Monday 14 April 2014

Mafuriko Dar:Watu kumi wapoteza maisha

 
Mafuriko jijini Dar es Salaam
Watu kumi wamekufa, na mamia kukosa mahali pa kuishi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo, ambapo alisema kati ya watu hao kumi, watano ni watu wazima na watoto watano.

nyesha mfululizo kuanzia Ijumaa maeneo mbalimbali jini Dar es Salaam zimesababisha vifo hivyo na kuharibu miundombinu ya barabara yakiwemo madaraja sita kubomolewa na maji ya mvua hizo. Waandishi wa BBC jijini Dar es Salaam waliozunguka maeneo mbalimbali ya jiji hilo wameshuhudia uharibifu mkubwa wa miundombinu, mali na makaazi ya watu.
Daraja la Mpiji linalounganisha wilaya ya Kinondoni katika mkoa wa Dar es Salaam na Bagamoyo mkoa wa Pwani limekatika na kupoteza mawasiliano kati ya mikoa hiyo miwili.
Daraja jipya la Kawe jijini Dar es Salaam likizidiwa na mafuriko
Waziri wa Ujenzi, Dr. John Magufuli alifika Jumamosi katika eneo la tukio na kusema serikali italifunga daraja hilo kwa siku mbili wakati kazi ya ukarabati ikifanyika ili kuharakisha urejeshaji wa mawasiliano kati ya mikoa hiyo.
Watu walioathirika zaidi kutokana na mafuriko hayo ni watu waliojenga mabondeni, hasa maeneo ya Jangwani, na bonde lote la mto Msimbazi.
Wakaazi hawa ambao mara kwa mara hukumbwa na kadhia hii hata pale mvua ndogo zinaponyesha, hali ya sasa imekuwa tishio zaidi kwa maisha yao na mali, huku mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadiq Meck Sadiq akisema serikali haitaweza kuendelea kuwasaidia waathirika hawa, ambao wanapuuza wito unaotolewa mara kwa mara kuwataka kuyahama maeneo hayo hatarishi, na wengine hata kwenda mahakamani kupinga amri ya kuwataka kuhama.
Eneo la Jwangwani jijini Dar es Salaam likiwa limefurika maji
Mwaka 2012, serikali ya mkoa wa Dar es Salaam iliwataka wakaazi wa bonde la Jangwani waliokuwa wameathiriwa na mafuriko kuhamia katika maeneo salama likiwemo eneo la Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ambako waligawiwa viwanja.
Hata hivyo baadhi yao waligoma kuhama na wale waliohama wanadaiwa wengine walivitelekeza viwanja walivyogawiwa na kurejea katika maeneo yao ya mabondeni.
Mradi mwingine muhimu wa Mabasi yaendayo kasi, DART unaolenga kutatua tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam, nao umeathiriwa na mvua zinazonyesha na kusababisha hasara ya kiasi cha dola elfu thelathini za Kimarekani kutokana na magari yake matatu kuharibiwa pamoja na mashine nyingine na mifuko ya saruji kuchukuliwa na maji hivyo kusitisha shughuli zake za ujenzi zilizo katika hatua za mwisho kukamilika kwa barabara ya Mbezi hadi Kivukoni katikati ya jiji.
Picha ya anga ya mafuriko Dar es Salaam
Mvua zilizoripotiwa kunyesha kote nchini zimesababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali ukiwemo mkoa wa Morogoro uliopo magharibi mwa mkoa wa Dar es Salaam.
Mpaka sasa mkoa wa Dar es Salaam umeripotiwa kukosa mawasiliano na mikoa mingine kutokana na kuharibika kwa miundombinu ya barabara na reli.
Wakati huo huo makamu wa Rais, Dokta Mohammed Gharib Bilal, akiwa pamoja na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadiq Meck Sadiq na kamanda wa polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova wamenusurika katika ajali ya helikopta wakati wakikagua athari za mafuriko katika mkoa wa Dar es Salaam.
Habari zinasema walipata majeraha kidogo na kuendelea na shughuli za kukagua maeneo ya mafuriko katika mkoa wa Pwani.
na BBC

0 comments:

Post a Comment

OFFICIAL MEMBER

OFFICIAL MEMBER

Please Share This Site

HABARI ZETU

LIKE PAGE YETU HAPA