wakiwa kwenye hafla ya kusaini Kandarasi ya Utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Taarifa za Anga. 

Baadhi ya wadau mbalimbali wa uSafiri wa anga wakiwa kwenye hafla ya kusaini Kandarasi ya Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Usimamizi na Utoaji wa Taarifa za Anga. 
Picha za pamoja 

 

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA